Saturday, May 26, 2018

MUME AUA MKEWE KISHA KUMZIKA

  Malunde       Saturday, May 26, 2018

MUUGUZI wa Hosptali ya Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, Rosemery Magombora (43, anadaiwa kuuawa na mume wake, Robert Ruyange, kwa kumpiga kwa gongo na kisha kumzika pembeni ya nyumba yao. 

Shangazi wa marehemu, Veronica Makonda, amesimulia tukio hilo na kudai kuwa Rosemary alikuwa na ugomvi wa mara kwa mara na mzazi mwenzake. Alisema Rosemary alikuwa na tabia ya kwenda kwao Buza kila Ijumaa na kurudi kwake Mkuranga na mara ya mwisho alitokea kwake Jumatatu iliyopita.

“Baada ya kutoka kwangu siku ya Jumatatu iliyopita asubuhi, aliniiarifu amefika salama na anajiandaa kwenda kazini lakini baada ya muda si mrefu mumewe alinipigia simu kuwa mkewe kasahau simu kwenye gari….nilishangaa maana nilikuwa nimeongea naye muda si mrefu,” alisema na kuongeza:

“Nikashangaa mpaka saa nne asubuhi hajanipigia simu kuniuliza lolote maana ni kawaida yetu kuzungumza mara kwa mara na huwa kila muda ananiuliza shangazi umekula, lakini nikaona kimya, nikaanza kuwa na wasiwasi,” alisema.

Baada ya saa nyingi kupita, alisema alimpigia simu majira ya saa tano lakini alikuwa hapatikani ndipo alipoamua kwenda Mkuranga kituo cha polisi na kutoa taarifa hiyo.

“Nilipofika polisi waliniuliza kama nina mashaka na nani, nikawaambia nina wasiwasi na mumewe ndiye anaweza kujua alipo kwani mara nyingi Rose amekuwa akiniambia kuwa ana ugomvi na mumewe na kuwa wamekuwa wakilala vitanda tofauti kwa muda mrefu,” alisema.

Veronoka alisema Rosemary alizaa mtoto mmoja na Ruyange na waliishi pamoja kwa zaidi ya miaka minne.

Mganga Mfawidhi wa Hosptali ya Mkuranga, Steven Mwandambo, amekiri kuwa muuguzi huyo amefariki dunia na kuelezea kuwa walikuwa wakimtafuta tangu Jumanne bila mafanikio hadi walipopata taarifa za mauaji hayo.

"Polisi walimhoji mtuhumiwa ambaye alikiri amefanya tukio hilo na kama unavyoona tupo hapa, kazi ya kuufukua mwili wa marehemu inaendelea na tutauhifadhi hospitalini taratibu nyingine zitaendelea," alisema Dk. Mwandambo. 

Mkurugenzi Mtendaji wa Mkuranga, Mshamu Munde, alimwelezea Rosemary kuwa alikuwa mchapakaz hodari na hakuwahi hata siku moja kukosa kwenda kazini lakini walishangaa Jumatatu hakutokea kazini.

"Wakati tukijiandaa kwenda nyumbani kwa marehemu njiani tulikutana na mume wake ambaye naye alidai anakuja ofisini kutoa ripoti ya mke wake kupotea. Tulishangaa sana na tulianza kufuatilia suala hilo hadi polisi lakini mwisho wa siku ukweli ukadhihirika kuwa kumbe mumewe alimuua,” alisema .

Alisema Rosemary alikuwa ofisa muuguzi wa hosptali hiyo na alikuwa mtumishi mwadilifu na kuwa kifo chake kimeacha simanzi kwa wafanyakazi wenzie.

Polisi walifika na kuufukua mwili wa marehemu na mume wake anayedaiwa kufanya tukio hilo ndiye aliyewaelekeza.
Chanzo- Nipashe
Usikubali kupitwa na habari..Pakua App ya Malunde1 blog HAPA Ili tuwe tunakutumia habari moja kwa moja Kwenye Simu yako
Loading...
logoblog

Kama Una Habari,Picha,Video,Tangazo n.k Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 757 478 553 ,0625 918 527

Malunde 1 blog Ipo PlayStore....Pakua App yetu mpya HAPA Upate Habari Mpya Moja Kwa Moja Kwenye Simu yako..Utasoma habari hata kama hauna MB..Bofya Hapa
https://play.google.com/store/apps/details?id=com.malunde.blog
Previous
« Prev Post