TARURA YASHAURIWA KUACHA UJENZI WA BARABARA ZA UZITO WA TANI KUMI

Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) wametakiwa kuachana na ujenzi wa barabara za kiwango cha lami zenye uwezo wa kubeba magari yenye uzito wa tani kumi (10), na badala yake wajenge barabara zenye uwezo wa kuhimili uzito wa tani thelathini (30) ili kuongeza tija kwa wananchi katikika shughuli za usafirishaji wa mazao. 

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa (USEMI) Mhe. Abdallah Chaurembo (Mb) wakati wa ziara ya kamati hiyo katika Mkoa wa Iringa kukagua ujenzi wa barabara za mradi wa “Agri-Connect” unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Jumuia ya Ulaya katika wilaya za Mufindi na kilolo.

“Tumeona barabara hii imejengwa kwa uwezo wa kupitisha tani 10, sasa sisi kama kamati tumeshauri TARURA wajenge barabara zeneye uwezo wa kuhimili tani 30 ili wananchi waweze kufanya biashara zao za mazao kwa furaha bila bughudha,” alisema Mhe. Chaurembo.

Pia alieleza kuwa wananchi kwa muda mrefu walikuwa na kilio cha barabara ambazo zinatoka kwenye uzalishaji kupeleka masokoni, ambapo mradi huu sasa umejibu kilio hicho baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuridhia fedha za ujenzi kwa barabara hizo ambazo sasa zimerahisisha usafirishaji.

Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI (Afya) Dr. Festo Dugange (Mb) alisema kuwa kazi kubwa na nzuri imefanyika katika ujenzi wa barabara hiyo ambayo itafungua uchumi na kurahisisha shughuli za kijamii kwa wananchi.

“Dhamira ya Serikali inayoongozwa na Rais samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kuwa inafungua miundombinu na uchumi wa wananchi wakiwemo wananchi wa Mufindi. Hivyo tunatarajia barabara hii sasa itakuwa mkombozi mkubwa wa kiuchumi na shughuli za kijamii; na jukumu la OR-TAMISEMI ni kuhakikisha kwamba barabara zinajengwa kwa ubora na kukamilika kwa wakati na kutimiza malengo ya Serikali yaliyopangwa, “alisema Dr. Dugange.

Naye Mhe. Thea Ntara (Mb) alisema kuwa barabara hii itawasaidia sana wakulima siyo tu wa mazao ya chai na mbogamboga bali hata wakulima wa mazao ya miti kama mbao na magogo hivyo kusaidia kukua kwa uchumi wa wananchi wa Mufindi na Mkoa wa Iringa kwa ujumla, ikiwa ni pamoja na kuwavutia wawekezaji.

Kwa upande mwingine diwani wa kata ya Mtwango, Mhe. Monte E. Kalamlya alisema kuwa barabara hiyo imekuwa ni chachu kwa wananchi wa kata ya Luhunga na wanaotoka vijiji vya jirani kwa sababu imefanya nauli zimepungua na kurahisisha usafiri na usafirishaji wa mazao ambalo ni lengo la serikali kuhakikisha kuwa Maisha ya mwananchi yanakuwa nafuu.

“Kwakweli kupitia barabara hii mazao yetu ya chai yatafika haraka kwenda kiwandani na uchumi sasa utaenda kufunguka kwa kasi na maendeleo yatapatikana, na wananchi wameipokea kwa mikono miwili,” alisema

Mradi wa Agri-Connect katika Mkoa wa IIringa, wilaya ya Mufindi unahusisha barabara ya Sawala- Mkonge-Iyegeya yenye urefu wa kilomita 30.3 iliyojengwa kwa thamani ya shilingi 8,167,087,887.00.

Mradi huo lengo lake kuu ni kurahisisha usafirishaji wa mazao ya Mboga mboga, Chai, matunda na mazao mengine toka mashambani kwenda mikoa mingine au kwenda viwandani ama katika maghala ya kuhifadhia.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments