MWANAMKE 'ALIYEFARIKI' MWEZI DISEMBA AJIFUNGUA MTOTO

Mtoto akiwa kwenye mashine ya kumpatia joto

Mwanamke mmoja mwenye miaka 26 amejifungua mtoto wa kiume siku ya Alhamisi licha ya kutangazwa kuwa ni mfu toka Disemba.

Mwanamichezo wa kimataifa, bi Catarina Sequeira alipatwa na shambulio kali la pumu akiwa nyumbani kwake.

Bi Sequeira amezikwa Ijumaa, siku moja baada ya mtoto kutolewa tumboni mwake.

Mtoto huyo aliyepewa jina la Salvador, amezaliwa baada ya kukua kwa wiki 32 tumboni mwa mama yake kwa wiki 32, na sasa yupo chini ya uangalizi kwenye hospitali ya watoto.

Hii ni mara ya pili nchini Ureno kwa mtoto kuzaliwa kutoka kwa mama ambaye ni 'mfu wa ubongo'.

Sequeira ambaye alikuwa mwanariadha wa mbio za mitumbwi amekuwa akisumbuliwa na pumu toka utoto wake.

Aliwahi kuiwakilisha nchi yake kwenye mashindano ya kimataifa wakati wa uhai wake.

Shambulio lililochukua uhai wake lilimpata akiwa na mimba ya wiki 19, hali iliyomfanya kupoteza fahamu. Siku chache akiwa chumba cha wagonjwa mahututi hali ilizidi kuwa mbaya na akatangazwa kuwa 'mfu wa ubongo' Disemba 26. Madaktari wakamuwekea mashine ya kusaidia kupumua ili mtoto tumboni aweze kuishi. Mashine hiyo iliwekwa kwa siku 56.
Sheria ya kutoa viungo yaamua 'kesi' hii

Madaktari wanasema malengo yalikuwa ni kusubiri mpaka Ijumaa ambapo ujauzito huo ungefikisha wiki 32, lakini mfumo wa hewa wa mama huyo uliharibika ghafla na kulazimisha upasuaji ufanyike Alhamisi ili mtoto atolewe.

Wiki 32 ndiyo kipindi ambacho madaktari wanansema mtoto anakuwa na uwezekano mkubwa wa kuishi.
Mkuu wa kitengo cha maadili cha hospitali hiyo, Filipe Almeida, ameelezea kuwa maamuzi ya kumuacha mtoto aendelee kukuwa kwenye tumbo la mama yake yalifikiwa kwa pamoja na familia ya mama huyo, kwa sababu katika uhai wake hakuwahi kipinga kwa maandishi sheria ya kutoa viungo vyake baaa ya kufariki.

"Kuwa mtoaji wa viungo si tu kuwa na nafasi ya kutoa ini au mapafu, lakini pia inahusu kuwa na uwezo wa kujitoa ili mtoto wako aishi," Almeida ameuambia mtandao wa Observador.

Baba wa mtoto huyo alitaka azaliwe, kama ilivyokuwa kwa familia nzima ya marehemu.

Hata hivyo mama wa Sequeira, bi Maria de Fátima Branco, ameiambia televisheni moja ya Ureno kuwa alimuaga binti yake Disemba 26, na uamuzi wa kumuacha mtoto huyo azaliwe umefikiwa baada ya baba yake, Bruno, amekuwa akitaka kuwa baba kwa muda sasa.

Mtoto huyo amezaliwa akiwa na uzito wa kilo 1.7kg na anatazamiwa kubaki hospitali kwa walau wiki tatu zijazo.

Mwaka 2016, mtoto mwengine ajulikanaye kama, Lourenço, alizaliwa jijini Lisbon baada ya kukaa kwa wiki 15 baada ya mama yake kufariki.
Chanzo - BBC

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
أحدث أقدم