

Fundi Japhat Paschal akiwa ameshika risti aliyotoa kwa wananchi baada ya kuwachangisha fedha kwa madai ya kuwapelekea umeme.
Ofisa Uhusiano na Huduma kwa wateja wa TANESCO Wilaya ya Kahama, Robert Msemo akitoa elimu na utaratibu wa upatikanaji wa umeme kwa njia ya NIKONEKTI pamoja na *152*00#
Na Mwandishi Wetu, Malunde 1 blog Kahama.
WANANCHI wa Kitongoji cha Mhama Kijiji cha Igung’hwa Kata ya Kinaga Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, wamemkamata fundi anayesadikiwa kuwa ‘kishoka’' Japhet Paschal (40) na kumkabidhi kwa maofisa wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), baada ya kuwatapeli wananchi kwa kuwatoza Sh.30,000 kila kaya kwa madai ya kuwasajili katika mfumo ili wapatiwe huduma ya umeme.
Paschal alifika katika kitongoji hicho akiwa na ramani iliyodaiwa kuonyesha maeneo ambayo nguzo za umeme zingefungwa. Kwa kuwa baadhi ya alama zilizokuwa kwenye ramani hiyo zilionekana kuwa ndani ya maeneo yao ya makazi, wananchi walishawishika kumpatia fedha hizo wakiamini wangepatiwa huduma ya umeme kwa haraka.
Ili kuwashawishi zaidi wananchi kutoa fedha hizo, Paschal aliwapatia risiti za malipo zilizoandikwa kwa mkono, zikiwa na jina la “Japhat Paschal – Mkandarasi wa Umeme Majumbani na Viwandani” huku kiasi cha fedha kikitofautiana kulingana na ukubwa wa makazi yao.
Kukamatwa kwa fundi huyo kumetokana na elimu inayotolewa na TANESCO kuhusu namna ya kukabiliana na uharibifu wa miundombinu ya umeme pamoja na mafundi ‘vishoka’kupitia Ofisa Usalama wa Miundombinu wa TANESCO, Mhandisi Frank Njavike.
Akizungumza Septemba 25, 2026 siku ya Ijumaa mmoja wa wakazi wa kitongoji hicho, Andrew Makoye (46), amesema walipata taarifa kutoka kwa baadhi ya wananchi kwamba wangetembelewa na mkandarasi wa umeme kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), ambaye angewapimia maeneo na kuwasajili katika mfumo wa TANESCO ili wapate huduma ya umeme.
Makoye amesema Septemba 24, 2026, walimpokea mtu huyo na kumsikiliza, ambapo aliwataka kila kaya kutoa Sh.30,000 kwa ajili ya usajili katika mfumo ili wapate huduma ya umeme huku akidai kuwa wangetakiwa pia kulipa gharama nyingine kwa ajili ya ufungaji wa mifumo ya umeme ndani ya nyumba zao.
“Kitongoji ninachotoka kina zaidi ya kaya 28 na kila kaya imetoa Sh.30,000 na kuendelea ili ipate umeme. Awali tulimuamini kwa sababu alikuwa na ramani iliyoonyesha nguzo za umeme zitakapowekwa pale huduma itakapowafikia", amesema Makoye.
Amesema mashaka yalianza baada ya kupata taarifa kutoka kwa viongozi wa kijiji na kata kwamba hawakuwa na taarifa kuhusu ujio wa mtu huyo.
“Baadhi ya kaya zilikuwa bado hazijampatia fedha,
hivyo tulimuita aje kuchukua fedha. Alipofika tulimkamata na kutoa taarifa kwa TANESCO" Ameongeza.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Igung’hwa, Agness Kashinje, amesema viongozi hawakuwa na taarifa kuhusu fundi huyo kuwatembelea wananchi na kuwachangisha fedha, jambo lililowafanya kuanza kumfuatilia na baadaye kushirikiana na wananchi waliokuwa wamechangishwa fedha kumkamata.
Amesema utaratibu wa viongozi wa eneo hilo ni kupokea taarifa za wageni wanaoingia katika kata na kuwafahamisha wananchi kuhusu shughuli wanazokuja kuzifanya.
“Wageni wanaoingia katika kata yetu huwa tunapokea taarifa zao na kuwatambulisha kwa wananchi ili wajue ujumbe waliokuja nao. Huyu fundi ‘kishoka’ hatukuwa na taarifa zake, jambo lililotufanya kumtilia shaka na hatimaye kushirikiana na wananchi kumkamata"Amesema Kashinje.
Naye Diwani wa Kata ya Kinaga, Gerald Joseph amesema hapo awali kulikuwa na mafundi ‘vishoka’ waliofika katika maeneo hayo na kuwachangisha wananchi fedha kwa ahadi ya kuwafikishia umeme, lakini baadaye walitoweka bila kutekeleza ahadi zao.
Amesema baadhi ya mafundi hao walikamatwa baadaye mkoani Shinyanga, hatua iliyosababisha viongozi kushirikiana na TANESCO kutoa elimu kwa wananchi katika vitongoji na vijiji ili kujikinga na utapeli wa aina hiyo.
Amesema Kitongoji cha Mhama kilikuwa hakijafikiwa na elimu hiyo kwa wakati, jambo ambalo lilimpa nafasi fundi huyo kuwashawishi wananchi na kuwatoza fedha.
Akijieleza baada ya kukamatwa, Japhet Paschal amekiri kuwachangisha wananchi fedha na kuwapatia risiti zilizoandikwa kwa mkono kwa ajili ya kuwafungia mifumo ya umeme katika makazi yao na si kuwapelekea huduma ya umeme.
Amesema amekuwa akifanya kazi hiyo katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Kahama na kwamba baada ya kukamatwa amerejesha fedha zote alizowachangisha wananchi.
“Wapo ambao niliwatoza Sh.170,000 kulingana na ukubwa wa makazi yao. Niliwaeleza kuwa fedha za usajili katika mfumo wa TANESCO hulipwa kwa namba ya malipo (Control Number) inayotolewa na TANESCO nasio kama walivyosema hapa" Amesema.
Ofisa Usalama wa Miundombinu wa TANESCO Mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Frank Njavike amesema alipata taarifa kuhusu fundi huyo kuwachangisha wananchi fedha na kuwaagiza wananchi kuweka mtego ili kumkamata jambo ambalo walifanikiwa kulitekeleza.
Amesema hakuna fedha ya serikali inayotakiwa kupita mikononi mwa mtu binafsi, bali malipo yanapaswa kufanyika kupitia namba rasmi ya malipo (Control Number) inayotolewa na taasisi husika.
Njavike amesema kitendo cha fundi huyo kuwatoza wananchi fedha kwa utaratibu huo kinaweza kulichafua jina la TANESCO na watumishi wake.
Amesema fundi huyo aliwadanganya wananchi kuwa angewapelekea huduma ya umeme katika kitongoji ambacho hadi sasa hakijafikiwa na miundombinu ya umeme, ingawa eneo hilo limo katika mpango wa utekelezaji wa miradi ya kuwafikishia wananchi huduma hiyo.
Amewataka wananchi kuendelea kutoa taarifa kwa TANESCO au viongozi wa maeneo yao pale wanapokuwa na mashaka na watu wanaojitambulisha kuwa ni wahandisi au maafisa wa TANESCO au REA.







Social Plugin