Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BALILE - MJI WA SERIKALI MTUMBA NI SOMO JIPYA LA UJENZI WA MIJI YA KISASA TANZANIA



Na Dotto Kwilasa, Dodoma

UPANGAJI wa miundombinu ya huduma muhimu chini ya ardhi katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma umetajwa kuwa somo kwa miji mingine nchini inayotafuta kuboresha mandhari, usalama na mifumo ya utoaji huduma.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, amesema uzoefu wa Mtumba unaonesha umuhimu wa kuzingatia mipango ya muda mrefu katika ujenzi wa miji, hususan namna ya kuweka miundombinu ya umeme, maji na mawasiliano.

Balile ameyasema hayo leo Oktoba 28,2026 Jijini Dodoma baada ya kushiriki ziara ya wahariri na waandishi wa habari katika Mji wa Serikali Mtumba, ambapo walijionea maendeleo ya ujenzi wa majengo na miundombinu ya Serikali.

Amesema jambo lililomvutia ni uwekaji wa nyaya na mabomba muhimu chini ya ardhi, utaratibu unaosaidia kuhifadhi mwonekano wa mji na kuondoa baadhi ya changamoto zinazoweza kujitokeza pale miundombinu hiyo inapowekwa juu.

“Kwa kweli tumefanya ziara hii kama wahariri na waandishi wa habari, tumeona ujenzi mkubwa unaoendelea kufanywa na Serikali katika Mji wa Serikali hapa Mtumba, Dodoma. Kwa kweli ni uwekezaji mkubwa na umeleta heshima ya pekee,” amesema.

Ameeleza kuwa mfumo huo unaweza kuwa rejea kwa maeneo mengine, ikiwemo Dar es Salaam, ambako katika baadhi ya maeneo nyaya za umeme na mawasiliano zinazoonekana juu zinaathiri mandhari na zinaweza kuibua changamoto za kiusalama.

Akitolea mfano wa Barabara ya Samora jijini Dar es Salaam, Balile amesema miji inapaswa kuzingatia upangaji wa miundombinu tangu mwanzo ili kupunguza changamoto zinazoweza kujitokeza kadiri shughuli za maendeleo zinavyoongezeka.

“Tunadhani kwamba kwa uzuri huu wa mji, ingekuwa vyema mji huu ukageuka somo, hata Dar es Salaam wafikirie kufanya kitu tunachokiona hapa Mtumba. Kwa kweli ni mji mzuri sana,” amesema.

Balile ametoa pongezi kwa Serikali, wahandisi na wataalamu waliohusika katika kuanzisha na kuendeleza mradi huo, akibainisha kuwa mafanikio ya ujenzi wa mji yanahitaji mipango madhubuti na uwekezaji unaozingatia mahitaji ya baadaye.

Aidha, amezipongeza Serikali za Awamu ya Tano na ya Sita kwa kuendeleza wazo la ujenzi wa Mji wa Serikali Mtumba, akisema mwendelezo wa mipango ya maendeleo ni muhimu katika kufanikisha miradi mikubwa ya kitaifa.

Amesisitiza kuwa uzoefu wa Mtumba unapaswa kuchochea mijadala kuhusu namna ya kuboresha mipango miji nchini, kwa kuzingatia usanifu wa majengo, usalama wa miundombinu na ubora wa mazingira ya maeneo ya makazi na shughuli za kiuchumi.






Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com