WAFUGAJI WATAKIWA KUMILIKI MAENEO NA KUPANDA MALISHO


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kegonga wilayani Tarime mkoani Mara, ambapo amewaeleza wananchi hao kumiliki maeneo kwa ajili ya shughuli za ufugaji na kupanda malisho.

Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Mhe. Kanali Michael Mtenjele akiwasalimu wananchi wa Kijiji cha Masanga wilayani humo wakati wa ziara ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi wilayani humo.


Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mhe.Mwita Waitara akiwasalimia wananchi wa Kijiji cha Kegonga wilayani Tarime mkoani Mara ambapo ameishukuru serikali kwa jitihada zinazofanyika za kupeleka maendeleo, lakini ameomba tatizo la migogoro kati ya wafugaji na hifadhi ya mbuga ya Serengeti kuhusu mipaka litatuliwe.


Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Kegonga wilayani Tarime mkoani Mara wakimsikiliza Waziri wa Mifugo na Uvuvi (hayupo pichani) wakati alipofanya ziara ya kikazi katika Kijiji hicho na kuzungumza na wananchi hao.

.......................


Wafugaji wilayani Tarime wametakiwa kumiliki maeneo na kupanda majani kwa ajili ya malisho ya mifugo yao.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashamba Ndaki alipokuwa anazungumza na wananchi wa Kijiji cha Karekatonga wilaya ya Tarime mkoa wa Mara baada ya kusikiliza kero zao.

Waziri Ndaki amesema kuwa wafugaji wanatakiwa kubadilika na kuanza kufuga kisasa na kibiashara kwa kuhakikisha mifugo wanayofuga inapata malisho ya kutosha kulingana na maeneo wanayoyamiliki pamoja na huduma za mifugo.

Malisho ni moja ya changamoto kubwa inayowakabili wafugaji wengi na hivyo kusababisha mifugo kufa hasa kipindi cha ukame. Hivyo wafugaji wameshauriwa kumiliki mifugo inayoendana na eneo la malisho wanayomiliki.

Vilevile Waziri Ndaki amekemea vikali suala la upigwaji risasi mifugo linalodaiwa kufanywa na askari wa wanyamapori. Wananchi katika vijiji vinavyoizunguka Mbuga ya Serengeti wamelalamikia tatizo hilo na hivyo kumuomba Mhe. Waziri kuwasaidia wafugaji hao.

Aidha, Waziri Ndaki amekemea vikali suala la mifugo kupigwa risasi kwa kuwa lipo kinyume na sheria zinazolinda mifugo hapa nchini. Hii ni kutokana na wananchi hao kulalamika kuhusu mifugo yao kupigwa risasi na askari wa wanyamapori.

Naye Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mhe. Mwita Waitara amesema kuwa serikali katika jimbo hilo imefanya mambo mengi ya maendeleo lakini wananchi wameomba suala la alama za mipaka kati ya vijiji na eneo la hifadhi ya Serengeti liwekwe wazi ili kuondoa migogoro iliyopo sasa kati ya wafugaji na askari wa wanyamapori.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments