BABA AMUUA MWANAYE KISHA KUMZIKA KISA KAJISAIDIA KILA MAHALI NDANI

Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza linamshikilia mwanaume mmoja kwa tuhuma za mauaji ya mtoto wake wilayani Ukerewe mwenye miaka miwili baada ya kumchapa fimbo sehemu mbalimbali za mwili kutokana na kujisaidia kinyesi kwenye nyumba hali iliyopelekea kupoteza maisha.


Hayo yamebainishwa na Kamanda wa Polisi Mkoani Mwanza Naibu Kamishina wa Polisi Ahmed Msangi wakati alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari na kumtaja mtuhumiwa huyo kuwa ni Buyanza Magayane (39) ambapo baada ya kufanya tukio hilo alimzika mtoto huyo aliyefahamika kwa jina la Baraka Buyanza kwenye shamba lake lililopo nyuma ya nyumba yake, ambapo kitendo hicho ni kosa kisheria.

Aidha, Kamanda Msangi amesema inadaiwa mtuhumiwa huyo alikuwa ametengana na mkewe yaani mama wa marehemu kwa muda mrefu, hivyo marehemu alikuwa akiishi na baba yake mzazi anayetuhumiwa kusababisha kifo chake pamoja na mama yake wa kambo.

Inasemekana Mei 23, 2018 mtuhumiwa alikuwa ametoka kwenye shughuli zake za kila siku ndipo aliporudi nyumbani, alimkuta marehemu akiwa amejisaidia kinyesi katika sehemu tofauti tofauti za nyumba yake ndipo alipomchukua kisha kumchapa kwa fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake na kumfungia ndani ya chumba peke yake baada ya muda alipokwenda kumuangalia alimkuta mtoto huyo ameshafariki.

Mbali na hilo, Kamanda Msangi amesema mwili wa marehemu tayari umeshafukuliwa na umeenda kuhifadhiwa katika hospitali ya Wilaya ya Ukerewe kwa ajili ya uchunguzi na pindi utakapomalizika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani ili hatua stahiki za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yake.

Kwa upande mwingine, Kamanda Msangi ametoa wito kwa walezi na wazazi kuacha tabia ya kutoa adhabu za vipigo mara kwa mara kwa watoto pindi wanapokosea bali wawaelekeze kwa hekima na busara.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527