NEC YATANGAZA UCHAGUZI MDOGO KATA 23 ZA TANZANIA BARA


Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Mhe. Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele (katikati) akiongoza kikao cha Tume jijini Dodoma leo Februari 15,2024 ambapo pamoja na mambo mengine kilitangaza uchaguzi mdogo wa kata 23 za Tanzania Bara utakaofanyika Machi 20,2024. Kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa Tume, Mhe. Jaji (Rufaa) Mstaafu, Mbarouk Salim Mbarouk na kulia ni Katibu wa Tume na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Kailima R.K.

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Mhe. Jaji (R) Jacobs Mwambegele (kushoto) akiongoza kikao cha Tume jijini Dodoma leo Februari 15,2024 ambapo pamoja na mambo mengine kilitangaza uchaguzi mdogo wa kata 23 za Tanzania Bara utakaofanyika Machi 20,2024. Pamoja nae ni Katibu wa Tume na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Kailima R.K.

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Mhe. Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele (kulia) akiongoza kikao cha Tume jijini Dodoma leo Februari 15,2024 ambapo pamoja na mambo mengine kilitangaza uchaguzi mdogo wa kata 23 za Tanzania Bara utakaofanyika Machi 20,2024. Kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa Tume, Jaji (Rufaa) Mstaafu, Mbarouk Salim Mbarouk.

Wajumbe wa Tume wakiwa katika kikao cha Tume

**************
Tume ya Taifa ya Uchaguzi imetangaza uchguzi mdogo wa madiwani kwenye kata 23 za Tanzania Bara.

Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Kailima Ramadhani jijini Dodoma leo tarehe 15 Februari, 2023 uchaguzi huo utafanyika tarehe 20 Machi, 2024.

“Fomu za uteuzi zitatolewa kuanzia tarehe 27 Februari, 2024 hadi tarehe 04 Machi, 2024, uteuzi wa wagombea utafanyika tarehe 04 Machi, 2024 na kampeni za uchaguzi zitafanyika kuanzia tarehe 05 hadi 19 Machi, 2024,” imesema taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imeanisha kuwa uchaguzi huo umetangazwa kwa kuzingatia matakwa ya kifungu cha 13(3) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292 baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa, akiitaarifu Tume kuhusu uwepo wa nafasi wazi za madiwani katika kata 23 za Tanzania Bara.

Imeongeza kuwa Waziri ametoa taarifa hiyo kwa kuzingatia matakwa ya kifungu cha 13(1) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292.

“Tume inatumia nafasi hii kuvikumbusha vyama vya siasa, wagombea na wadau wote wa uchaguzi kuzingatia Katiba, Sheria, Kanuni, Maadili ya Uchaguzi, Taratibu, Miongozo na maelekezo ya Tume katika kipindi cha uchaguzi huu mdogo,” imesema taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo kata zitakazofanya uchaguzi huo mdogo ni Kimbiji (Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni), Kasingirima (Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma/Ujiji), Ndevelwa (Halmashauri ya Manispaa ya Tabora), Msangani (Halmashauri ya Mji Kibaha), Fukayosi(Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo), Mlanzi (Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti), Utiri (Halmashauri ya Mji Mbinga) na Mbingamhalule (Halmashauri ya Wilaya ya Songea).

Nyingine ni Isebya (Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe), Kibata (Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa), Mshikamano (Halmashauri ya Wilaya ya Musoma), Busegwe (Halmashauri ya Wilaya ya Butiama), Nkokwa (Halmashauri ya Wilaya ya Kyela), Kamwene (Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba), Chipuputa (Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu), Buzilasoga (Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema), Mhande (Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba), Kabwe (Halmashauri ya Nkasi), Bukundi (Halmashauri ya Wilaya ya Meatu) Mkuzi (Halmashauri ya Wilaya ya Muheza) na Boma, Mtimbwani na Mayomboni (Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga).

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments