

Na Damas Makangale. Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Benki ya Dunia Tanzania (World Bank- Tanzania ) Deni la taifa ni vumilivu , mfumuko wa bei umethibitiwa na uchumi wa nchini unaendelea kuimarika kwa kuongezeka kwa matumizi ya serikali yenye tija kwenye uwekezaji na ukuaji wa sekta binafsi kuimarika katika uchangiaji wa uchumi wa nchini.
Akizungumza kwenye uzinduzi wa ripoti hiyo ya Benki ya Dunia (WB) ya maendeleo na ukuaji wa uchumi wa nchini jijini Dar es Salaam ambayo ilibeba kauli mbiu ‘kufanya Ajira ziwe na Tija’ Waziri wa nchini Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo alisema kwama alisema kwamba uchumi wa nchini unakwenda sambamba na Dira ya taifa ya Maendeleo 2050 ambayo inalenga kuleta matokeo Chanya kwa nchini na watanzania.
Profesa mkumbo alisema kwamba kwa mujibu wa ripoti ya Benki ya Dunia (WB) kuhusu kwa Tanzania kwa kiwango cha ukuaji wa uchumi na mfumuko wa bei ni vumilivu na zinaweza kuendelea kuthibitiwa ili kuhakikisha zinakwenda sambamba na Dira ya Taifa 2050 kwa maslahi mapana ya taifa na watanzania.
“Dira ya Taifa ya maendeleo ni lazima ianze kutekelezwa sasa kwa minajili ya kufungua fursa za ajira , kuleta mabadiliko kwenye taasisi za elimu , masoko yanayoendana na ujenzi wa miundimbinu na teknolojia ambayo ina nafasi kwa vijana wengi zaidi kuingia kwenye soko la ajira ndani na nje ya nchini hususani kwenye soko la ukanda wa Afrika Mashariki,” alisema Profesa Mkumbo.
Amesema kwamba mabadiliko ya uchumi wa taifa ni lazima yaende sambamba ya ukuaji wa teknoojia na kutoa nafasi kwa watanzania hususani taasisi za elimu ili kuweza kutoa mafunzo na kuandaa kizazi cha sasa na kijacho kwenye maendeleo ya sayansi na teknolojia ili waweze kushindana kwenye soko la ajira.
“Soko la ajira la siku za usoni sio tu vyeti bali uwezo wa watanzania kuweza kushindana kwenye soko la ajira zenye tija na ni muhimu kwa taasisi, vyuo vya ufundi na vyuo vikuu kuwajengea vijana uwezo zaidi wa kufanya kazi kwa kuleta matokeo Chanya kwenye mahali pa kazi,” aliongeza
Aliongeza kwamba Dira ya Taifa 2050 ni muongozo kwa watendaji wa serikali kuwataka kuwa wawajibikaji huku sekta binafsi ikijikita zaidi kwenye ubunifu , kuongeza tija na uwekezaji zaidi ili kufungua milango ya ajira na kukuza uchumi wa taifa.
Profesa mkumbo alisisitiza umuhimu kwa kuhakikisha watanzania wanapata fursa ya kuongeza nguvu kwenye teknolojia na maarifa ili Dira ya taifa iwe chachu ya kuleta mabadiliko kwenye maisha ya kila siku ya watanzania.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kitengo wa Benki ya Dunia kwa Tanzania , Malawi , Zambia na Zimbabwe , Bw Firas Raad amesema kwamba mwenendo wa uchumi wa Tanzania ni mzuri kutokana na mfumuko wa bei kuwa katika kiwango cha chini kinacholengwa na Benki Kuu ya Tanzania (BOT).
Alisema kwamba deni la serikali liko katika kiwango kinachoweza kudhibitiwa na huku hatari ya matatizo makubwa ya deni ikiwa kwenye kiwango cha wastani huku ukusanyaji wa mapato ukiongezeka na usimamizi wa sera za fedha na bajeti ukiendeshwa ndani ya mfumo unaoaminika.
“Katika zaidi ya miongo mitatu ambayo nimekuwa nikifanya kazi katika eneo la maendeleo ya kimataifa, nimetumia muda mwingi katika nchi zinazojitahidi kujenga misingi ya uchumi ambayo Tanzania tayari imefanikiwa kuiweka na kuiimarisha. Pia nimeona kwa karibu gharama ambazo uchumi na jamii hulipa pale misingi hiyo inapokosekana,” alisema.
Bw Raad aliongeza kwamba uchumi wa Tanzania ulikua kwa asilimia 5.9 mwaka 2025, huku ukuaji ukiwa wastani wa asilimia 5.7 kwa mwaka katika kipindi cha miongo miwili iliyopita.
Hata hivyo, ukuaji huo bado haujapunguza umaskini kwa kiwango kinacholingana na kasi ya ukuaji wa uchumi. Ukuaji huo umejikita katika shughuli zinazozalisha ajira chache kwa kulinganisha, wakati watanzania wengi bado wanaendelea kufanya kazi katika shughuli zenye tija ndogo.
Alifafanua kwaba idadi ya watanzania wanaoishi chini ya mstari wa kimataifa wa umaskini haijabadilika kwa kiasi kikubwa — ikipungua kwa kiwango kidogo tu kati ya mwaka 2018 na 2025.
Alisema kwamba hali hii ilimfanya Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Musa Omar kusema hivi karibuni katika hotuba yake ya bajeti kwamba: “Bado tuna kazi kubwa ya kufanya katika kupambana na umaskini.” Benki ya Dunia, tunashirikiana na tathmini hiyo kwa ujumla.
Aliongeza kwamba zaidi ya theluthi mbili ya watanzania walio katika umri wa kufanya kazi walikuwa wameajiriwa mwaka 2024 — ikiwa ni moja ya viwango vya juu vya ajira duniani. Hata hivyo, ajira nyingi kati ya hizo zipo katika shughuli zenye kipato kidogo na tija ndogo, huku zaidi ya nusu ya nguvu kazi ikiwa bado inajishughulisha na kilimo cha wakulima wadogo.
Amesema kati ya ajira milioni 26 zilizopo Tanzania, ripoti hiyo inaonyesha ushahidi wa takribani ajira 550,000 pekee zinazoweza kuchukuliwa kuwa ni ajira zenye ubora — yaani ajira zinazotoa malipo yanayostahili, mkataba wa maandishi, hifadhi ya jamii na usalama wa ajira.
Alisisitiza kwamba katika kipindi cha muongo mmoja uliopita, Tanzania imewekeza kwa kiasi kikubwa katika mtaji na miundombinu. uwekezaji huo unaonekana wazi na umechangia kwa kiasi kikubwa kuunda mwelekeo wa ukuaji wa uchumi wa Tanzania, na utaendelea kuwa na mchango huo kwa miongo ijayo.

Social Plugin