HUYU NDIYO MKURUGENZI MPYA WA VODACOM TANZANIA

Mkurugenzi mtendaji wa Vodacom, Ian Ferrao ametangaza kuachia mikoba ya kuiongoza kampuni hiyo baada ya mkataba wake kufika tamani.


Kutokana na hilo, Ferrao atakabidhi majukumu kwa mrithi wake, Sylvia Mulinge kuanzia Juni Mosi na kuhitimisha miaka mitatu ya kuiongoza kampuni hiyo inayoongoza kwa idadi kubwa ya wateja nchini.


Taarifa iliyotolewa na mwenyekiti wa bodi ya Vodacom, Ali Mufuruki inaeleza makabidhiano ya ofisi kati ya Ferrao na Sylivia yatafantika kwa miezi mitatu na kukamilika Agosti 31.


Mufuruki alimpongeza Ferrao kwa mchango mkubwa alioutoa katika kipindi alichoiongoza kampuni hiyo pekee iliyofanikiwa kujiorodhesha Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE) licha ya Serikali kuzitaka kampuni zote za mawasilinao kufanya hivyo.


Nafasi ya Ferrao itachukuliwa na anayetokea kampuni ya Safaricom ya Kenya ambako kwa sasa anafanya kazi kama mkurugenzi wa Huduma kwa wateja aliyojiunga nayo tangu mwaka 2006.


Akizungumzia kuondoka kwa Ferao jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Bodi ya Vodacom, Ali Mufuruki alimpongeza kwa kuiendesha kampuni hiyo kwa mafanikio tangu alipojiunga nayo mwaka 2015.


“Bodi inamshukuru Ian kwa uongozi wake makini. Ameivusha kampuni katika hatua muhimu, akiiacha na jina kubwa Tanzania. Ian ni rasilimali muhimu kwa Vodacom. Miaka yake mitatu ilikuwa endelevu iliyojaa mikakati na maoni yaliyoibadilisha Vodacom kufanya biashara kisasa. Anaiacha timu madhubuti iliyojizatiti kuleta mafanikio,” alisema Mufuruki.


Kabla ya kujiunga na Vodacom Tanzania, Ferrao alikuwa mkurugenzi mtendaji wa Vodacom nchini Lesotho. 


“Ilikuwa ni nafasi adhimu kuiongoza Vodacom Tanzania katika kipindi cha mabadiliko na ukuaji. Najisikia fahari kufanya kazi Tanzania na kusaidia kuipeleka katika ulimwengu wa kidigiti na mabadiliko ya teknolojia,” alisema.


Sylvia, aliyekuwa mkurugenzi wa huduma kwa wateja wa kampuni kubwa zaidi ya mawasiliano nchini Kenya, Safaricom aliyojiunga nayo tangu mwaka 2006.


Kwa majukumu haya mapya, Sylvia atalazimika kuendeleza mafanikio aliyoyapata Ferrao kwenye ukurugenzi wake.


Licha ya kufanikiwa kuorodhesha asilimia 25 ya hisa zake DSE zenye thamani ya Sh476 bilioni na kuwavuta zaidi ya wawekezaji 40,000 wa ndani, tayari kampuni hiyo imelipa gawio la Sh28.5 bilioni.


“Sera ya gawio inataka walau asilimia 50 ya faida iliyopatikana itolewe kwa wanahisa lakini Vodacom imelipa asilimia 60,” inasema taarifa hiyo.


Mwenyekiti wa bodi alimtakia kila la heri Ferrao na kumkaribisha mkurugenzi mpya atakayeiongoza Vodacom kuwahudumia Watanzania kwa kuanzia Juni Mosi.


“Tunamtakia heri Ferrao na familia yake maisha mema. Naomba kumkaribisha mtendaji mkuu mpya ambaye nina uhakika atafanya kazi na timu ya Vodacom na tutafurahia mafanikio siku zijazo,” alisema Mufuruki.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527