MKAPA ATAKA MDAHALO KUNUSURU HALI MBAYA YA ELIMU TANZANIA

MKUU wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa amesema elimu ya Tanzania ina mushkeli, hivyo unatakiwa kuitishwa mdahalo, kubaini chanzo cha tatizo na changamoto zinazokwamisha kupanda kwa elimu nchini na kuzitafutia ufumbuzi wa kuiboresha.



Mkapa ambaye alikuwa Rais wa Awamu ya Nne, alitoa kauli hiyo katika sherehe ya kumuaga Makamu wa Mkuu wa UDOM aliyemaliza muda wake, Profesa Idrisa Kikula na kumkaribisha Profesa Egid Mubofu chuoni hapo. 


Katika kuikwamua elimu nchini, Mkapa alimwagiza Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa Mubofu kuitisha mdahalo chuoni hapo, ambao hautahusisha wanataaluma wa Udom peke yao, bali na wadau wa elimu kutoka katika taasisi, jumuiya au jamii nyingine, kujadili mstakabali wa elimu nchini ambao hauendi vizuri.


Kabla ya kuitisha mdahalo huo, Mkapa alimwagiza Profesa Mubofu, kufanya hadidu za rejea kwa kusoma hotuba aliyotoa wakati akizungumza na Baraza la Chuo hicho mwaka jana, ambapo aliagiza kuwepo na juhudi za makusudi kuhakikisha mkakati unawekwa kuboresha elimu nchini. 


“Mdahalo huo wa wadau wa elimu utaweza kubainisha ni wapi elimu nchini imekwama, sababu zinazochangia na changamoto zinazochangia na wapi twende au tuirekebishe, kwani amekuwa akisikia kwamba nchi hii kielimu ni ya chini kuliko Kenya na Uganda, ila hana uhakika kuhusu hilo,” alisema.


Mkapa alisema anasoma sana magazeti, wakati mwingine hadi anamkera mkewe, lakini kupitia maoni ya watu mbalimbali zikiwemo barua za wasomaji wanalalamika kwamba elimu imeshuka, ina mushkeli, na yeye kama raia ana wajibu wa kutoa maoni yake kuhusu mustakabali wa elimu nchini. 


“Tatizo sijui ni nini, ni lugha, ratiba ya masomo, ushirikiano au ni ushirikishwaji wa waliiohitimu, wanafunzi, wakufunzi, wazazi au tatizo ni nini, mdahalo unaweza kutoa jawabu la wapi hatujaenda vizuri tujirekebishe ili tusonge mbele kielimu,” alisema.


Alitoa mfano wa matokeo ya Kidato cha Nne, mwaka jana yaliyotangazwa mwaka huu, ambapo katika shule 10 zilizofanya vizuri, shule za serikali ni mbili na zilizobaki nane ni za watu binafsi au kanisa. 


“Kwa nini si za serikali ambayo ndiyo inayosimamia elimu nchini?” Alihoji. Aliwapongeza Profesa Kikula na wenzake, Profesa Shaban Mlacha na Profesa Ludovick Kinabo, kwa kukifikisha chuo hicho kilipo kutoka kuwa pori lenye jengo moja la Chimwaga hadi kuwa mji wa majengo na kitaaluma.


Aliiomba serikali iwape tuzo kwa kazi hiyo kubwa. Akizungumza baada ya kuvua joho la uongozi chuoni hapo, alioushika tangu Februari mwaka 2007, Profesa Kikula alisema Udom ilikuwa pori na sasa ni chuo kikubwa na cha pili kwa ubora Tanzania. 


Alisema kuwa aliahidi kwa Mkapa wakati huo kwamba iwe mvua au jua, lazima chuo kisimame na ndivyo ilivyo. Wakati akimtambulisha Profesa Mubofu aliyemteua kushika nafasi ya Makamu wake, Mkapa alisema Makamu huyo mpya ni Mwalimu, Mhadhiri, Kiongozi na Mbobevu katika taaluma.


Alimtaka asiwe na shaka kusimamia chuo, kwani ataweza, lakini akaiomba serikali kumpa msaada wa fedha kuendeleza ujenzi wa majengo chuoni hapo. 


Akizungumza baada ya kuvikwa joho la Makamu Mkuu wa Chuo na kukabidhiwa zana za kazi, Profesa Mubofu aliahidi kuendeleza kazi iliyoanzwa na mtangulizi wake Profesa Kikula, akaahidi kwenda kwa viwango kwani amekwenda chuoni hapo akitoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS).


Alisema alikubali jukumu la kusimamia chuo hicho na kwamba atatumia taaluma, akili na maarifa yake yote kusimamia taaluma, utafiti na ushauri na hasa kuondoa changamoto zilizopo katika chuo hicho chenye wahadhiri na wanafunzi na watumishi 27,000 na kuhakikisha kinasonga mbele. 


Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo, Gaudentia Kabaka alimkaribisha Makamu Mkuu wa Chuo hicho, na kumhakikishia ushirikiano katika kuinua taaluma, kuongeza utafiti na ushauri katika kuhakikisha chuo hicho chenye umri wa miaka 10, kinazidi kubwa bora zaidi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527