DKT. KIRUSWA : GGML INAIBEBA GEITA, WIZARA YA MADINI KUTAFSIRI VYEMA MABORESHO SHERIA YA MADINI


Naibu Waziri wa Madini, Dk.Stephen Kiruswa, akizungumza na wafanyakazi wa kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) alipotembelea banda la kampuni hiyo katika maonesho ya Jukwaa la Pili la Utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini jiji Arusha. (Kushoto) ni Wakili Mwandamizi wa Sheria wa GGML, David Nzaligo na wengine ni maofisa waandamizi kutoka Madini.
Naibu Waziri wa Madini, Dk.Stephen Kiruswa akipokea zawadi kutoka kwa Meneja Mawasiliano wa kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML), Stephen Mhando (kulia) alipotembelea banda la kampuni hiyo katika maonesho ya Jukwaa la Pili la Utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini jiji Arusha. Kushoto ni maofisa waandamizi kutoka Madini.


*******
NAIBU Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa amesema mojawapo ya kampuni za madini zinazoongoza nchini kwa kutafsiri na kutekeleza vyema matakwa ya Sheria ya Madini iliyofanyiwa maboresho mwaka 2017, ni kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) ambayo mbali na kuinufaisha jamii inayozunguka mgodi huo, pia imeupatia sifa za kipekee mkoa wa Geita na wizara ya madini kwa ujumla.


Dkt. Kiruswa ametoa kauli hiyo alipotembelea banda la GGML katika maonesho ya Jukwaa la Pili la Utekelezaji wa Ushirikishwaji wa Watanzania katika Sekta ya Madini jijini Arusha.


Jukwaa hilo lilikutanisha kampuni za uchimbaji wa madini, watoa huduma wa madini kwenye migodi ya madini na taasisi za kifedha.


Amesema GGML imetekeleza vyema matakwa ya sheria hiyo mathalani katika utoaji wa huduma kwenye jamii unaofanywa na migodi ya madini (CSR).


Katika utekelezaji wa mpango huo wa CSR, Mwanasheria Mkuu wa Kampuni uya Geita Gold Mining Limited (GGML) David Nzaligo alimueleza Dkt. Kiruswa kwamba kila mwaka kampuni hiyo hutenga zaidi ya Shilingi bilioni tisa ambazo hutekeleza miradi mbalimbali ya kijamii chini ya usimamizi wa halmshauri na wilaya za mkoa wa Geita.


Aidha, Dkt. Kiruswa amesema mafanikio ya maboresho ya sheria ya madini yaliyopelekea kutungwa kwa kanuni za ushirikishwaji wa watanzania katika sekta ya madini, yalichochea ongezeko la fursa mbalimbali katika nafasi za ajira na mafunzo, uhaulishaji wa teknolojia, utafiti na maendeleo, matumizi ya huduma na bidhaa zinazotolewa na kuzalishwa na watanzania.


Akizungumzia mfumo wa ushirikishwaji wa watanzania katika sekta ya madini (Local Content), Dk. Kiruswa amesema mfumo utawezesha kampuni za uchimbaji wa madini na watoa huduma kwenye migodi ya madini kuwasilisha nyaraka mbalimbali kwenye mfumo huo kwa njia ya kieletroniki badala ya kutumia nakala ngumu kama ilivyokuwa ikifanyika awali.


Hata hivyo, kampuni hiyo ya GGML katika utekelezaji wa mfumo huo, imetoa zabuni kwa kampuni za ndani katika utoaji wa huduma mbalimbali ikiwamo usafirishaji kwa kampuni ya Blue Coast ambayo inamilikiwa na mtanzania.


Kuhusu ajira, Dk. Kiruswa amefafanua kuwa watanzania katika migodi mikubwa zimeongezeka kutoka 6,668 mwaka 2018 hadi kufikia 15,341 mwaka 2022.


Kwa upande wa GGML katika eneo hilo la ajira hadi sasa imeajiri zaidi ya wafanyakazi 2,249 na wakandarasi 4,152 ambao asilimia 97 ni raia wa Tanzania.

Pamoja na mambo mengine, Dkt. Kiruswa amesema sheria hiyo imesaidia kuongeza manunuzi ya ndani ya nchi ambapo mwaka 2022 jumla ya Dola za Kimarekani bilioni 2.22 sawa na asilimia 97.4 ya manunuzi yote ya kampuni za madini yalifanyika kwa kutumia kampuni za watanzania, ukilinganisha na Dola za Kimarekani milioni 238.71 sawa na asilimia 46 ya manunuzi yote kwa mwaka 2018 kutumika.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments