Thursday, April 19, 2018

BABA MTAKATIFU AMTEUA PADRE BEATUS URASSA KUWA ASKOFU WA JIMBO LA SUMBAWANGA…HII HAPA HISTORIA YAKE

  Malunde       Thursday, April 19, 2018
Mheshimiwa Padre Beatus Christian Urassa wa Shirika la Kazi ya Roho Mtakatifu (ALCP / OSS) aliyeteuliwa kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Sumbawanga 

Baba Mtakatifu Francisko amekubali na kuridhia ombi lililowasilishwa kwake na Askofu Damian Kyaruzi wa Jimbo Katoliki Sumbawanga, Tanzania la kung’atuka kutoka madarakani. 

Wakati huo huo, Baba Mtakatifu amemteua Mheshimiwa Padre Beatus Christian Urassa wa Shirika la Kazi ya Roho Mtakatifu (ALCP / OSS) kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Sumbawanga. 

Askofu mteule Beatus Christian Urassa alizaliwa tarehe 2 Agosti 1965 huko Keni Mashati Rombo, Jimbo Katoliki la Moshi. Alipata majiundo na masomo yake ya kifalsafa kutoka Seminari kuu ya Shirika la Mitume wa Yesu, Lang’at, Jijini Nairobi nchini Kenya. 

Baadaye akajiunga na Shirika la Kazi ya Roho Mtakatifu na kupelekwa kuendelea na masomo yake ya kitaalimungu kwenye Seminari kuu ya Mtakatifu Charles Lwanga, maarufu kama Segerea, iliyoko Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania.


Baadaye alitumwa mjini Roma kuendelea na masomo ya taalimungu maisha ya kiroho kwenye Taasisi ya Kipapa ya Teresianum, iliyoko Roma na hapo akajipatia shahada ya uzamivu katika maisha ya kiroho! Tarehe 12 Julai 1997, akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. 

Tangu wakati huo, kama Padre na Mtawa, amefanya kazi mbali mbali. Kati ya mwaka 1997-1998 alikuwa ni Katibu mkuu wa Halmashauri kuu ya Shirika la Kazi ya Roho Mtakatifu (ALCP / OSS) yenye Makao makuu yake Jimbo Katoliki la Moshi.

Kati ya mwaka 1998-1999, alikuwa ni Paroko usu, Parokia ya Mwananyamala, Jimbo kuu la Dar es Salaam. Kati ya mwaka 1999-2000 akateuliwa kuwa ni mlezi katika nyumba yao ya malezi, iliyoko Jimbo Katoliki la Morogoro. 

Kati ya mwaka 2000 hadi mwaka 2003 akatumwa Roma kuendelea na masomo ya juu na huko akajipatia Shahada ya uzamivu. Kuanzia mwaka 2003 hadi mwaka 2015 amekuwa ni Padre mkuu wa Kanda Shirika la Kazi ya Roho Mtakatifu (ALCP / OSS).

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Vatican News!

(Richard Mjigwa)
Usikubali kupitwa na habari..Pakua App ya Malunde1 blog HAPA Ili tuwe tunakutumia habari moja kwa moja Kwenye Simu yako
Loading...
logoblog

Kama Una Habari,Picha,Video,Tangazo n.k Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 757 478 553 ,0625 918 527

Malunde 1 blog Ipo PlayStore....Pakua App yetu mpya HAPA Upate Habari Mpya Moja Kwa Moja Kwenye Simu yako..Utasoma habari hata kama hauna MB..Bofya Hapa
https://play.google.com/store/apps/details?id=com.malunde.blog
Previous
« Prev Post