RATIBA YA ROBO FAINALI CHAMPIONS LEAGUE

Mabingwa watarajiwa wa ligi kuu England, Manchester City imepangwa kucheza na wapinzani wao wa ligi hiyo, Liverpool kwenye hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kufuatia droo iliyochezeshwa jana mjini Zurich.


Liverpool iliyoiondoa Porto kwenye hatua ya 16 bora itakuwa nyumbani kuwakaribisha City iliyowafungasha virago Basle, kwenye mchezo wa kwanza wa hatua hiyo


Mabingwa watetezi, Real Madrid waliotinga hatua hiyo kwa kuiondoa PSG, watasafiri kwenda Turin, Italia kuumana na wanafainali wenzao wa msimu uliopita, Juventus kwenye mchezo mwingine wa hatua hiyo.


Juve imetinga robo fainali baada ya kuwanyamazisha Tottenham kwenye hatua ya 16 bora.


Juve na Real zilicheza fainali ya michuano hiyo msimu uliopita na Wahispania walichukua kombe hilo baada ya kuibuka na ushindi.


Mabingwa wa Ujerumani, Bayern Munich, watasafiri kwenda Hispania kuumana na wababe wa Manchester United, Sevilla huku vigogo wengine wa Hispania, Barcelona walioiondosha Chelsea kwenye hatua ya 16 bora watakuwa nyumbani kuwakaribisha Roma ya Italia.


Mchezo kati ya Liverpool na Man City unatarajiwa kuvuta hisia za mashabiki wengi wa soka Duniani kutokana na ushindani wa timu hizo za Uingereza.


Michezo ya mkondo wa kwanza inatazamiwa kuchezwa Aprili 3 na 4 huku michezo ya marudio ikipangwa kuchezwa Aprili 10 na 11.

Theme images by rion819. Powered by Blogger.