Wednesday, May 16, 2018

JINSI LULU ALIVYONASWA MTAANI LEO AKITOKA KUTUMIKIA ADHABU YAKE

  Malunde       Wednesday, May 16, 2018

Msanii wa Filamu nchini, Elizabeth Michael ‘Lulu’ akiondoka katika ofisi za Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi baada ya kutumikia adhabu yake ya kifungo cha nje kwa kufanya usafi katika ofisi hizo zilizopo eneo la Posta Mpya jijini Dar es Salaam leo. Lulu atatumikia kifungo hicho mpaka novemba 12 mwaka huu. Picha na Ericky Boniphace 
****
Tofauti na siku nyingine, hali ya hewa ya jiji la Dar es Salaam inaonekana shwari kiasi. Manyunyu ya mvua yamekatika, kuna jua ambalo limeambatana na wingu la kawaida.

Katika geti la kuingia na kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani, wanaonekana watu wachache wakiingia na kutoka, kila mmoja ana jambo lake lililomleta wizarani hapo.

Huku hali ya hewa ikisoma kuwa joto la Dar es Salaam Jumatano ya Mei 16 ni nyuzi joto 29 °C, watu wanaonekana kuifurahia hali hiyo tofauti na mvua zilizonyesha mfululizo kwa siku kadhaa.

Kuna ukimya kidogo, macho ya baadhi ya wafanyakazi wa mapokezi katika geti la Wizara ya Mambo ya Ndani, yanaelekezwa katika mlango mkuu wa kuingilia wizarani. Ninapoyainua macho yangu nakutana na msichana mrembo akitoka katika jengo la wizara hiyo.
Saa yangu ya mkononi inasoma kuwa ni saa 4:15 asubuhi, namkodelea macho mrembo huyo anayetembea bila wasiwasi akielekea katika geti la kutokea.

Gari dogo jeusi aina ya Toyota Camry lililokuwa limefika na kuegeshwa kwa muda mfupi ndani ya uzio, linaonekana likisogea kwenye geti la kutokea.

Akiwa amevaa dera jekundu huku akiwa amebana nywele zake kwa staili ya kidoti, mrembo huyo analisogelea gari hilo na anapoingia katika siti ya nyuma, gari linaondoka kwa mwendo wa kawaida kabla na kukata kona kuelekea maeneo ya Posta.
Huyo ni Elizabeth Michael, ambaye ameanza maisha mapya ya kifungo cha nje katika Wizara ya Mambo ya Ndani tangu Jumatatu wiki hii.

Ametimiza siku ya tatu tangu aanze kutumikia jamii katika Wizara ya Mambo ya Ndani. Ameshatimiza saa 12 kati ya saa 512 anazodaiwa mpaka atakapomaliza kifungo hicho cha nje Novemba 12, mwaka huu.

Mmoja wa wafanyakazi wa usafi kutoka kampuni binafsi katika wizara hiyo, anasema kuwa Elizabeth maarufu zaidi kwa jina la Lulu amekuwa akifika wizarani hapo saa 12 asubuhi na huondoka kati ya saa 4:00 mpaka 4:30 asubuhi.

“Mfano jana (Jumanne) aliondoka saa nne na nusu, leo (Jumatano) kaondoka kama ulivyomuona mwenyewe (saa 4:15 asubuhi).
Amesema kuwa Lulu huletwa na gari binafsi saa 12 asubuhi na tangu aanze kazi za kufagia na kudeki pamoja na usafi mwingine kwa ujumla amekuwa akifanya kazi hizo kwenye ghorofa ya nne ya wizara hiyo.

Lulu ambaye alihukumiwa miaka miwili jela kwa kupatikana na hatia ya kumuua bila kukusudia mpenzi wake Steven Kanumba amebadilishiwa adhabu na tangu Jumatatu anatumikia kifungo cha nje.
Gari lililombeba msanii wa filamu nchini Elizabeth Michael likiondoka eneo zilipo ofisi za Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Posta Mpya jijini Dar es Salaam leo. Picha na Anthony Siame
Chanzo- Mwananchi
Usikubali kupitwa na habari..Pakua App ya Malunde1 blog HAPA Ili tuwe tunakutumia habari moja kwa moja Kwenye Simu yako
Loading...
logoblog

Kama Una Habari,Picha,Video,Tangazo n.k Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 757 478 553 ,0625 918 527

Malunde 1 blog Ipo PlayStore....Pakua App yetu mpya HAPA Upate Habari Mpya Moja Kwa Moja Kwenye Simu yako..Utasoma habari hata kama hauna MB..Bofya Hapa
https://play.google.com/store/apps/details?id=com.malunde.blog
Previous
« Prev Post