MFAHAMU ASKOFU CHITETO ALIYEFARIKI BAADA YA MAHUBIRI MSIBANI


MFAHAMU KWA UFUPI MAREHEMU ASKOFU CANON, CAPT, GEORGE YORAM CHITETO, DAYOSISI YA MPWAPWA KANISA ANGLIKANA TANZANIA

 Na Maiko Luoga +255 762 705 839

Mhashamu Baba Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania na Dayosisi ya Tanga Maimbo Mndolwa, kwa masikitiko amewajulisha Waumini wa Dayosisi ya Mpwapwa na Tanzania kwa ujumla Taarifa za kifo cha CAPT. GEORGE YORAM CHITETO, Askofu wa Kanisa Anglikana Tanzania, Dayosisi ya Mpwapwa kilichotokea Septemba 03, 2022.

Askofu Chiteto alifariki Dunia muda mfupi baada ya kutoa Mahubiri katika Misa ya kuaga mwili wa Hilda Lugendo aliyekuwa Mwenyekiti wa Taifa wa Ushirika wa Mama wa Kikristo (UMAKI), Kanisa Anglikana Tanzania, iliyo fanyika katika Kanisa Anglikana Kristo Mfalme Muheza Dayosisi ya Tanga.

Katika Mahubiri yake Askofu Chiteto alitembea na ujumbe wenye kichwa cha neno uliosema JITAHIDI KUINGIA, alifafanua ujumbe huo kutoka Kitabu cha Injili kama alivyoiandika Luka Mtakatifu sura ya 13 aya ya 24 inayoeleza “Jitahidini kuingia katika mlango ulio mwembamba kwa maana wengi watatamani kuingia lakini hawataweza” 

Kupitia ujumbe huo aliwashauri Wakristo kufanya bidi ya kumtumikia Mungu ili kujijengea heshima au hadhi mbele za Mungu ili wanapomaliza kazi na kufariki Dunia, Mungu awapokee katika ufalme wa Mbingu, 

Aidha alitoa mfano wa Mama mmoja aliyekuwa akiuugua na kuweweseka katika hatua za mwisho za kufariki ndipo Askofu Chiteto alialikwa kwenda kumfanyia maombi alipofika hapo alimwambia mama huyo kuwa aseme japo neno moja la kutubu kwa Mungu ili aweze kuingia katika mlango mwembamba lakini Mama huyo hakutaka kutubu hadi alipofariki Dunia.

“Nilipofika Hospital mama yule alikuwa anahangaika anawaambia Madakitari kuwa anaona giza anawataka wafungue mapazia, mimi nilipofika nilimwambia Mama ebu sema japo neno moja la kutubu ili Mungu akusamehe uingie mbinguni lakini hakutaka akaishia kunitukana hadi alipofariki katika mazingira hayo ya kutukana”

Alitoa mfano wa pili akimzungumzia kijana mwimbaji wa Kwaya ambae alienda kumuongoza maombi kuwa Kijana huyo alimweleza Askofu Chiteto kuwa anaona mlango umefunguka malaika wanapanda na kushuka na Yesu amesimama pembeni kisha Kijana huyo akafumba macho na kufariki Dunia hivyo alisema anaamini Kijana huyo alikufa kifo kizuri.

“Niliona kijana yule ana hadhi kubwa, mimi palepale nikasema na Mungu kifo changu kiwe hivihivi yaani isibadilike hata sentesi moja, yaani unapokuja kuniita mlango uwe umefunguka sio kusema fungua fungua, Tujiulize sote kama tuna hadhi au wenye hadhi ni wachache?” alihoji Askofu George Chiteto dakika chache kabla ya kufariki Dunia.
  
Mara baada ya kumaliza kutoa mahubiri kwenye Ibada hiyo, Dakika chache baadae Askofu Chiteto Alijisikia vibaya na kukimbizwa Hospitali Teule ya Wilaya ya Muheza  mkoani Tanga ambapo alifariki Dunia wakati jitihada za kuokoa uhai wake zikiendelea, Taarifa ya kifo chake ilithibitishwa na Madaktari kwa Askofu Mkuu ambae aliwatangazia waumini Msiba huo.
 
Marehemu Askofu CAPT. GEORGE YORAM CHITETO aliwekwa wakfu na kuwekwa kitini kuwa Askofu wa Dayosisi ya Mpwapwa, Kanisa Anglikana Tanzania siku ya BWANA ya tarehe 28 Agosti mwaka huu 2022 katika Kanisa la Watakatifu wote Mpwapwa. 

