MAAFISA AFYA,MAAFISA BIASHARA WAFUNDWA UDHIBITI WA USALAMA WA VYAKULA NA VIPODOZI


Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya udhiti wa usalama wa vyakula na vipodozo kutoka halmashauri za mkoa Kigoma wakiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi wa serikali mkoa Kigoma na watendaji wa ngazi ya Juu wa Shirika la Viwango nchini (TBS). (Picha na Fadhili Abdallah)
Meneja utafiti na mafunzo kutoka TBS, Hamisi Sudi (kushoto aliyesimama) akizungumza wakati wa mafunzo kwa maafisa afya na maafisa biashara wa halmashauri za mkoa Kigoma kuhusu udhibiti wa usalama wa chakula na vipodozi.
Benedicto Mwalyambi (kulia) Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji sekretariet ya mkoa Kigoma akifungua mafunzo kwa maafisa afya na maafisa biashara wa halmashauri za mkoa Kigoma kujengewa uwezo juu ya usimamizi wa usalama wa vyakula na vipodozi katika mafunzo yanayoendeshwa na Shirika la viwango nchini (TBS)

Na Fadhili Abdallah,Kigoma

SHIRIKA la viwango nchini (TBS) limesema kuwa mafunzo yanayoendelea kutolewa na shirika hilo kwa maafisa afya na maafisa biashara wa halmashauri kwenye mikoa mbalimbali nchini yataimarisha usimamizi wa sheria na taratibu za kiutendaji zinazopaswa kufuatwa na wazalishaji na wauzaji wa bidhaa za chakula na vipodozi nchini na kuondoa migongano inayoweza kujitokeza.

Meneja utafiti na mafunzo kutoka TBS, Hamisi Sudi akizungumza wakati wa mafunzo kwa watendaji hao mjini Kigoma ambapo alisema kuwa mafunzo hayo yanakuja ikiwa sehemu ya mkataba wa ushirikiano baina ya Wizara ya Biashara na Wizara ya Tawala za mikoa na serikali za mitaa ili usimamizi wa sheria na kanuni zieleweke bayana na kuondoa migongano kweye utekelezaji wake.

Alisema kuwa katika muundo wa sasa ambapo baadhi ya shughuli zilizokuwa zikifanywa na Mamlaka ya chakula na dawa (TFDA) ambayo kwa sasa inafahamika kama Mamlaka ya udhibiti wa dawa na vifaa tiba (TMDA) zimehamishiwa TBS hivyo kuongeza majukumu ya kiutendaji hivyo mafunzo hayo yanalenga kuwatumia maafisa wa halmashauri kusaidia kusimamia utekelezaji wa majukumu hayo.

Sudi alisema kuwa Sheria namba nane ya fedha ya mwaka 2019 ya kuimarisha usalama na udhibiti wa bidhaa za vyakula na vipodozi pamoja na usajili wa bidhaa hizo, majengo ambayo yanatumiwa kuzalisha au kuuza jukumu ambalo shirika hilo halina idadi ya kutosha ya kusimamia na hivyo kutumia maafisa biashara na maafisa afya katika halmashauri kusimamia utekelezaji wa majukumu hayo.

Ofisa Ukaguzi kutoka TBS makao makuu Baraka Mbajije ambaye ni mratibu wa mafunzo hayo alisema kuwa jambo kubwa ambalo wanalifanya ni kufundisha kanuni za usimamizi kwa watendaji wa halmashauri wanaosimamia jukumu la usimamizi wa usalama wa chakula na vipodozi na nyongeza ya majukumu baada ya baadhi ya majukumu ya TFDA kuhamishiwa TBS.

Kwa upande wake Afisa biashara kutoka sekretariet ya mkoa Kigoma,Omari Ndimuligo alisema kuwa mafunzo hayo kwao ni muhimu katika kujua sheria,taratinu na miongozi katika kusimamia jukumu walilopewa la kusimamia udhibiti wa usalama wa vyakula na vipodozi.

Ndimuligo alisema kuwa ni jambo jema kujua vizuri sheria hiyo ili isitokee migongano na kuonekana wanawaonea wafanyabiashara hasa suala la kuteketeza bidhaa vya vyakula na vipodozi ambazo hazina viwango, zilizopigwa marufuku na ambazo ni hatari kwa maisha ya binadamu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments