JAFO ASISITIZA NCHI ZILIZOENDELEA KUTIMIZA WAJIBU WAO


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo akizungumza na Katibu Mkuu wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Prof. Petteri Taalas katika moja ya mikutano inayoendelea Glasgow Scotland. Mazungumzo yao yamejikita katika njia bora za kuhimili mabadiliko ya Tabianchi ambayo ni tatizo kubwa kwa sasa duniani. Kutoka kulia wa nne ni Mhe. Saada Mkuya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais – Zanzibar, Dkt. Agnes Kijazi, Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (kushoto) na Wakurugenzi wa Mazingira kutoka Zanzibar Bi. Farhat Mbarouk na Dkt. Andrew Komba kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo akifafanua jambo kwa Katibu Mkuu wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Prof. Petteri Taalas katika moja ya mikutano inayoendelea Glasgow Scotland. Kulia ni Mhe. Saada Mkuya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais – Zanzibar na Dkt. Agnes Kijazi, Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (kushoto)


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa 26 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi unaoendelea Glasgow, Uingereza. Kutoka kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Uingereza Dkt. Asha Rose Migiro, Mhe. Saada Mkuya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais – Zanzibar, Balozi Prof. Gastorn Kennedy Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa na Bw. Kamran Fazil Mkurugenzi wa Eco Village

********************************

Na Mwandishi wetu, Glasgow, Scotland

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Selemani Jafo amesema Athari za mabadiliko ya Tabianchi zinaonekana dhahiri katika maeneo mbalimbali nchini na kusema kuwa ipo haja ya kuongeza jitihada za dhati katika kukabiliana nayo.

Waziri Jafo ameyasema hayo hii leo mjini Glasgow Scotland katika Mkutano wa 26 wa Nchi wa Wanachama wa Mkataba wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi.

Amezitaja athari hizo kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa kina cha maji ya bahari kulikosababisha kisiwa cha Maziwe Wilaya ya Pangani na kisiwa cha Fungu la Nyani Wilaya ya Rufiji kumezwa na maji ya bahari na kuongezeka kwa kina cha maji kwenye Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika.

“Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi Ili kukabiliana na athari hizi ambazo zinatishia kurudisha nyuma juhudi za serikali za miongo kadhaa za kukuza uchumi na kuleta maendeleo kwa watu wake” Jafo alisisitiza.

Amesisitiza kuwa katika mkutano unaoendea viongozi wa mataifa makubwa ambayo kwa kiasi kikubwa mataifa yao ndio chanzo cha uzalishaji wa hewa ya ukaa wameonyesha nia ya dhati ya kutekeleza makubaliano waliojiwekea ya kutoa fedha kwa wakati ili kutekeleza miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi.

Amesema mataifa hayo yanawajibika kutokana na makubaliano ya Mkataba wa Paris ambao unazitaka nchi zilizoendelea kutoa kiasi cha Dola Bilioni Mia moja kila mwaka kwa nchi zinazoendelea ili ziweze kukabiliana na athari za Mabadiliko ya Tabianchi.

“Tunadhamiria na kusisitiza kuwa sasa tutoke kwenye maneno na twende kwenye vitendo, wenye jukumu la kutoa fedha watoe ili miradi mbalimbali ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi iweze kutekelezeka kwa wakati” Jafo alisisitiza.

Waziri Jafo amesema katika kuungana na Jumuiya ya Kimataifa kupunguza uzalishaji wa gesijoto, Tanzania pia imechukua hatua stahiki zikiwemo Kuandaa Mpango wa Taifa wa Kupunguza Gesijoto (2021 - 2026); Kuimarisha usimamizi wa misitu na program za upandaji miti; kuendelea na ujenzi wa Mradi wa umeme wa Bwawa la Mwl Nyerere; Ujenzi wa Reli ya kisasa; kuanza kutumika kwa gesi majumbani na kwenye uendeshaji wa mitambo viwandani na kwenye magari badala ya dizeli na petroli na Mfumo wa usafiri wa mabasi yaendayo kasi katika jiji la Dar es salaam ambavyo vinachangia kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa.

Nae Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa kwanza Rais (Zanzibar) Dkt. Saada Mkuya amesema athari za mabadiliko ya tabianchi ni kubwa kwa upande wa Zanzibar kutokana na kuongezeka kwa kina cha bahari na kusabisha baadhi ya visiwa kutoweka na baadhi ya maeneo ya ardhi kuingiwa na maji chumvi na kuathiri shughuli za uzalishaji hususan kilimo na uvuvi hivyo kuathiri uchumi.

Awali Waziri Jafo na Waziri Dkt. Saada Mkuya wamekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Prof.Petteri Taalas na kuzungumzia masuala ya kuhimili mabadiliko ya Tabianchi ambayo ni changamoto kubwa kwa sasa duniani.

Mkutano wa 26 wa Nchi wa wanachama wa Mkataba wa Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi unaendelea Glasgow, Scotland na utamalizika tarehe 12 Novemba 2021.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments