AWACHOMA KISU WATOTO BAADA YA MKE WAKE KUOLEWA NA NJEMBA NYINGINE GEITA



na ALPHONCE KABILONDO - nipashe

JACKSON Bahati (27), mkazi wa kijiji cha Buhangizi, Kata ya Kagu, mkoani Geita, anadaiwa kuwajeruhi watoto wake wawili kwa kuwachoma kisu maeneo ya tumboni baada ya kwenda kijiji jirani na kumkuta mke wake ameolewa na mwanamume mwingine.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Kamishna Msaidizi (ACP) Dismas Kisusi, akithibitisha jana tukio hilo amesema kuwa tukio lilitokea majira ya saa 9:00 usiku Januari 27, mwaka huu.

Alisema baada ya kutenda kitendo hicho, mtuhumiwa naye alijichoma kisu mara nne kwenye tumbo lake na kisha kunywa sumu ya panya kwa lengo la kujiua.

Kamanda Kisusi aliwataja watoto waliojeruhiwa kuwa ni Leah Jackson (4) na Bahati Jackson (3) ambao wote walichomwa kisu maeneo ya tumboni na baada ya kutokea kwa tukio hilo, walipata msaada kutoka kwa raia wema na kupelekwa Hospitali ya Nzera na hadi sasa hali zao zinaendelea vizuri.

Kisusi alisema mtuhumiwa huyo akiwa chini ya ulinzi wa polisi, aliwahishwa na askari katika Hospitali ya Nzera na baadaye kuhamishiwa katika Hospitali ya Wilaya Sengerema mkoani Mwanza ambako mpaka sasa anaendelea kushikiliwa na polisi ili sheria ichukue mkondo wake.

"Chanzo cha tukio hilo ni mgogoro wa kifamilia ikiwa ni baada ya mama watoto, ambaye ni mke wa mtuhumiwa kutoroka nyumbani kwake na kuacha watoto hao na kwenda kusikojulikana. Baada ya baba watoto kumtafuta bila mafanikio ndipo akachukua uamuzi huo,” alisema.

Ofisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Geita, Last Lingson, alisema ili kuzuia matukio ya aina hiyo yanayotokana na usaliti na migogoro ndani ya familia, ni vyema wanandoa wajaribu kuangalia namna ya kuzuia viashiria hatarishi vinavyoweza kusababisha usaliti ndani ya ndoa.

Last aliwashauri watu ambao wako kwenye maumivu yanayotokana na migogoro ya ndoa kuwashirikisha wanasaikolojia au marafiki wa karibu mapema ili kuepuka kuchukua uamuzi unaoweza kuwagharimu ikiwamo kujiua na kufanya vitendo vya ukatili kwa ndugu zao wa karibu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
أحدث أقدم