ABDUL NONDO AKAMATWA NA POLISI CHUONI UDSM

Mwenyekiti wa Mtandao wa wanafunzi (TSNP) na Mwanafunzi wa mwaka wa tatu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Abdul Nondo amekamatwa na Jeshi la Polisi kwa kile kinachodaiwa kuwa ni kuonekana katika maeneo ya chuo hicho.


Akizungumza juu ya tukio hilo Mkurugenzi wa Idara ya Habari wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania, Hellen Sisya amesema Nondo alikamatwa jana Julai 26 saa tatu usiku wakati akizungumza na wenzake, katika eneo la chuo hicho.


"Nondo alikuwa maeneo ya chuo cha UDSM pamoja na wanafunzi wengine majira ya saa tatu usiku ndipo alipokamatwa na Auxilliary polisi wa UDSM na kuchukua maelezo lakini hawakukaa naye sana wakampeleka katika kituo cha polisi hapa hapa UDSM na wakasema hawawezi kumuachia kwa usiku ule kutokana sababu za kiusalama", amesema Hellen.


Aidha, Hellen amesema kwa mujibu wa maelezo ya awali aliyopewa ni kuwa Nondo amekamatwa kwa kosa la kuingia eneo la chuo kinyume cha sheria kutokana hapo awali alishazuiliwa kuendelea kusoma chuoni hapo.


Hata hivyo, taarifa mpya jioni hii zinaarifu kuwa Abdul Nondo tayari ameachiliwa kwa dhamana ya Polisi huku akitakiwa siku ya Jumatatu Julai 30, 2018 kuenda kuripoti.


Mnamo Machi 26, 2018, Abdu Nondo ambaye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wa mwaka wa tatu, alisimamishwa kuendelea na masomo yake na Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa William Anangisye baada ya kupandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa.


Nondo anakabiliwa na kesi mbili ambapo ya kwanza ni kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni kuwa yupo hatarini, akiwa katika eneo la Ubungo na kuzisambaza kwenye mtandao wa Whatsapp.


Kosa la pili likitajwa kuwa ni kutoa taarifa za uongo kwa mtumishi wa umma Mafinga wakati alipokuwa akitoa taarifa katika kituo cha polisi mjini Iringa kwa kusema kuwa alitekwa na watu wasiojulikana.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527