Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Kuelekea kwenye zoezi la Uchaguzi Mkuu wa Tanzania litakalofanyika Jumatano, Oktoba 29, 2025, viongozi wa dini, kijamii na wananchi wa Mkoa wa Dodoma wameungana kwa pamoja kuhimiza amani, wakisisitiza kuwa amani ni rasilimali muhimu inayowezesha maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, viongozi hao wamesema amani ni zawadi ya thamani kubwa kwa taifa lolote duniani, hivyo kila Mtanzania ana jukumu la kuhakikisha inalindwa na kuendelezwa kwa vizazi vijavyo.
Mchungaji Pendo Yohana kutoka Kijiji cha Michese amesema amani ndiyo msingi unaoruhusu utekelezaji wa mipango ya maendeleo, huku Askofu Antony Saimon, Mwenyekiti wa Umoja wa Madhehebu ya Kikristo Mkoa wa Dodoma, akibainisha kuwa bila amani, hata huduma muhimu kama afya, elimu na biashara haziwezi kusimama.
Kwa upande wake, Sheikh Ahmed Said Ahmed, msemaji wa Sheikh wa Mkoa wa Dodoma, amewataka Watanzania kuendelea kuwa walinzi wa amani, akisisitiza kuwa tofauti za kisiasa, kiimani au kijamii hazipaswi kuwa chanzo cha mifarakano.
“Amani siyo jambo la bahati. Ni matokeo ya busara, upendo na utiifu wa sheria. Kila mmoja wetu ana jukumu la kuilinda,” amesema Sheikh Ahmed.
Tafiti mbalimbali zinaonesha uhusiano wa moja kwa moja kati ya amani na maendeleo ikiwemo uboreshaji wa uchumi wa wananchi, ustawi wa huduma za kijamii, na ujenzi wa taifa lenye uthabiti wa kiusalama na ustawi wa watu wake.
Aidha, wananchi wa kawaida pia wamejitokeza kuunga mkono wito huo. Emmanuel Kamome, dereva wa bodaboda kutoka Dodoma, amesema kuwa atatumia nafasi yake kuelimisha wenzake kuhusu umuhimu wa kudumisha amani, huku Shukuru Chimwaga, msemaji wa Chama cha Waigizaji Mkoa wa Dodoma, akiahidi kutumia sanaa kama jukwaa la kuhamasisha wananchi kuepuka vurugu hasa kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi.
“Sanaa ni silaha ya kuleta umoja na maridhiano. Tumeamua kutumia vipaji vyetu kuhubiri amani badala ya migogoro,” amesema Chimwaga.
Viongozi wa dini na wananchi hao wameungana na wagombea mbalimbali wa nafasi za uongozi, akiwemo Dkt. Samia Suluhu Hassan, mgombea wa urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye mara kadhaa amesisitiza umuhimu wa vijana na jamii kuepuka kutumiwa na watu wenye nia ovu kuvuruga amani ya nchi kwa kisingizio cha uchaguzi.
Kwa mujibu wa Dkt. Samia, uchaguzi ni tendo la kidemokrasia linalolenga kuchagua viongozi bora, siyo sababu ya kuanzisha vurugu, mivutano au mgawanyiko wa kijamii.
Kwa ujumla, ujumbe wa viongozi hao wa dini na wananchi wa Dodoma umebeba ujumbe mzito wa uzalendo na umoja, ukikumbusha Watanzania wote kuwa amani ndiyo nguzo kuu ya maendeleo na ustawi wa Taifa.





Social Plugin