Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WALIMU WAAZA MAADHIMISHO YA MIAKA 60 YA KULINDA TAALUMA




Na Dotto Kwilasa, Dodoma

MAADHIMISHO ya Siku ya Mwalimu Duniani yameanza rasmi jijini Dodoma, yakihusisha utoaji wa huduma, elimu na usikilizaji wa changamoto za walimu, huku wadau mbalimbali wa sekta hiyo wakisisitiza umuhimu wa kulinda heshima ya taaluma ya ualimu na kuboresha mazingira yanayomwezesha mwalimu kufanya kazi yake.

Maadhimisho hayo yameanza Oktoba Mosi na yatafikia kilele Oktoba 5, 2026, yakiongozwa na kaulimbiu “Kusimama pamoja na walimu: Miaka 60 ya kulinda taaluma, kuendeleza hadhi yake na kuunda mustakabali wetu.”

Katika kuanza kwa maadhimisho hayo, viongozi na wadau wa elimu walifanya ziara ya kukagua mabanda yaliyowekwa katika viwanja vya Nyerere Square, Dodoma, ambako walimu na wananchi wanapata huduma na taarifa mbalimbali zinazohusu utumishi wa walimu.

Baada ya kukagua mabanda hayo, viongozi hao walielekea katika eneo maalum la mkutano katika ofisi za Chama cha Walimu Tanzania (CWT), ambako masuala mbalimbali yanayohusu taaluma, mazingira ya kazi na ustawi wa walimu yaliendelea kujadiliwa.

Kaimu Katibu Mkuu wa CWT, Magesa Protas, alisema maadhimisho hayo yanapaswa kuwa sehemu ya kutambua mchango wa walimu ambao, licha ya changamoto mbalimbali za kiutumishi, wameendelea kujitoa katika kuwahudumia wanafunzi na jamii.

Alisema walimu wanaipenda kazi yao na wanaendelea kuonyesha dhamira ya kuitendea haki taaluma hiyo kwa kujitoa katika kufundisha, kulea na kujenga maarifa ya wanafunzi.

“Walimu wanaipenda kazi yao na wanajua kuitendea haki kwa kujitoa kwa moyo. Sisi kama Chama cha Walimu tunaendelea kutoa pongezi kwa Serikali kwa kuendelea kuboresha maslahi ya walimu,” alisema.

Magesa alisema CWT imeendelea kuona hatua zinazochukuliwa katika kushughulikia baadhi ya changamoto za walimu, ikiwemo masuala ya kupandishwa vyeo na mambo mengine yanayohusu utumishi wao.

Alisema pamoja na hatua hizo, bado kuna mifumo ya kiutumishi yenye changamoto zinazohitaji kuendelea kufanyiwa kazi ili kumpa mwalimu unafuu na kumwezesha kuzingatia zaidi jukumu lake la msingi la kutoa elimu.

Kwa mujibu wa Magesa, mwalimu anapopata huduma na stahiki zake kwa wakati, hupunguza vikwazo vinavyoweza kumzuia kuzingatia kazi ya kufundisha na hivyo kuchangia mazingira bora ya kujifunzia kwa wanafunzi.

Alisema CWT itaendelea kuwasiliana na Serikali kuhusu changamoto zilizopo, huku akiiomba Serikali kuhakikisha madeni na stahiki mbalimbali za walimu zinalipwa kwa wakati.

“Tunaiomba Serikali iendelee kulipa madeni yote ya walimu kwa wakati. Tunapoendelea kusimama pamoja, tunazingatia mtoto na mzazi kwa sababu tunaamini kazi ya mwalimu ni kujenga maarifa, kulea, kuandaa vijana na kujenga msingi wa maendeleo ya Taifa,” alisema.

Magesa pia alitoa wito kwa jamii kuendelea kuwaheshimu walimu na kutengeneza mazingira salama yanayolinda hadhi ya taaluma hiyo.

Alisema ualimu ni taaluma yenye thamani kwa sababu inamhudumia mwanadamu na ina nafasi ya moja kwa moja katika kuandaa wataalamu, viongozi na wananchi wenye maarifa kwa ajili ya kizazi kijacho.

Aidha, alisema CWT inaendelea kujipanga kuwafikia walimu wengi zaidi nchini ili wawe sehemu ya umoja huo na kupata nafasi ya kuwasilisha changamoto zao pamoja na kushiriki katika juhudi za kuboresha mazingira ya kazi.
HUDUMA ZA WALIMU ZAPELEKWA KARIBU

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Maadili na Nidhamu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Asha Kubuva, alisema uwepo wa taasisi mbalimbali katika eneo la maadhimisho hayo umewezesha huduma kuwafikia walimu kwa urahisi zaidi.