Alizaliwa tarehe 7 Desemba, mwaka 1962 katika kijiji cha Inzomvu Wilaya ya Mpwapwa, Alisoma shule ya msingi Inzomvu mwaka 1975 hadi mwaka 1981, Baada ya hapo akajiunga na Chuo cha Maendeleo ya Jamii Chisalu kwa kozi ya Kilimo na ufugaji mwaka 1981, Mwaka 1984 – 1985 alijiunga na Chuo cha Jeshi la Kanisa (Church Army) Nairobi nchini Kenya. 

Mwaka 1987 aliamuriwa kwa daraja la Ushemasi akatumika katika daraja hilo kwa muda wa mwaka mmoja, mwaka 1988 aliamuriwa daraja la Ukasisi, Mwaka 1994 alijiunga na Chuo cha Mt. Filipo Kongwa kwa kozi ya Stashahada ya Theologia na kuhitimu mwaka 1996. 

Mwaka 2005 alijiunga na Chuo kikuu cha Gloucestershire kwa kozi ya Stashahada ya juu, Mwaka 2007-2010 alijiunga na Chuo Kikuu cha Mt. Yohana Dodoma na kuhitimu katika Shahada ya Sanaa ya Theologia na Elimu, Mwaka 2010 – 2011 alihitimu katika Shahada ya Uzamili ya Sanaa katika Theologia kutoka Chuo cha Mtakatifu Yohana. 

Askofu George Yoram Chiteto ameacha mke Mama Monica Chiteto na watoto sita, Ibada ya kuaga mwili wake itafanyika Septemba 05, 2022 kuanzia saa nane mchana katika Kanisa Anglikana Madaba – Muheza kisha siku hiyo jioni safari itaanza kutoka Muheza Mkoani Tanga kuelekea Mpwapwa mkoani Dodoma kwaajili ya mazishi yatakayofanyika siku ya tarehe 7 Septemba, mwaka huu 2022.

Enzi za uhai wake Askofu George Chiteto atakumbukwa zaidi kwa utumishi wake uliotukuka ndani ya Kanisa akipita katika maeneo ya mjini na Vijijini akihubiri na kuwaokoa wengi walio mkiri Yesu kuwa Bwana na mwokozi wao kupitia utumishi wa Marehemu Askofu Chiteto.

Pia atakumbukwa zaidi kwa Hotuba yake nzuri aliyoitoa agosti 28, 2022 mbele ya Mgeni Rasmi Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Bunge na Utaratibu George Simbachawene aliye mwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa kushiriki tukio hilo ambalo baada ya kuwekwa Wakfu Askofu Chiteto amehudumu kama Askofu wa Dayosisi ya Mpwapwa kwa muda wa siku sita pekee.

Katika Ibada hiyo ya kuwekwa Wakfu Marehemu George Chiteto kuwa Askofu wa tatu wa Dayosisi ya Mpapwa ilifanyika Changizo dogo iliyoongozwa na Waziri Simbachawene ya kupata fedha ili kufanikisha ununuzi wa Gari la Askofu na jumla ya Shilingi milioni 21 zilipatikana ambazo ni ahadi pamoja na fedha taslimu na zoezi hilo linaendelea.

Kufuatia Msiba huo Wakristo wa Kanisa Anglikana Dayosisi ya Mpwapwa na Tanzania kwa ujumla wameeleza kupokea msiba huo kwa mshituko na masikitiko makubwa kwakuwa Askofu hakuonesha hali ya ugonjwa hadi alipofariki Ghafla baada ya kumaliza kazi ya kuwahubiria waumini.

“Tumesikitishwa na tukio hili la kifo cha Baba Askofu maana alikuwa mzima, amehubiri hapa Kanisani tumependa mahubiri yake wengi tumefurahi na kushangilia lakini ghafla tukaona anatolewa nje na kukimbizwa Hospitali, mwishoni wa ibada Baba Askofu Mkuu alitangaza taarifa za kifo chake tumeumia sana” walieleza.
   
Kanisa linatoa pole kwa familia ya Baba Askofu Chiteto, mkewe na watoto, wahudumu na Wakristo wote wa Dayosisi ya Mpwapwa na Kanisa Anglikana Tanzania, Raha ya Milele umjalie Ee Bwana, na Mwanga wa Daima umwangazie. Roho ya Baba Askofu CAPT. GEORGE YORAM CHITETO na roho zao wote waaminifu waliofariki katika imani zipumzike kwa Amani. Amen.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments