FCS YAZINDUA MPANGO MKAKATI MPYA KUSAIDIA WANANCHI... DKT. TENGA ATAKA ASASI ZA KIRAIA KUSHIKAMANA

Rais wa Taasisi ya Foundation For Civil Society (FCS) Dkt. Stigimana Tenga amezitaka Asasi za kiraia nchini kushikamana kwa pamoja na kuhakikisha wanazisemea kazi wanazofanya katika Taasisi zao ili ziweze kufahamika kwa wananchi na jamii kwa ujumla.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mpango Mkakati mpya wa Foundation For Civil Society (FCS) Dkt. Tenga amesema Asasi za Kiraia zinapaswa kujengwa kutokana na kwamba ni muhimili mkubwa wa maendeleo nchini na wananchi wanapaswa kuzifahamu.

Pia amezitaka Asasi hizo kuhakikisha zinaangalia mifumo mbalimbali inayowaongoza ambayo ndiyo miundombinu ya uwajibikaji katika kazi zao hususani katika kutatua matatizo ya wananchi.

“Tuisemee sekta hii na yale yote ambayo sekta hii inayafanya kwenye jamii, yasemeeni mnayoyafanya ili yajulikane msione aibu yeyote,”alisema Dkt. Tenga.

Aliongeza kuwa Asasi zinapaswa kutatua matatizo ya wananchi na kusaidia kuyaondoa hilo ndiyo lengo kubwa la FCS katika Dira yake.

“Tujenge uwajibikaji katika misingi ya ubinadamu na utu bila kujali kuna nini, bali kuwashirikisha wenzetu matatizo ambayo sekta ya Asasi za kiraia nchini inapitia ambayo yanahitaji kutatuliwa kwani ni matatizo yanayojikita katika mifumo,” aliongeza Dkt. Tenga.

Aidha alisema hawapaswi kutatua matatizo kwa mbinu zile zile za zamani ambazo sio mbinu za kujenga mifumo bali ni mbinu za kutoa huduma.

“Tusipoangalia hivyo tutazidi kuona hizo mbinu zinaongezeka na kuwa kubwa sana na kuhakikisha wanaangalia mifumo ambayo ndio miundombiniu ya uwajibikaji katika asasi,” alisema.

Kwa Upande wake,Mkurugenzi Mtendaji wa FCS Francis Kiwanga alisema wamezindua mpango mkakati mpya wa FCS ambao unalenga kushuka chini hususani vijijini katika kuwasaidia wananchi.

Alisema kupitia mpango huo, Taasisi yao itaendelea kufanya kazi na Asasi mbalimbali za kiraia ambao ndiyo wadau wao muhimu katika kuwafikia wananchi.

Alisema falsafa ya Taasisi yao inaamini kuwa umaskini,hali ya kutokuwa na haki katika jamii,hali ya ukandamizaji watu wengine ni tatizo kubwa na ni adui wakubwa wa maendeleo.

Alisema katika rasilimali zao takribani asilimia 90 zinakwenda vijijini kuhudumia wananchi.

“Rasilimali zetu tunayogawa kila mwaka asilimia 90 inakwenda vijijini ,tunaamini waliopo Dar es Salaam ,Taasisi nyingi zinaweza kufanya kazi na watu wengine kokote duniani kuliko waliopo vijijini” alisema Kiwanga.

Pia aliongeza kwa kusema kuwa katika mpango kazi wao wanazingatia usawa wa kijinsia,kufanya kazi na wadau wao kuwapa heshima inayostahili na kuwaheshimu kwani wao ndio wabia wao wakubwa na kwamba sauti yao ina ukubwa wa kuweza kuwafikia wananchi.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Asasi za kiraia, Dkt. Richard Samabiga aliipongeza FCS kwa hatua hiyo ya kuzindua mpango mkakati huo ambao unaonyesha dira ya kusaidia wananchi katika maeneo mbalimbali.

Alisema mpango huo unaleta matumaini makubwa kwa Asasi za kiraia katika kufanya kazi zao za kusaidia wananchi.

Mpango mkakati huo umejikatika katika kutekeleza miradi ya utawala bora, usawa wa kijinsia na watu wenye ulemavu, kukuza uchumi na kujenga amani na utatuzi wa migogoro.
Rais wa FCS Dkt. Stigimana Tenga akizungumzia mpango huo mara baada ya kuzinduliwa rasmi mwishoni mwa wiki Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa FCS Francis Kiwanga (wa tatu kulia) akiwa na Rais wa Taasisi hiyo Dkt. Stigimana Tenga (katikati) na mwenyekiti wa Bodi ya FCS Dkt. Richard Samabiga (wa kwanza kulia) wakiangalia mpango mkakati utakaotekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano mara baada ya kufanyika uzinduzi rasmi wa mpango huo uliofanyika mwishoni mwa wiki kwenye Ofisi za FCS Jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mtendaji wa FCS Francis Kiwanga akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi huo akielezea namna ambavyo FCS itavyotekeleza majukumu yake katika kuusimamia mpango huo.
Baadhi ya watumishi wa FCS na wageni mbalimbali waalikwa wakiwa kwenye hafla ya uzinduzi huo.



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments