Na Beda Msimbe, TBN, Petersburg, Urusi - Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezitaka nchi za Magharibi na wachambuzi wa mambo ya kisiasa kuondoa hofu yoyote ile kuhusu ushirikiano wa nchi yake na Urusi, akisisitiza kuwa Tanzania ni nchi isiyofungamana na upande wowote na inaongozwa na diplomasia ya kiuchumi yenye kulinda maslahi ya taifa kwanza.
Kauli hiyo imekuja kufuatia maswali na hisia zilizoibuka kuhusu ziara yake nchini Urusi, ambapo baadhi ya waandishi wa habari walieleza uwepo wa dhana kwamba Tanzania huenda inaikabili mgongo nchi za Magharibi na kugeukia upande wa Mashariki kiitikadi.
Akizungumza pembezoni mwa Jukwaa la Uchumi la Kimataifa la St. Petersburg (SPIEF), Rais Samia alifafanua kuwa Tanzania haihamishi nguvu zake kutoka upande mmoja kwenda mwingine, bali inatanua wigo wa washirika ili kukuza uchumi na kuinua maisha ya wananchi wake.
Rais alieleza kuwa msimamo huu una mizizi mirefu ya kihistoria tangu enzi za Muasisi wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ambaye miaka 57 iliyopita alipotembelea Urusi alisisitiza falsafa hiyohiyo ya kutofungamana na upande wowote.
Aliongeza kuwa Watanzania wa sasa wanachotaka ni diplomasia ya uchumi inayofungua fursa za biashara na uwekezaji, na serikali inakaribisha taifa lolote lililo tayari kushirikiana nayo bila kujali tofauti zao za kijiografia.
Akitolea mfano uwiano wa washirika wa Tanzania, Kiongozi mkuu huyo wa nchi alitaja kuwa nchi yetu ina uhusiano imara sana na Marekani, ambayo inaongoza kwa uwekezaji mkubwa nchini kukiwa na zaidi ya kampuni 500 za Kimarekani zilizowekeza katika sekta za utalii na migodi.
Vilevile alitaja ushirikiano mzuri na China katika sekta ya miundombinu na uchukuzi, India katika biashara, Japan katika nishati na elimu, pamoja na mataifa ya Ulaya, Australia, Uingereza, na Ufaransa yanayochangia maendeleo kupitia programu mbalimbali za uwezeshaji wa kifedha.
Rais Samia alihitimisha kwa kusema kuwa kuelekea utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2050 inayolenga kukuza uchumi kufikia thamani ya dola trilioni moja, Tanzania haitasita kushirikiana na nchi yoyote inayoweza kuwa mshirika mzuri wa kibiashara, kwani lengo kuu si ushindani wa kisiasa bali ni ustawi wa wananchi wa Tanzania.

Social Plugin