KIGWANGALLA AMVAA MASHA KUHUSU FASTJET...WAMESHINDWA KUFANYA BIASHARA WAO WENYEWEPichani, Kushoto ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamisi Kigwangalla, Kulia ni Lawrence Masha

Waziri wa Maliasili na Utalii, Hamisi Kigwangalla ameitetea Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kukanusha kwamba haijazuia vibali vya kuingiza ndege mpya kwenye Kampuni ya Fastjet Tanzania inayomilikiwa na aliyekuwa Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Waziri Kigwangalla amesema kwamba kwa taarifa alizonazo ni kuwa Kampuni ya Fastjet imeshindwa kufanya biashara nchini na sio inavyosemekana kuwa imezuiwa kuingiza ndege mpya na serikali.

Masha akizungumza na chombo kimoja cha habari nchini, siku ya jana alisema “TCAA inasema ili niweze kuingiza ndege hiyo nimalize kwanza madeni yote, baadhi ya madeni tayari yamelipwa na Fastjet Plc mengine Fastjet Tanzania. Tayari tumemaliza, lakini fedha imeisha, kwa kuwa tayari fedha nyingine tulizitumia kutimiza matakwa yao, wangeniruhusu nifanye kazi ili nipate fedha ya kulipa yaliyobaki''.
Pichani, Ndege ya Fastjet.

Akijibu kuhusu malalamiko hayo Kigwangalla amesema "Kwa taarifa nilizonazo ni kwamba wameshindwa kufanya biashara wao wenyewe! Na hakuna sababu ya kuwazuia kuingiza ndege yao mpya. Ni kwamba wazungu wamejiondoa wamebaki wazawa na hawajazuiliwa kuingiza ndege zao" Kigwangalla

Hivi karibuni Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Anga nchini (TCAA) ilisema Shirika la Ndege la fast jet kwa sasa halina hali nzuri na limepoteza sifa ya kuendelea na huduma hiyo, hivyo ilitoa notisi ya siku 28 ya nia ya kulifuta kabisa shirika hilo.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga, Hamza Johari, amesema 'Notice' hiyo inaanza Disemba 17 hadi Januari huku akitoa tahadhari kwa wananchi kutotumia usafiri wa shirika hilo ili kuepuka usumbufu.

Aidha amesema kuwa pamoja na kuzuiwa kufanya huduma nchini, lakini hawatakiwi kuondoka kwakuwa wanadeni, "Mamlaka imezuia ndege hiyo (Fastjet) isiondoke hapa nchini kwa sababu Shirika linadaiwa madeni mengi, TCAA pekee inadai zaidi ya bilioni 1.4".

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
أحدث أقدم