WABUNGE SITA WANUSURIKA KIFO AJALI YA GARI...BUNGE LATOA KAULI

Wabunge sita wa Jamhuri Muungano wa Tanzania kutoka Visiwani Zanzibar wamenusurika kufa baada ya gari waliyokuwa wakisafiria kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam kupata ajali katika eneo la Bwawani mkoani Morogoro, usiku wa kuamkia leo.

Hayo yamethibitishwa na Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Morogoro Ulrich Matei, wakati alipokuwa anazungumza na mwandishi wa habari hii na kusema chanzo cha ajali hiyo imesababishwa na mnyama aina ya mbwa aliyekuwa anavuka barabara kutoka upande mmoja kwenda upande mwingine.

"Ni kweli hili tukio limetokea na muda huu tupo katika kiwanja cha ndege Mzinga mkoani Morogoro kwaajili ya kuwapakia hawa Wabunge wote kuelekea Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kupatiwa huduma nyingine zaidi kutokana na majeruhi waliyoyapata", amesema Kamanda Mtei.

Pamoja na hayo, Kamanda Mtei ameendelea kwa kusema "kati ya hao sita, mmoja amepata majeruhi ya kichwa. Hawa wote ni Wabunge wa Jamhuri Muungano wa Tanzania kutoka Visiwani Zanzibar. Chanzo cha ajali hii kimetokana na mnyama aina ya mbwa akiwa anatoka upande mmoja wa barabara na kuelekea upande mwingine na kupelekea dereva aliyekuwa anaendesha gari hilo kushika 'break ya faster' na kusababisha gari hiyo kugeuka ilipokuwa inatokea".

Kwa upande mwingine, Kamanda Mtei amesema wao kama Jeshi la Polisi hawana tabia ya kuuliza mtu anatokea chama gani wakati wa kutoa msaada kwa kuwa wanaogopa kuonekana wabaguzi katika utoaji wa huduma zao. 

Katibu wa Bunge, Steven Kagaigai amesema chombo hicho cha dola kinafuatilia kwa ukaribu ajali ya wabunge sita iliyotokea jana usiku, Machi 29, 2018 mkoani Morogoro.

Kagaigai amesema baada ya kupokea taarifa hizo wamefanya mawasiliano na uongozi wa Hospitali ya Morogoro na walishauriwa kuwahamishia Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

“Ndiyo taarifa hizo ninazo, wamepata ajali huko Morogoro, tayari tumeshafanya taratibu za kuwapeleka Muhimbili kwa huduma zaidi na ofisi yetu inawajibika kwa kila hatua,” amesema Kagaigai.

Wabunge hao ambao wote ni kutoka Zanzibar ni Haji Ameir Haji (Makunduchi), Khamis Ali Vuai (Mkwajuni), Bhagwanji Maganlal Meisuria (Chwaka), Makame Mashaka Foum (Kijini), Juma Othman Hija (Tumbatu).

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
أحدث أقدم