UKAWA WALIVALIA NJUGA SAKATA LA KOROSHO...SASA KUFUNGUA KESI MAHAKAMANI

Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, James Mbatia, amesema endapo serikali haitatoa fedha za mauzo ya korosho, Umoja huo wa Katiba ya Wananchi utakwenda mahakamani kudai haki hiyo.


Mbatia alitoa kauli hiyo alipozungumza na waandishi wa habari kwenye Viwanja vya Bunge jijini Dodoma jana akiwa na wabunge wa vyama vinavyounda Ukawa.


Umoja huo unaundwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi na NLD.


Mbatia ambaye pia ni Mbunge wa Vunjo (NCCR-Mageuzi), alisema watazitumia siku mbili zilizobaki za Bunge la Bajeti kudai bungeni malipo hayo ya korosho na endapo serikali haitatoa fedha hizo, watalazimika kuisaka haki hiyo nje ya Bunge kwa kufunga kesi mahakamani.


"Korosho ambayo ilikuwa inatuingizia fedha za kigeni ni wazi sasa uchumi wa taifa letu utazidi kudidimia na ukididimia wote tunaumia," Mbatia alisema na kuongeza:


"Sasa tutaendelea kupinga bungeni wakati wa mjadala wa 'Finance Bill' (Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2018), hiyo sheria inayotaka kupokonya haki za wakulima, ikishindikana tutaidai haki hii mahakamani."


Mbatia alisema serikali inapaswa kuwa makini kwa kuwa taifa linapokuwa limepasuka na watu wake kuwa na hofu, haliwezi kuwa na maendeleo.


"Jambo hili la korosho ni kubwa na tusipolisimamia vizuri hatutafika pazuri. Kwenye Finance Bill, serikali ihakikishe wakulima hawa wa korosho wanapata haki zao za msingi," alisema Mbatia huku akieleza kuwa wanaunga mkono hoja ya Mbunge wa Kilwa Kusini, Seleman Bungara 'Bwege' (CUF) kuitisha maandamano kudai fedha hizo.


Naye Mbunge wa Malindi, Ally Saleh (CUF), alisema kitendo cha serikali kutotoa fedha hizo za wakulima ni kuvunja sheria na wawekezaji wataogopa kuja nchini.


“Serikali inapothubutu kuondosha fedha za wakulima ambazo zipo kisheria, tunapeleka ujumbe mbovu kwa wawekezaji. Sasa hivi tunataka kujenga viwanda na kukaribisha wawekezaji, ina maana kwamba hatuheshimu sheria, hivyo wawekezaji wataogopa kuja kuwekeza," alisemana kuongeza:


“Serikali inashindwa kuwekeza kwenye zao ambalo ni 'the best' (bora zaidi) katika nchi kwa sasa na inasema inashawishi watu waje wawekeze viwanda vya kubangua. Je, utamleta nani aje awekeze ikiwa serikali haiaminiki? Nadhani serikali inapaswa kuwa makini sana katika hili."


Naye Mbunge wa Mchinga, Hamidu Bobali (CUF), alisema hakubaliani na maelezo yaliyowasilishwa bungeni Jumatatu na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk. Adelardus Kilangi, kuwa serikali haitolipa fedha hizo kwa sababu za kisheria na kwamba wanayo nakala ya hukumu ya mahakama inayoonyesha serikali ilishindwa katika kesi dhidi ya Bodi ya Korosho na kutakiwa kulipa fedha hizo.


Katika maelezo yake bungeni, Dk. Kilangi alisema fedha hizo ni za umma na kwamba Bodi ya Korosho inakusanya kwa niaba ya serikali na kupanga matumizi.


“Msimamo huo umetokana na uamuzi wa kesi zilizofunguliwa kwenye Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa na haujawahi kupingwa," alisema na kuongeza kuwa:


“Serikali haiwezi kulipa fedha kwenye mfuko ambao haujaanzishwa kwenye sheria ambayo haijatungwa na Bunge. Endapo serikali ikifanya kinyume cha hapo, itakuwa imevunja sheria."

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
أحدث أقدم