ATUPWA JELA KWA KUJIFANYA MWANDISHI WA HABARI WA TBC


Mahakama ya wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa imemhukumu Michael Paul(32) mkazi wa Mazwi mjini Sumbawanga kutumikia kifungo cha miezi sita jela kwa kosa la kujifanya ni mwandishi wa habari ambaye anafanya kazi katika shirika la utangazaji la taifa(TBC) mkoani humo.

Akisoma hukumu hiyo leo hakimu wa mahakama hiyo Ramadhani Rugemalila alisema kuwa kutokana na mtuhumiwa kukiri kosa anahukumiwa kwenda jela ili iwefundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hiyo.

Awali mahakamani hapo mwendesha mashtaka wa polisi Hamimu Gwelo aliiambia mahakama kuwa mnamo siku ya Januari 22 mtuhumiwa alifika katika kikao kilichokuwa kikiendelea katika wilaya ya Nkasi na kujitambulisha kuwa yeye ni mfanyakazi wa TBC wakati akijua wazi kuwa anadanganya.

Baada ya utambulisho huo wajumbe wa kikao hicho walimtilia shaka na kisha kumuomba mkuu wa polisi wa wilaya hiyo amuhoji kwa kuwa wanamfahamu mwakilishi wa TBC mkoani humo.

Mkuu wa polisi huyo alifika na kumkamata mtuhumiwa na kumfikisha kituo cha polisi na kisha kuwasiliana na mwakilishi wa TBC mkoani Rukwa Nswima Ernest ambapo alikana kumfahamu wala kufahamu taarifa zake.

Aliendelea kuiambia mahakama kuwa baada ya mtuhumiwa kubanwa na jeshi la polisi alikiri kuwa alifanya hivyo ili ajipatie kipato kutokana na ugumu wa maisha unaomkabili.

Baada ya Paul kufikishwa mahakamani alikiri kutenda kosa hilo na kumuomba mahakama imsamehe kwani hatarudia tena kutenda kosa hilo, utetezi uliopingwa na mwendesha mashtaka wa polisi.

Ndipo mahakama hiyo ilimuhukumu kwenda jela miezi sita ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama yake.

Na Walter Mguluchuma - Malunde1 blog Nkasi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527