Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Mwanza
WANUFAIKA wa Mradi wa Kunusuru Kaya Maskini unaosimamiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), wilayani Misungwi Mkoa wa Mwanza, wameipongeza Serikali inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha maisha yao.
Wananchi hao wameeleza kunufaika kwa namna mbalimbali ikiwemo kupitia ruzuku, mafunzo ya ujasiriamali na ajira katika miradi ya maendeleo, ambazo zimewawezesha kujikwamua kiuchumi na kumudu gharama za maisha.
Wanufaika hao wametoa pongezi hizo leo, Oktoba 17, 2026, wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Umasikini, wakieleza kuwa msaada wanaoupata kupitia TASAF umewawezesha kuanzisha shughuli za uzalishaji mali, kuweka akiba, kuanzisha biashara na kuboresha makazi pamoja na huduma za familia zao.
Wamesema kupitia vikundi vya ujasiriamali na mafunzo wanayopatiwa, wamejifunza kutengeneza bidhaa mbalimbali zikiwamo sabuni, vitambaa vya batiki, vikapu na mikeka, huku wengine wakijihusisha na ufugaji, uvuvi na shughuli za kilimo ambazo zimekuwa chanzo cha mapato na kuwawezesha kukabiliana na changamoto za kiuchumi.
Akizungumza kuhusu manufaa aliyoyapata, mnufaika wa TASAF Muyanja Mafuru amesema kabla ya kujiunga na mfuko huo aliishi katika mazingira magumu, akitumia nyumba iliyojengwa kwa miti kuanzia chini hadi juu na kuezekwa kwa nyasi, huku akihangaika kutafuta mahitaji muhimu ya familia yake.
“Baada ya kujiunga na TASAF, nilianza kupokea ruzuku na kushiriki katika miradi ya mfuko huo, ambako nilikuwa nikilipwa fedha. Nilianza kuweka akiba kidogo kidogo na baadaye tukapatiwa mafunzo ya kutengeneza sabuni za maji za kusafishia vyoo na mafuta ya mgando ya mche.
Amesema mafunzo ya ujasiriamali na uwezeshaji alioupata vimemsaidia kupanua shughuli zake za kujipatia kipato na kupunguza utegemezi, akisisitiza kuwa fursa hizo zimekuwa muhimu kwa familia yake katika kuboresha maisha na kuwekeza kwa ajili ya maendeleo ya baadaye.
Kwa upande wake, mnufaika wa TASAF kupitia kikundi cha Mliman City, Helena Kazungu, mkazi wa Kijiji cha Igenge, Kata ya Mbarika, amesema kikundi hicho kilianzishwa mwaka 2024 kwa kushirikiana na wataalamu wa ustawi wa jamii, kikiwa na wanawake 12 walioamua kuungana na kuanzisha shughuli za uzalishaji mali.
Amesema kila mwanachama alichangia Shilingi 50,000 na kupata mtaji wa awali wa kununua vitambaa, rangi na vifaa vingine vya kutengeneza batiki.
Kazungu amesema baada ya kupata mafunzo, wanawake hao walianza kutengeneza na kuuza vitambaa vya batiki kwa bei zinazotofautiana kulingana na aina ya bidhaa, huku wakitumia sehemu ya mapato kuendeleza mtaji, kuweka akiba na kukopeshana.
Ameongeza utaratibu huo umewasaidia kuendelea na biashara hata wanapokabiliwa na changamoto za soko, na baadhi yao wameweza kununua mifugo na kuwekeza katika mazao ya kilimo ili kuongeza kipato.
Ameeleza kuwa, manufaa ya TASAF yameonekana pia katika kuboresha makazi, ambapo baadhi ya wanachama wameweza kuvuta maji hadi nyumbani, kujenga vyoo bora na kuanza maandalizi ya ujenzi wa nyumba.
Ameongeza kuwa mfuko huo umesaidia familia kugharamia mahitaji ya watoto wanaosoma sekondari na kuwawezesha wanawake na wazee kushiriki katika shughuli za kiuchumi.Ameoomba Serikali iendelee kuwawezesha wanufaika kwa kuwapatia mitaji zaidi, mafunzo na fursa za kukuza biashara zao.
Mnufaika mwingine wa TASAF, ambaye aliyesema ana watoto sita, ameeleza kuwa kabla ya kujiunga na mfuko huo mwaka 2024 alikuwa akikabiliwa na changamoto za kupata chakula na kugharamia elimu ya watoto wake.
Amesema ruzuku aliyokuwa akipokea, pamoja na shughuli za ujasiriamali na miradi ya maendeleo, imemsaidia kuboresha maisha ya familia yake, huku watoto wake wakiendelea na masomo na baadhi wakifikia elimu ya sekondari.
Kwa ujumla, wanufaika hao wameitaka Serikali kuendeleza programu za TASAF kwa kuwa zimewapa fursa ya kujitegemea badala ya kutegemea misaada pekee.
Wamesema kuongezewa mitaji, kuimarishwa kwa mafunzo ya biashara na kupanuliwa kwa fursa za ajira katika miradi ya jamii kutawasaidia kuongeza uzalishaji, kuimarisha kipato na kuendelea kupunguza umaskini katika kaya zao.
Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Umasikini, yanayofanyika Oktoba 17 kila mwaka, yanatoa nafasi ya kutathmini juhudi za kukabiliana na umaskini na kuhimiza ushiriki wa wananchi katika kujenga maisha bora.









Social Plugin