Picha : AGPAHI YAMWAGIWA SIFA UTEKELEZAJI WA MRADI WA BORESHA KWA WATU WANAOISHI NA VVU SIMIYU



Meneja wa Shirika la AGPAHI kanda ya ziwa, Dk. Nkingwa Mabelele akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za shirika hilo katika kikao cha ushauri cha mkoa wa Simiyu (RCC) kilichofanyika katika ukumbi wa KKKT Mjini Bariadi Desemba 5,2017. Picha zote na Derick Milton - Simiyu News blog
Dk. Nkingwa Mabelele, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Shughuli za shirika la AGPAHI ikiwa pamoja na Mradi wa Boresha, ambao unawahudumia watu wanaoishi na maambukizi ya VVU mkoa wa Simiyu.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi mkoa wa Simiyu Robert Rweyo akichangia taarifa ya shirika la AGPAHI katika kikao cha ushauri cha mkoa (RCC) ambapo alipongeza mradi wa Boresha huku akiomba halmashauri yake kupatiwa gari kama halmashauri zingine zilivyopatiwa.
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Antony Mtaka, akiongea na wajumbe wa kikao cha ushauri cha Mkoa (RCC).
Wajumbe wa kikao cha Ushauri mkoa wa Simiyu (RCC) wakiendelea na kikao.
Mbunge wa Jimbo la Itilima, Njalu Silanga akichangia taarifa iliyowasilishwa na Dk Nkingwa Mabelele, wakati wa kikao cha ushauri cha mkoa (RCC) ,ambapo alisema kuwa shirika hilo limefanikisha kufikika kwa haraka huduma za afya kwa wahusika baada ya kutolewa gari katika idara ya afya, na watu wanaoishi na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi wamekuwa wakipata huduma kwa wakati na kutatuliwa changamoto zao.
Wajumbe wakiendelea na kikao.

Wajumbe wakiendelea na kikao.
Makamu Mwenyekiti wa halmashauri Wilaya ya Busega Mikness Mahela, akichangia taarifa iliyowasilishwa na Dk. Nkingwa Mabelele.
Dk. Nkingwa Mabelele, alieleza kuwa kwa sasa shirika la agphai linatekeleza miradi wa Boresha katika mikoa sita ambayo ni Geita, Mara, Shinyanga, Mwanza, Tanga na Simiyu.
Wajumbe wa Kikao cha Ushauri Mkoa, wakifuatilia taarifa ya Shirika la AGPAHI kwa ukaribu.

 ****
Uongozi wa mkoa wa Simiyu, Madiwani, pamoja na wabunge wamelipongeza Shirika la Kitanzania lisilo la kiserikali la Ariel Glaser Pediatric Aids Healthcare Initiative (AGPAHI) linalojihusisha na mapambano dhidi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) na UKIMWI katika kutekeleza mradi wake wa Boresha mkoani Simiyu.

Pongezi hilo zimetolewa na viongozi hao katika kikao cha ushauri cha mkoa kilichofanyika Desemba 5,2017 katika ukumbi wa KKKT Mjini Bariadi, ambapo walisema utekelezaji wa mradi huo kwa watu wanaoishi na maambukizi ya VVU imesaidia mkoa wa Simiyu kupunguza maambukizi mapya ya VVU.

Akiongea kwa niaba ya wabunge, mbunge wa Jimbo la Itilima Mhe. Njalu Silanga mara baada ya Meneja wa Shirika la AGPAHI kanda ya Ziwa, Dk. Nkingwa Mabelele kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za shirika.

Alisema shirika hilo limerahisisha usafiri kwa wasimamizi wa shughuli za UKIMWI wilayani hivyo kufanikisha utoaji wa huduma bora za afya kwa watu wanaoishi na VVU , baada ya kutolewa gari katika idara ya Afya, ambapo wagonjwa wamekuwa wakipata huduma kwa wakati na kutatuliwa changamoto zao.

Kwa upande wake ,mwenyekiti wa Halmashauri Mji wa Bariadi, Robert Rweyo pamoja na Makamu Mwenyekiti wa halmashauri Wilaya ya Busega, Mikness Mahela walipongeza kazi za shirika la AGPAHI hasa katika kuwahudumia watu wanaoishi na VVU. 

“Tumekuwa tukiona kazi nzuri za AGPAHI, tunalipongeza sana shirika hili kwani ni moja kati ya taasisi zisizo za kiserikali ambazo zinafanya vizuri kwenye mkoa wetu hasa kuwahudumia wananchi ambao wanaishi na VVU ” ,alisema Mahela.

Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka alisema amekuwa akifuatilia kazi za shirika la AGPAHI kwa ukaribu na alilipongeza shirika kwa kutekeleza mradi wa Boresha vizuri huku akiliomba kusaidia mkoa katika kutoa elimu zaidi ya uzazi wa mpango.

“Mkoani kwetu tuna tatizo kubwa la wananchi wake kutopenda kutumia njia ya uzazi wa mpango, tunawaomba kama mnaona inafaa kusaidia katika kutoa elimu kwa wananchi wetu juu ya umuhimu wa elimu ya uzazi wa mpango” ,alisema Mtaka.

Awali akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Shirika hilo ndani ya mkoa wa Simiyu, Meneja wa Shirika hilo kanda ya Ziwa, Dk. Nkingwa Mabelele alisema katika mradi huo wamewapima jumla ya wananchi 197,649 sawa na asilimia 151% ya lengo la mradi kwa kipindi cha Oktoba 2016 hadi Septemba 2017, na kati ya waliopimwa 6,783 walibainika kuwa na VVU. 

Alisema waliwapima wananchi hao kwa mkoa mzima ambapo waliobainika kuwa na VVU walianzishiwa huduma za matibabu (dawa za ARVs) mara moja.

Aidha Dk. Mabelele alieleza kuwa katika mikoa wanayoendesha mradi wa BORESHA ni Geita, Mara, Simiyu, Shinyanga, Mwanza, na Tanga wamefanikiwa kuwapima watu 1,472,286 ikiwa ni asilimia 146% ambapo walilenga kuwafikia wananchi 1, 018, 591. 

Alisema kati ya wananchi hao waliopimwa afya zao, 63416 walibainika kuishi na VVU, zoezi ambalo lilifanyika katika kipindi cha Mwezi Oktoba 2016 hadi June 2017.

AGPAHI ni shirika la kitanzania lisilo la kiserikali linajishughulisha na programu za kutokomeza maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) na Ukimwi, kuzuia maambukizi mapya ya VVU kwa watoto, matunzo na huduma za matibabu kwa watu wanaoishi na VVU nchini Tanzania.

Kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Wahisani, shirika limekuwa likiunga mkono utoaji wa huduma za VVU katika mifumo iliyopo.

AGPAHI imejikita katika kutoa msaada wa huduma zenye ubora wa hali ya juu na kuhakikisha jitihada za kufikia lengo la pamoja la kutokomeza Maambukizi ya VVU kwa watoto linafikiwa.Shirika linafanyakazi katika mikoa ya Tanga, Mwanza, Geita, Mara, Shinyanga, Simiyu na mkoa wa Manyara wilayani Simanjiro kwenye machimbo ya Mererani.

Na Derick Milton - Simiyu News blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527