Alisema badala ya mwalimu kuzunguka katika maeneo mbalimbali kutafuta majibu ya changamoto zake, maadhimisho hayo yamewakutanisha wadau wanaohusika na huduma mbalimbali zinazomgusa mwalimu.

“Mwalimu hakosi huduma hapa. Kuna masuala mengine tunawaelekeza na kuwabeba kuwapeleka sehemu husika,” alisema.

Kubuva alisema maadhimisho hayo pia yametumika kutoa elimu na kuhamasisha walimu kushiriki katika shughuli za kijamii, ikiwemo uchangiaji wa damu.

Alisema ushiriki wa walimu katika kuchangia damu ni sehemu ya kutambua kwamba mchango wa mwalimu kwa jamii hauishii darasani pekee, bali unaweza pia kuonekana katika matendo yanayookoa na kuboresha maisha ya watu wengine.

Alisema kupitia shughuli hiyo, walimu wanapata fursa ya kuchangia damu ambayo inaweza kutumika kuwasaidia wagonjwa, wajawazito, watoto na watu wengine wanaohitaji damu hospitalini.

Kubuva aliwataka walimu wenye changamoto za kiutumishi kuzifikisha mapema kwa mamlaka husika badala ya kusubiri hali kuwa kubwa.

Alisema kufanya hivyo kunasaidia changamoto kushughulikiwa kwa wakati na kumwezesha mwalimu kuendelea na majukumu yake bila vikwazo visivyo vya lazima.
TSC YAWEKA WAZI JUKUMU LAKE KWA WALIMU

Naye Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia Ajira na Maendeleo ya Walimu wa TSC, Magthilde Scapinga, alisema maadhimisho hayo pia yametumika kuwafahamisha wananchi na walimu kuhusu majukumu ya Tume hiyo.

Scapinga alisema TSC ni taasisi ya Serikali iliyo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), yenye jukumu la kusimamia na kuendeleza utumishi wa walimu katika maeneo ya ajira, maadili na maendeleo yao wakiwa watumishi wa umma.

Alisema Tume hiyo ilianzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Tume, Sura ya 448, pamoja na kanuni zake za mwaka 2016 na ilianza kutekeleza majukumu rasmi mwaka huo.

Kwa mujibu wa Scapinga, TSC ina Makao Makuu Dodoma na ina ofisi 139 katika wilaya zote za Tanzania Bara, zinazosaidia kusogeza huduma karibu na walimu.

Alisema miongoni mwa majukumu ya Tume ni kusimamia ajira za walimu, kupandisha vyeo, kubadilisha kada kwa walimu wanaojiendeleza kitaaluma na kuhakikisha masuala yao ya kiutumishi yanafuatwa kwa mujibu wa taratibu.

“Tunafahamu walimu wanaajiriwa wakiwa na ngazi fulani ya elimu, lakini wakiwa ndani ya utumishi wanaendelea kujiendeleza. Wanapopata sifa za juu zaidi, Tume tunalo jukumu la kuhakikisha wanabadilishwa muundo kwa kadri ya elimu na sifa walizonazo,” alisema.

Alisema TSC pia huendelea kumhudumia mwalimu hadi anapofikia hatua ya kustaafu, ikiwemo kutoa kibali cha kustaafu na kusimamia upatikanaji wa stahiki zake kwa mujibu wa taratibu.

Katika eneo la maadili na nidhamu, Scapinga alisema Tume huanza kwa kutoa elimu kwa walimu kuhusu taratibu na maadili ya utumishi kabla ya kuchukua hatua kwa wale wanaokiuka kanuni.

Alisema TSC pia ni mamlaka ya rufaa kwa walimu ambao hawajaridhika na maamuzi yaliyotolewa katika ngazi za chini.

Alieleza kuwa masuala ya nidhamu yanaweza kuanzia katika ngazi ya shule na wilaya, huku mwalimu asiyeridhika na uamuzi wa ngazi ya chini akiwa na nafasi ya kukata rufaa kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa hadi kufikia Tume Makao Makuu na hatua zinazofuata kwa mujibu wa sheria.

Scapinga alisema maadhimisho ya Siku ya Mwalimu Duniani yanatoa fursa ya kutambua mchango wa mwalimu kama sehemu muhimu ya maendeleo ya jamii.

Alisema Oktoba 5 kila mwaka huadhimishwa Siku ya Mwalimu Duniani, ikiwa ni siku ya kutambua na kuthamini mchango wa walimu katika jamii, huku maadhimisho ya mwaka huu yakiendelea Dodoma hadi kilele chake Oktoba 5.

Maadhimisho hayo yanaendelea katika viwanja vya Nyerere Square, Dodoma, yakihusisha TSC, CWT na wadau wengine wanaotoa huduma na elimu kwa walimu na wananchi wanaofika katika mabanda hayo.









Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com