CAG AKABIDHI RIPOTI 17 ZA UKAGUZI KWA RAIS MAGUFULI

Ripoti 17 za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad, kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 30, 2018 zimekabidhiwa rasmi kwa Rais Dk. John Magufuli.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Dar es Salaam na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT), ripoti hiyo imewasilishwa na CAG katika hafla fupi iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam juzi na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka ofisi hiyo. 

CAG alimkabidhi Magufuli ripoti ya Ukaguzi wa Serikali Kuu, Ripoti ya Ukaguzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, Ripoti ya Ukaguzi wa Mashirika ya Umma na Ripoti ya Ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo. 

Pia alikabidhi Ripoti ya Ukaguzi wa Mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Ripoti ya Ukaguzi wa Ufanisi na ripoti 11 za ukaguzi wa ufanisi katika sekta mbalimbali. 

Sekta hizo ni pamoja na usimamizi wa shughuli za ujenzi wa miradi ya umwagiliaji, usimamizi wa miradi ya maji vijijini, usimamizi wa miradi ya maji itokanayo na visima virefu. 

Nyingine ni matengenezo ya mitambo ya kuzalisha umeme, usimamizi wa elimu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu, usimamizi wa mfumo wa ununuzi wa magari ya Serikali kwa pamoja pia sekta ya ufuatiliaji wa shughuli za ujenzi na majengo ya mijini, usimamizi wa utoaji wa huduma za afya za rufaa na dharura kwa hospitali za rufaa ngazi ya juu, upatikanaji na usambazaji wa pembejeo za kilimo, usimamizi wa utoaji wa huduma ya bima ya afya na ufuatiliaji wa mapendekezo ya ukaguzi wa ufanisi.

Akizungumza baada ya kupokea ripoti hiyo, Magufuli aliipongeza ofisi ya CAG kwa kazi nzuri inayofanya na pia kuahidi kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nao kwa karibu na katika kukabiliana na kudhibiti matumizi mabaya na upotevu wa fedha za umma. 

Kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania Ibara ya 143 kifungu kidogo 2 na 4, kinamtaka CAG kukabidhi ripoti hizo kwa Rais kabla ya Machi 31, kila mwaka na baada ya hapo zinawasilishwa bungeni siku saba za mwanzo za kikao cha Bunge kinachofuata. 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527