Na Dotto Kwilasa,Dodoma
UJENZI wa Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma umeongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za umma kupitia uwekezaji wa miundombinu ya kisasa na matumizi ya mifumo ya Serikali mtandao, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema.
Msigwa ameyasema hayo alipokutana na waandishi wa habari na wahariri waliotembelea Mji wa Serikali Mtumba, siku chache kabla ya uzinduzi rasmi wa majengo na miundombinu ya mji huo unaolenga kuboresha mazingira ya utendaji kazi serikalini na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imewekeza katika ujenzi wa mji wenye miundombinu ya kisasa unaokidhi hadhi ya Tanzania, huku ukiweka mazingira rafiki kwa wananchi wanaofika kupata huduma katika taasisi mbalimbali za umma.
Kwa mujibu wa Msigwa, uwekezaji huo haujaishia katika ujenzi wa majengo na barabara pekee, bali umehusisha pia mifumo ya kiteknolojia inayowezesha utoaji wa huduma kwa haraka na kwa ufanisi zaidi.
Amesema mifumo hiyo inatoa fursa kwa baadhi ya wananchi kupata huduma kwa njia ya mtandao bila kulazimika kufika moja kwa moja katika ofisi za Serikali, hatua inayoweza kupunguza gharama za usafiri na muda unaotumika kufuatilia huduma.
“Tumefanya uwekezaji mkubwa katika mifumo ya uendeshaji wa Serikali. Kwa hiyo, tunaweza kusema kwa lugha ya Kiingereza kuwa huu ni Smart City, kwa maana huduma zinatolewa kwa ufanisi zaidi kupitia mifumo maalumu,” amesema Msigwa.
Ameeleza kuwa matumizi ya mifumo ya Serikali mtandao ni sehemu ya jitihada za kuboresha mawasiliano na utendaji wa taasisi za umma, huku yakilenga kurahisisha upatikanaji wa huduma na kuongeza ufanisi katika shughuli za kila siku za watumishi.
Katika hatua nyingine, Msigwa amesema Serikali imejenga jumla ya kilomita 59 za barabara za lami ndani ya Mji wa Serikali Mtumba, miundombinu inayorahisisha usafiri na kuwawezesha wananchi kufika katika ofisi mbalimbali kwa urahisi.
Amesema barabara hizo na miundombinu mingine iliyowekwa ndani ya mji huo inalenga kuhakikisha wananchi wanaofika kwa ajili ya kupata huduma wanapata mazingira bora ya kufika katika taasisi wanazohitaji bila kukumbana na changamoto za barabara zisizo na lami.
Aidha, amesema muonekano wa majengo na uwekezaji katika miundombinu ya kisasa unaifanya Mji wa Serikali Mtumba kuwa miongoni mwa maeneo yanayoweza kuvutia wageni wanaotembelea Dodoma.
Msigwa amewashukuru waandishi wa habari na wahariri walioshiriki ziara hiyo, akieleza kuwa ziara hiyo ni fursa ya kuwapatia taarifa kuhusu uwekezaji uliofanywa na Serikali na malengo yake katika kuboresha huduma kwa umma.
Amesisitiza kuwa kukusanywa kwa ofisi mbalimbali za Serikali katika eneo moja kunatarajiwa kurahisisha wananchi kupata huduma kutoka taasisi tofauti, kupunguza usumbufu wa kufuatilia huduma katika maeneo yaliyotawanyika na kuboresha uratibu wa shughuli za Serikali.
Uwekezaji huo unaweka mkazo katika kuunganisha miundombinu ya kisasa na teknolojia ili kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi wa umma na kuongeza urahisi wa upatikanaji wa huduma kwa wananchi.







TAFUTA HABARI
Social Plugin