Taharuki : WAOMBOLEZAJI WAKIMBIA JENEZA LA MAREHEMU MKOANI RUKWA


Hali ya taharuki na hofu imezuka katika kijiji cha Katani kata ya Nkandasi wilayani Nkasi mkoani Rukwa na kusababisha waombolezaji kutimua mbio na kuacha jeneza lenye mwili wa marehemu baada ya mvua kubwa kuanza kunyesha ghafla yenye upepo na radi.

Tukio hilo lilitokea jana majira ya saa 6 mchana baada ya kuanza kunyesha mvua kubwa iliyoambatana na radi na upepo mkali ulioezua baadhi ya nyumba za wananchi hao ambao walikuwa wakiomboleza msiba wa mwananchi mwenzao aliyefariki baada ya kuugua siku chache zilizopita. 

Malunde1 blog imeambiwa kuwa tukio hilo limezua hisia za kishirikina kwa wananchi wa kijiji hicho kwani miezi miwili iliyopita baba yake na marehemu huyo alifariki baada ya kugongwa na gari la kampuni ya ujenzi wa barabara na walipofanya maziko siku iliyofuata walikuta ngozi ya kondoo juu ya kaburi la marehemu kitendo kilicho washangaza wakazi hao.

Akizungumza na Malunde1 blog mwenyekiti wa serikali ya kitongoji cha Kaungo, Robert Kanoni alisema wakiwa wanaelekea kufanya mazishi ya marehemu Dismas Kanoni aliyefari juzi, ghafla mvua kubwa ilianza kunyesha hali iliyosababisha baadhi ya waombolezaji kutimua mbio na kurejea majumbani kutokana na hofu iliyoibuka kufuatia tukio hilo.

Alisema baadhi ya wananchi walivumilia hali hiyo na kurudisha nyumbani jeneza lililokuwa na mwili wa marehemu na kuahirisha maziko kwa muda ili kupisha mvua hiyo  na baadaye walikwenda kuzika katika makaburi yaliyopo kijijini hapo. 


Kanoni alisema kutokana na mvua hiyo nyumba zipatazo 10 zimebomoka kabisa na zinatakiwa kujengwa upya huku nyumba nyingine saba, zikiwa zimeezuliwa paa na kuwaacha wakazi wake wakiwa hawana sehemu ya kukaa licha ya kuwa wamepata hifadhi na misaada ya kibinaadamu kwa wenzao. 

Naye Peter Kalale mkazi wa kijiji hicho akizungumzia tukio hilo alisema mara kwa mara kijiji hicho kimekuwa kikikumbwa na dhoruba pindi mvua zinaponyesha kwakuwa kimepitiwa na mkondo wa upepo mkali ambao unasababisha hali hiyo. 

Alisema changamoto iliyopo ni tabia ya wananchi kukata miti kwa ajili ya mashamba na hivyo kusababisha pepo zinapovuma hazikuti kizuizi chochote na hivyo imekuwa sababu ya kuezuliwa nyumba zao na hata kubomoka kabisa. 


Kwa upande wake mwenyekiti wa kamati ya maafa ya wilaya hiyo ambaye ni mkuu wa wilaya hiyo Said Mtanda ilikiri kutokea kwa tukio hilo na kutoa wito kwa wananchi kujenga nyumba bora kwani miongoni mwa nyumba hizo zipo ambazo zimeezekwa kwa nyasi.

Alisema kuwa sera ya serikali ya awamu ya tano ni kuwahimiza wananchi wajenge nyumba bora na za kisasa ili waweze kuepuka majanga yanayotokana na tabia nchi kwani bila kufanya hivyo wananchi wataendelea kupata hasara.
Na Walter Mguluchuma - Malunde1 blog Nkasi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
أحدث أقدم