RAIS WA FIFA AKUTANA NA WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA

SERIKALI ya Tanzania inalipongeza Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kwa jitihada na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na shirikisho hilo katika mapambano dhidi ya rushwa.


Kauli hiyo imetolewa jana (Alhamisi, Februari 22, 2018) na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika kikao chake na Rais wa FIFA Bw. Gianni Infantino kilichofanyika jijini Dae es Salaam.


“Serikali tunaunga mkono mapambano dhidi ya rushwa kwenye michezo pamoja na matumizi mabaya ya fedha na ya madaraka yanayofanywa na FIFA”.


Waziri Mkuu amesema wanaunga mkono mapambano hayo ili Taifa liweze kupata mafanikio makubwa katika mpira wa miguu ikiwa ni pamoja na kupata viongozi wenye maono ya mbali katika kuendeleza mchezo huo.


Amesema FIFA ambayo ni kitovu cha mapambano dhidi ya rushwa kwenye michezo , hivyo Tanzania inaiunga mkono kwa kuhakikisha sekta ya michezo inatumia vizuri fedha zilizopo kwa ajili ya kuendeleza michezo.


Waziri Mkuu amesema Serikali itahakikisha inasimamia matumizi sahihi ya madaraka katika sekta ya michezo nchini ili kuleta maendeleo kwenye mpira wa miguu.


Serikali inaipongeza FIFA kwa jitihada za dhati za kuendeleza mpira wa miguu duniani kwa kuwa mipango mbalimbali ya kuendeleza mpira wa miguu kwa vijana wadogo wa kike na wa kiume nchini.


“Tunatambua msukumo wa FIFA wa kuendelea mpira wa miguu duniani ikiwa ni pamoja na kuboresha viwanja vya michezo pamoja na maendeleo yote wanayoyafanya katika sekta hiyo.


Pia ameishukuru FIFA kwa kuipa Tanzania heshima ya kuwa mwenyeji wa mashindano ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 yatakayofanyika mwakani jijini Dar es Salaam na kwamba Serikali itayasimamia vizuri na inajiandaa kwa kushinda.


Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemshukuru Rais wa FIFA Bw. Infantino kwa niaba ya Rais Dkt John Magufuli kwa kuendesha mkutano mkubwa wa viongozi wa mpira wa miguu duniani Tanzania. Mkutano huo ulihusisha Marais na Makatibu Wakuu wa nchi 21.


Pia alimpongeza Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) Bw. Ahmad Ahmad kwa jitihada zake za anazozifanya katika kuendeleza mpira barani Afrika na kwamba Serikali ya Tanzania inamuunga mkono.


Rais wa FIFA Bw. Infantino ambaye ameahidi kuisaidia Tanzania kwa kuboresha miundombinu ya viwanja vya michezo aliwasili nchini leo alfajiri akiongozana na Rais wa Shirikisho la Soka Afrika Bw. Ahmad Ahmad kwa ajili ya mkutano wa FIFA uliofanyika nchini Tanzania February 22, 2018.


Bw. Infantino amewasili kwa mara ya kwanza Tanzania toka awe Rais wa FIFA na alipokelewa na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dtk. Harrison Mwakyembe na Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa Bw. Leodger Tenga na Rais wa TFF Bw. Wallace Karia.


(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, FEBRUARI 22, 2018
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akimkabidhi zawadi ya Kinyango Rais wa Shirikisho la Mpira Duniani(FIFA)Bwana Gianni Infantino katika mkutano na waandishi wa Habari uliofanyika Ofisini kwa Waziri Mkuu February 22/2017Jijini Dar es salaam Tanzania( Picha na ofisi ya waziri mkuu)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akipokea Bandera ya FIFA kutoka kwa Rais wa Shirikisho la Mpira Duniani(FIFA)Bwana Gianni Infantino katika mkutano na waandishi wa Habari uliofanyika Ofisini kwa Waziri Mkuu February 22/2017Jijini Dar es salaam Tanzania ( Picha na ofisi ya waziri mkuu)

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527