CCM KUACHANA NA SIASA ZA KUSIFU MTU | MALUNDE 1 BLOG

Tuesday, August 14, 2018

CCM KUACHANA NA SIASA ZA KUSIFU MTU

  Malunde       Tuesday, August 14, 2018

Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amesema chama hicho kimejipanga kuondokana na siasa za kusifu mtu.


Alisema hayo jana jijini Dar es Salaam katika mkutano na waandishi wa habari kuzungumzia mafanikio ya chama chake katika uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata 77 na ubunge wa Jimbo la Buyungu.


Baadhi ya wanachama wa vyama vya upinzani wakiwamo wabunge na madiwani ambao wanavihama vyama vyao na kujiunga na CCM wengi wamekuwa wakieleza sababu kuwa ni kuunga mkono juhudi za Rais John Magufuli.


Akijibu maswali ya waandishi wa habari jana kuhusu suala hilo, Dk Bashiru alisema CCM ni chombo chao na Tanzania ni yao.


“Kama ambavyo Tanzania itakuwapo bila Magufuli na CCM itakuwapo bila Magufuli. Kama ambavyo ipo bila Mzee Karume na Mzee Nyerere. Tupo na mimi hapa nipo. CCM chini ya Bashiru, chini ya Kinana, chini ya Makamba, chini ya Mangula, chini ya Mkama ipo,” alisema Dk Bashiru.


Alisema, “Tunataka kuua siasa za ubinafsi, za nafsi moja, za mtu mmoja na Rais Magufuli hapendi kutajwa kama mtu mmoja, hapendi majivuno na hawezi kuwa na majivuno ndani ya CCM. Akiwa na majivuno amepoteza sifa na sifa kubwa inayompamba na kukipamba chama chetu ni mtu wa watu anayeleta maendeleo kwa watu na yeye ni mtu. Kwa kuwa ni mtu, atakuwapo na hatakuwapo.”


Dk Bashiru alipoulizwa ni kwa nini wasiwaambie wahamiaji wa CCM kufuta kauli hiyo alisema haiwezekani kwa kuwa Rais Magufuli ndiye mshika chombo.


“Chombo kitakwenda mrama. Anasifiwa mwendesha chombo kwa sababu chombo chenyewe ni madhubuti na amehimili usukani. Ukifunga bao, unasifiwa wewe, timu inapata sifa,” alisema.


“Tunataka kuua utaratibu wa siasa za kusifu mtu, mwenyekiti wa chama kile au hiki, akiondoka kinadondoka naye. Tunataka kiongozi na sifa za kiongozi lazima zielekeze kwake kwa niaba ya anaowaongoza. Ukiona sifa zake kwa anaowaongoza pia wanakuwa nazo,” alisema.


Kauli ya Dk Bashiru imekuja siku chache baada ya Rais mstaafu, Benjamin Mkapa kutaka Serikali itambulishwe kuwa ya CCM na si ya mtu.


Mkapa alitoa kauli hiyo katika mkutano wa viongozi wastaafu ulioandaliwa na Rais Magufuli Ikulu ya Dar es Salaam.


Rais huyo wa Awamu ya Tatu alisema angependa kusikia zaidi Serikali ikijitambulisha kama Serikali ya CCM hasa kwa mawaziri.


“Ni Serikali ya CCM inaongozwa na Rais wetu Magufuli lakini naye ni Rais wa CCM na CCM ndiyo iliyompa urais. Kwa hiyo hii ya kusema mimi, mimi, aah! Ni Serikali ya CCM, itajenga hamasa ya kuhakikisha inachaguliwa tena,” alisema Mkapa.


Hoja hiyo inashabihiana na ile iliyotolewa hivi karibuni na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad akiwa New York, Marekani.


Akizungumzia mafanikio ya malengo ya maendeleo endelevu (SDG), Profesa Assad alisema yatategemea kuimarishwa kwa mifumo ya taasisi na si viongozi wenye nguvu.


Profesa Assad akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Redio Umoja wa Mataifa alisema, “Tumekuwa na ‘strong personalities’ (watu wenye nguvu) badala ya kuwa na ‘strong institutions’ (taasisi zenye nguvu.”


Dk Bashiru katika mkutano na waandishi jana alisema, “Tumetoka katika zama za kusifu mtu, Tunapomtumia Rais Magufuli, ni kiongozi nyuma, yake kuna umma wa wanachama na wananchi. Lakini ili umma huo uwe na mwelekeo anakuwepo kiongozi,” alisema.


Katibu mkuu huyo alisema, “Kwa hiyo Rais Magufuli ukimtaja, zungumza kama mwenyekiti wa CCM iliyowahi kuongozwa na Mwalimu Nyerere, Mzee Mwinyi, Mzee Mkapa, Mzee Kikwete naye atakuwa Mzee Magufuli.”

Na Elias Msuya, Mwananchi
Usikubali kupitwa na habari..Pakua App ya Malunde1 blog HAPA Ili tuwe tunakutumia habari moja kwa moja Kwenye Simu yako
Loading...
logoblog

Kama Una Habari,Picha,Video,Tangazo n.k Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 757 478 553 ,0625 918 527

Malunde 1 blog Ipo PlayStore....Pakua App yetu mpya HAPA Upate Habari Mpya Moja Kwa Moja Kwenye Simu yako..Utasoma habari hata kama hauna MB..Bofya Hapa
https://play.google.com/store/apps/details?id=com.malunde.blog
Previous
« Prev Post