e-GA YAKABIDHI KOMPYUTA 10 KWA JESHI LA POLISI



Na Mwandishi wetu,Dar Es Salaam.

Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) imetoa mchango wa kompyuta 10 kwa Jeshi la  Polisi nchini, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha matumizi ya teknolojia katika utoaji wa haki kwa wananchi.


Makabidhiano hayo yamefanyika  katika Ofisi za Mamlaka jijini Dar es Salaam ambapo kwa upande wa e-GA Bw. Benjamin Dotto  Mkurugenzi wa Miundombinu na Uwezeshaji wa TEHAMA alikabidhi komputa hizo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu Mhandisi. Benedict Ndomba. 


Akiongea wakati wa makabidhiano hayo,  Dotto amesema kuwa, e-GA imekuwa ikishirikiana na Taasisi mbalimbali za Umma likiwemo Jeshi la Polisi, katika kuhakikisha matumizi ya Teknolojia yanarahisisha utendaji kazi wa Taasisi na utoaji wa huduma kwa umma.


“Teknolojia hurahisisha mchakato wa utoaji wa haki na sisi e-GA tukaona ni vizuri kuchangia kwa kutoa kompyuta hizi ili zirahisishe mchakato wa haki jinai katika Jeshi la Polisi”, amesema Dotto.


Kwa upande wake, Mkuu wa TEHAMA wa Jeshi la Polisi Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Justus Mafuru amesema kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ameagiza kutengeneza Mfumo wa haki jinai ambao tayari umekwishatengenezwa.


“Kwa niaba ya IGP tunaishukuru e-GA kwa mchango huu wa kompyuta ambao utasaidia upatikanaji wa haki kwa wananchi kwa urahisi na haraka kupitia Teknolojia na kwakuwa Mfumo wa hakijinai umekwishatengenezwa kwa sasa tunahitaji vifaa”, aameema ACP Mafuru.


Mamlaka ya Serikali Mtandao ni Taasisi ya Umma iliyoanzishwa kwa Sheria ya Serikali Mtandao Na. 10 ya mwaka 2019, ikiwa na majukumu ya kuratibu, kusimamia na kukuza jitihada za Serikali Mtandao, pamoja na kusimamia uzingatiaji wa Sera, Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao katika taasisi za umma.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments