Na mwandishi wetu,Dar
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameongoza ujumbe wa Tanzania katika mazungumzo rasmi na ujumbe wa Jamhuri ya Singapore ulioongozwa na Rais wa nchi hiyo, Mhe. Tharman Shanmugaratnam, yaliyofanyika tarehe 09 Juni, 2026.
Mazungumzo hayo yamelenga kuimarisha na kupanua ushirikiano wa pande mbili kati ya Tanzania na Singapore katika maeneo mbalimbali ya kimkakati, ikiwemo biashara, uwekezaji, maendeleo ya rasilimali watu na ujuzi, pamoja na uchumi wa kidijitali.
Viongozi hao wawili walisisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano unaochochea ukuaji wa uchumi, kuongeza fursa za uwekezaji na kuimarisha ubadilishanaji wa uzoefu katika sekta mbalimbali zenye manufaa kwa mataifa yote mawili.
Baada ya mazungumzo hayo, Tanzania na Singapore zilishuhudia utiaji saini wa mikataba na hati za ushirikiano zinazolenga kuendeleza uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi kati ya nchi hizo mbili.
Shughuli hizo zilihitimishwa kwa mkutano wa pamoja na waandishi wa habari ambapo viongozi hao walieleza dhamira yao ya kuendelea kukuza ushirikiano na kuimarisha mahusiano ya kirafiki yaliyopo kati ya Tanzania na Singapore.



Social Plugin