WAKAMATWA NA KILO 64 ZA DAWA ZA KULEVYA AINA YA HEROIN



Wakazi wawili wa Dar es Salaam wamekamatwa eneo la Kilambo mkoani Mtwara lililopo mpakani na nchi ya Msumbiji wakiwa na pakiti zenye uzito wa kilo 64 za dawa za kulevya aina ya heroin.


Akizungumza na Mwananchi jana, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Rogers Sianga alisema watuhumiwa walikamatwa Desemba 7 wakiwa na dawa hizo zikitokea mkoani Pemba nchini Msumbiji kuingizwa Tanzania.


Sianga alisema pakiti hizo zilifichwa kwenye gari na kila moja ilifungwa kwa ujazo wa kilo moja.


Alisema watuhumiwa walipokamatwa walipelekwa kwa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa ajili ya ukaguzi wa kina.


Sianga alisema utaratibu wa kisheria unafanyika ili kuwafikisha mahakamani.


Kwa mujibu wa marekebisho ya sheria ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya, mtu akikamatwa anasafirisha dawa hizo zaidi ya gramu 20 hapewi dhamana na adhabu yake ni kifungo cha maisha iwapo atatiwa hatiani.


Sianga alisema DCEA imewadhibiti wafanyabiashara wa dawa za kulevya ambao sasa wanaitumia Msumbiji kupitishia mizigo na baadaye kuiingiza nchini.


Alisema wana taarifa kuwa wafanyabiashara haramu wa dawa za kulevya wamekimbilia nchi za jirani na wataendelea kuwafuatilia kuhakikisha haziingii nchini.


Kamishna huyo alisema juzi waliteketeza ekari nne za bangi eneo la Arumeru Magharibi mkoani Arusha.


Alisema mamlaka inaendelea kuwatafuta watuhumiwa wanaohusika na mashamba hayo.


Kamishna wa Sheria wa DCEA, Edwin Kakolaki alisema kwa mujibu wa kifungu cha 15(1)(a) cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya namba 5 ya mwaka 2015 kama ilivyofanyiwa marekebisho watuhumiwa hawatapata dhamana.


Alisema iwapo watatiwa hatiani na Mahakama, adhabu ni kifungo cha maisha na mali zao ikiwemo gari waliokuwa wakilitumia kusafirishia dawa za kulevya zitataifishwa.


Kakolaki alisema washtakiwa wa bangi na mirungi kwa mujibu wa kifungu cha 11(1) (b) cha sheria hiyo wakipatikana na hatia adhabu ni kifungo cha miaka 30 jela na huwa hakuna faini au dhamana.


Februari 10, Rais John Magufuli alianza kuisuka Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa kumteua Sianga.

Na Pamela Chilongola, Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527