POLISI WATOA MSIMAMO...WAMPA SOMO KANGI LUGOLA KUHUSU MBWA,ZITTO KABWE


Na Fortune Francis na Bakari Kiango, mwananchi
Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola alitumia dakika chache kuulizia alipo mbwa wa polisi na kumuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi atoe majibu ndani ya saa saba, lakini Jeshi la Polisi likatumia saa 336.
Waziri akaagiza jeshi hilo kumkamata kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe baada ya siku mbili, lakini kabla hazijaisha polisi wametoa msimamo.
Na maelezo yao yanaweka maswali kuhusu ushirikiano wa utendaji kazi kati ya wateule hao wawili wa Rais.
Jana msemaji wa Jeshi la Polisi, Baranabas Mwakalukwa aliitisha mkutano na waandishi wa habari na kuwaeleza utaratibu wa chombo hicho cha dola katika kushughulikia wanaovunja sheria na pia taratibu za mbwa wanaowatumia katika shughuli zao.
Kuhusu agizo lake la kutaka Zitto ajisalimishe ndani ya siku mbili au polisi imkamate kwa madai kuwa alikiuka agizo la Rais la kuzuia wanasiasa kufanya mkutano nje ya maeneo yao, Mwakalukwa alisema watamkamata iwapo watajiridhisha kuwa alifanya kosa kama taratibu zao zinavyotaka.
Mwakalukwa alisema tayari wamefungua jalada la uchunguzi kuhusu tuhuma zinazomkabili na kwamba uchunguzi unaendelea.
“Jeshi la Polisi linafanya kazi kwa mujibu wa taratibu na sheria,” alisema Mwakalukwa.
“Hivyo tutakapomuita, ataripoti kwa kamanda wa polisi mkoa wa Lindi kwenye himaya ambako atatuhumiwa kufanya kosa hilo.”
Kauli hiyo ni tofauti na maagizo ya Lugola kwamba iwapo Zitto hatajisalimishe kwa kamanda wa polisi wa Lindi, angeagiza IGP amkamate popote alipo.
Mbali na kuagiza akamatwe, Lugola alitaja mashtaka ya Zitto kuwa ni kukiuka agizo la Rais na kutukana viongozi.
“Baadhi ya Watanzania wenzetu wanatoa kauli za uchochezi na kutukana viongozi, pia (huko) bado ni kukaidi agizo la Rais,” alisema Lugola wakati akitoa maagizo hayo akisisitiza kuwa wabunge ndio wenye tabia hiyo. Lugola pia alimuagiza IGP Sirro kumchukulia hatua kamanda wa polisi wa wilaya ya Kilwa kwa kushindwa kuchukua hatua dhidi ya Zitto ambaye pia ni mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini.
Hii ni mara ya pili kwa Jeshi la Polisi kusimamia taratibu zake baada ya kupewa amri na waziri. Awali, Waziri wa Maliasili na Utalii alilipa siku saba likamate watu wanne kwa madai kuwa wanajihusisha na ujangili, lakini chombo hicho kikasema kimepokea maagizo hayo “lakini hakifanyi kazi kwa shinikizo” kwa kuwa kina taratibu zake.
Wakati polisi wakisema hayo, katibu wa itikadi na uenezi wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu amesema Zitto hatatii agizo la Lugola.
Shaibu aliwaambia wanahabari jana kuwa wanasheria wa chama hicho wamelipitia agizo la Lugola kwa undani na kujiridhisha kuwa lina makosa na halina nguvu kisheria.
Alisema Lugola hakutafakari kabla ya kutoa agizo hilo na badala yake ametumia siasa zaidi badala ya sheria.
“Zitto akiitwa kisheria ataenda kuripoti polisi na hatuna sababu ya kuogopa,” alisema Shaibu.
“Zitto ni kiongozi na mbunge akiitikia wito huu wa Lugola atakuwa hajiheshimu yeye na chama hiki. Yaani tumetesti mitambo mara moja tu, pale Kilwa kwa kumpandisha jukwaani Zitto imekuwa nongwa watu wanalipuka? Hatuwezi kuvumilia hali hii.”
Shaibu alimshauri Lugola kuwa mtulivu katika kuiongoza wizara hiyo na kuzingatia sheria.
Alisema wizara hiyo ni nyeti na inagusa haki na utu wa Watanzania na kumkumbusha kauli zake mbili kuhusu sakata la kupotea kwa mwandishi wa habari wa Mwananchi, Azory Gwanda.
Mbwa alikuwa mafunzoni
Katika tukio jingine linaloonyesha utata katika utendaji kazi wa wateule hao wawili, Jeshi la Polisi limeeleza kuwa hakuna mbwa aliyetoroshwa kutoka Bandari ya Dar es Salaam na badala yake alikuwa mafunzoni.
Lugola alitaka maelezo ya mbwa huyo Julai 19 baada ya kubaini katika daftari la bandari kuwa alitoka lakini hakurejeshwa kama ilivyokuwa kwa mbwa wengine.
Kitendo hicho kilimfanya amuagize IGP Simon Sirro aliyekuwepo siku hiyo, ampe majibu saa 12:00 jioni siku hiyo.
Lakini jana, Mwakalukwa alisema mbwa anayejulikana kwa jina la Hobby alikuwepo kikosini siku Waziri alipotembelea na ana afya nzuri akiendelea na majukumu yake ya kila siku.
Alisema, mbwa ambaye hakuwepo siku huyo, yaani Julai 19, ni Gilo, ambaye alisema yuko kwenye mafunzo Bwalo la Polisi, Oysterbay na yataisha Septemba 12.
Kuhusiana na kutoonekana kwa mbwa zaidi ya 30, kamanda wa kikosi cha mbwa na farasi Eugine Emmanueli alisema hakuna mbwa hata mmoja aliyepotea bali wanyama hao huenda kwenye majukumu na baadaye hurejeshwa.
“Mbwa wanatoka na kwenda kwenye kazi na wengine hubaki kwa ajili ya usalama,” alisema.
“Si lazima kuandika au kuieleza jamii mbwa huyu ameenda wapi.”
Hata hivyo, mwishoni mwa mwezi uliopita, Waziri Lugola aliwaambia waandishi wa habari kuwa tayari Hobby amepatikana.
Theme images by rion819. Powered by Blogger.