Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MTUMBA KUFUMBUA FURSA MPYA ZA UTAWALA NA UCHUMI WA DODOMA



Na Dotto Kwilasa, Dodoma

DODOMA inatarajiwa kuimarisha nafasi yake kama kitovu cha shughuli za Serikali nchini kupitia Mji wa Serikali Mtumba, unaokusudiwa kuunganisha wizara na taasisi za umma katika eneo moja na kurahisisha uratibu wa majukumu ya kitaifa.

Hatua hiyo inatarajiwa kuimarisha mawasiliano baina ya taasisi za Serikali, kupunguza changamoto za kiutendaji zinazotokana na kutawanyika kwa ofisi katika maeneo mbalimbali na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya Serikali.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuzindua rasmi majengo ya ofisi za wizara na taasisi za Serikali pamoja na barabara za lami katika Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma, Oktoba 30, 2026.

Kwa mujibu wa Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu)Prof.Palamagamba Kabudi Ujenzi wa Mji wa Serikali Mtumba ni sehemu ya mpango wa Serikali wa kuimarisha Dodoma kama Makao Makuu ya Serikali, kwa kuweka miundombinu inayowezesha shughuli za kiutawala kufanyika katika mazingira yaliyoratibiwa zaidi.

Akizungumza Dodoma Oktoba 27, 2026, uzinduzi huo ni sehemu ya utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi wa umma na kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi na kwamba Kuwepo kwa wizara na taasisi katika eneo moja kunatarajiwa kurahisisha uratibu wa shughuli za Serikali, mawasiliano baina ya watumishi na utekelezaji wa majukumu yanayohitaji ushirikiano wa taasisi mbalimbali.

Aidha, kukamilika kwa miundombinu hiyo kunatoa fursa ya kuimarisha mifumo ya kiutendaji na kuweka mazingira yanayoweza kusaidia taasisi za umma kuwahudumia wananchi kwa ufanisi zaidi.

FURSA ZA KIUCHUMI KWA DODOMA

Mbali na umuhimu wake kiutawala,Prof.Kabudi amesema maendeleo ya Mji wa Serikali Mtumba yanaweza kuchochea shughuli za kiuchumi katika Jiji la Dodoma na maeneo yanayolizunguka.

Amesema Kuongezeka kwa shughuli za Serikali katika eneo hilo kunatoa fursa kwa sekta binafsi kushiriki katika huduma za usafirishaji, malazi, biashara, chakula na huduma nyingine zinazohitajika na watumishi pamoja na wageni wanaofika kwa shughuli za kikazi.

Hata hivyo, manufaa hayo yanategemea pia namna fursa zitakavyotumika, upatikanaji wa huduma saidizi na uwezo wa wafanyabiashara na wananchi wa eneo hilo kushiriki katika shughuli za kiuchumi zinazochochewa na uwekezaji huo.

Amesema Serikali imetoa wito kwa sekta binafsi kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji na wafanyabiashara ili kutumia fursa zinazotokana na maendeleo ya Mji wa Serikali na Makao Makuu ya nchi kwa ujumla.

Hatua hiyo inalenga kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi katika shughuli za kiuchumi zinazoweza kuongezeka kutokana na upanuzi wa miundombinu na shughuli za kiutawala jijini Dodoma.

MIUNDOMBINU NA UWAJIBIKAJI

Katika taarifa hiyo, Serikali imesisitiza kuwa uwepo wa majengo mazuri pekee hautoshi, bali unapaswa kwenda sambamba na utendaji bora, nidhamu ya kazi na uzalendo ili wananchi wanufaike na uwekezaji unaofanyika.

Aidha amesema Watumishi wa umma wametakiwa kutumia mazingira hayo kutekeleza majukumu yao kwa uwajibikaji, uadilifu na weledi, huku taasisi husika zikiendelea kuhakikisha kuwa huduma zinazotolewa zinakidhi mahitaji ya wananchi.

Kwa upande mwingine, wananchi, hususan wakazi wa Mkoa wa Dodoma, wametakiwa kujitokeza kwa wingi kushuhudia uzinduzi huo utakaofanyika Oktoba 30, 2026.

Uzinduzi huo unatarajiwa kuhusisha majengo ya ofisi za wizara na taasisi za Serikali pamoja na barabara za lami katika Mji wa Serikali Mtumba.

Kwa ujumla, maendeleo ya Mji wa Serikali Mtumba yanaweka msingi wa kuendelea kuimarisha nafasi ya Dodoma katika shughuli za kitaifa. Hata hivyo, mafanikio ya uwekezaji huo yatapimwa zaidi kwa ufanisi wa utendaji wa Serikali, ubora wa huduma zinazotolewa na namna fursa za kiuchumi zitakavyowanufaisha wananchi.













Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com