CHADEMA YAFANYA HARAMBEE UJENZI WA OFISI BUKOBA

Na Mbuke Shilagi Bukoba.

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) manispaa ya Bukoba Mkoani kimefanikiwa kufanya harambee ya ununuzi wa kiwanja na ujenzi wa ofisi na kufanikiwa kupata zaidi ya shilingi milioni 12.

Harambee hiyo imefanyika Machi 23,2024 katika ukumbi wa Bukoba Coop hotel na  kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa mkoa wa Kagera, viongozi kutoka Kanda ya ziwa Victoria na wanachama ambapo Mgeni rasmi alikuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya ziwa Viktoria Mhe. Ezekiel Wenje.

Akizungumza na Wanachama wa CHADEMA waliohudhuria harambee hiyo Mwenyekiti wa CHADEMA Manispaa ya Bukoba mh. Chief Kalumuna amesema kuwa kila kata waliweka pesa ambazo watachangia na ili kufanikiwa kila kiongozi alikuwa anachangia kiasi ambacho walipanga kuchangia ikiwa ni pamoja na mwanachama mmoja mmoja.

"Uchaguzi wa serikali za mitaa hauhusiki na ujenzi wa ofisi za chama tutaona hapa tunapata shilingi ngapi na zoezi la kuchangia litaendelea", amesema Mh. Chief Kalumuna.

Aidha Katibu Mkuu wa CHADEMA Kanda ya Ziwa Victoria Mhe. Zakaria Obadia amesema jambo hilo limepitishwa na ni maazimio ya chama kila kanda hivyo kazi hiyo ni kuimarisha nguvu ya chama na ujenzi wa ofisi itaweza kuunganisha wanachama.

"Kazi ya leo ambayo imefanyika ni kazi ambayo tulikubaliana kila Kanda na moja ya mambo ambayo tuliidhinisha ni ujenzi wa ofisi kila Kanda na wenzetu wa Bukoba mmeanza kusimama kwenye maazimio ambayo tulipitisha Julai 25, 2022 kwa hiyo hongereni sana",amesema Mhe. Obadia 

Naye mjumbe wa kamati kuu CHADEMA taifa Mh. Grace Kiweru ambaye pia amehudhuria harambee hiyo amesema kuwa mwaka huu kuna uchaguzi wa serikali za mitaa na mwaka 2025 kuna uchaguzi mkuu hivyo wapiga kura wachague viongozi makini na mahiri ambao watapigania maendeleo na kupongeza eneo ambalo CHADEMA imelinunua kwa ajili ya ujenzi wa ofisi ya chama.

"Kazi kubwa ambayo tumetumwa Bukoba na kamati kuu ya chama tumeimaliza zoezi la kuhoji na kuteua ila niwaombe naona wagombea na wapiga kura hapa niwaombe mkafanye uchaguzi wa kuchagua kiongozi bora usiende kuchagua kiongozi ambaye amekununulia chai au kukulipia nauli mkachague kiongozi makini na mwenyekupigania chama",amesema Mh. Grace Kiweru.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments