TAJIRI WA MABASI YA HBS NA SABENA ALIYEJIPIGA RISASI MDOMONI AZIKWA SIKONGE


Mwili wa mmiliki wa kampuni mbili za mabasi za HBS Express na Sabena, Sultan Ahmed maarufu kama Chapa, aliyejiua kwa kujipiga risasi mdomoni iliyotokea kisogoni  umezikwa jana jioni Sikonge mkoani Tabora.


Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora, Kamishna Msaidizi Mwandamizi Wilbrod Mutafungwa alisema tukio hilo la kujiua lilitokea jana saa 2:30 asubuhi nyumbani kwa marehemu na kwamba chanzo cha kujiua kwake huko hakijafahamika.

"Bado tunachunguza tukio hili, amejipiga risasi mdomoni, tunachunguza chanzo cha tukio hili," alisema Kamanda Mutafungwa.

Kamanda Mutafungwa alisema marehemu Chapa pia alikuwa akimiliki kituo cha mafuta ya petroli wilayani Sikonge.

Chapa anakuwa mfanyabiashara wa pili nchini kujiua kwa kujipiga risasi katika kipindi cha mwaka mmoja baada ya Festo Msalia, muuza vinywaji kwa bei ya jumla mkoani Dodoma, kujilipua Machi mwaka jana.

Msalia alijiua kwa kujipiga risasi kichwani baada ya kukamatwa na shehena kubwa ya viroba.

Aliyekuwa Kamanda wa polisi mkoani humo wakati huo, Lazaro Mambosasa alisema marehemu aliondoka nyumbani kwake kwa kutumia gari aina ya Toyota Prado na kwenda kujipiga risasi katika eneo la Veyula, nje kidogo ya mji wa Dodoma.

Mfanyabiashara hiyo alikamatwa na shehena ya viroba Machi 3, mwaka jana.
Theme images by rion819. Powered by Blogger.