Tanzia : MZEE KINGUNGE NGOMBALE MWIRU AFARIKI DUNIA




Mwanasiasa mkongwe nchini Tanzania Mzee Kingunge Ngombale Mwiru amefariki dunia leo alfajiri Ijumaa Februari 2,2018 wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya taifa ya Muhimbili jijini Dar es salaam.

Mmoja wa wanafamilia ya Kingunge,Idd Janguo ameiambia Malunde1 blog kuwa mzee Kingunge amefariki dunia leo majira ya saa 10 alfajiri akieleza kuwa hali ya mzee ilibadilika tangu juzi.

Mzee Kingunge alikuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili baada ya kushambuliwa na mbwa nyumbani kwake Jijini Dar es Salaam takriban mwezi mmoja uliopita.

Mke wa Kingunge Peras Ngombalemwiru alifariki dunia mwanzoni mwa mwezi January kutokana na ugonjwa wa kupooza kipindi ambacho Mzee Kingunge alikuwa tayari anapatiwa matibabu ya majeraha hayo.

Mzee Kingunge alikuwa kiongozi mwandamizi nchini Tanzania katika serikali za awamu nne zilizopita naamewahi kushika nyadhifa mbalimbali katika serikali zikiwemo ukuu wa mikoa ya Tanga na Singida, Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi na Waziri katika wizara mbalimbali. 

Ndugu Kingunge Ngombale Mwiru atakumbukwa kwa kulitumikia taifa la Tanzania kwa uadilifu mkuu na uzalendo uliotukuka unaofaa kuigwa na vizazi vya sasa na vijavyo. 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527