MAMIA YA WANAWAKE DAR WATAPELIWA MAPENZI , MAMILIONI YA FEDHA NA WAZUNGU WA FACEBOOK | MALUNDE 1 BLOG

Wednesday, December 27, 2017

MAMIA YA WANAWAKE DAR WATAPELIWA MAPENZI , MAMILIONI YA FEDHA NA WAZUNGU WA FACEBOOK

  Malunde       Wednesday, December 27, 2017

Ahadi ya zawadi kubwa ikiwemo fedha na kutekwa kimapenzi kwa njia ya mtandao, kumewaliza mamia ya wanawake wa Jiji la Dar es Salaam.

Watu hao wameingia katika wimbi la kutapeliwa mamilioni ya fedha na ‘wapenzi’ wao hao, wanaojitambulisha kuwa ni raia wa mataifa ya Ulaya na Marekani

. Uchunguzi uliofanywa na gazeti la Habarileo kwa muda wa zaidi ya mwezi mmoja sasa, kwa kuzungumza na wanawake watano, umebaini kuwa mamia ya wanawake wamelizwa kwa kutapeliwa fedha na wazungu hao, wanaofahamiana nao katika mtandao wa Facebook, huku wakiponzwa na ahadi za mapenzi na zawadi mbalimbali, ikiwemo fedha.

Matapeli hao huwafuatilia wanawake kwenye mitandao ya kijamii hasa Facebook, ambapo huanza kwa kuwaomba urafiki na kisha kupeana namba za simu na ndipo mwanzo wa mawasiliano ya kina yanapoanza.

Gazeti la Habarileo limebaini kuwa mtandao huo wa matapeli, hutumia namba mbalimbali za simu katika kuwatapeli wanawake zikiwemo namba za Ulaya, Marekani na za nchi jirani katika kuwasiliana na walengwa wao kwa njia za ujumbe mfupi wa maneno, huku gia yao ya kwanza ikiwa ni kuomba uhusiano wa kimapenzi.

Vyanzo vya kuaminika vilivyozungumza na gazeti hili, wakiwemo baadhi ya wanawake ambao tayari wametapeliwa fedha nyingi, vilisema wazungu hao baada ya kuomba urafiki na kukubaliwa, huendeleza mawasiliano kwa njia ya ujumbe mfupi au mazungumzo na wahusika kwa kasi ili kuwaaminisha juu ya uhusiano wao.

Wakati wote wa mawasiliano, wazungu hao hutoa ahadi mbalimbali kwa wanawake huku wakiahidi kuwatumia zawadi mbalimbali kama simu za gharama kubwa, kompyuta mpakato, Ipad na dola za Marekani kati ya 20,000 na 30,000, huku lengo lao mahususi ikiwa ni kuwatapeli.

Mmoja wa waathirika wa matukio hayo, mkazi wa Tabata jijini Dar es Salaam aliyeomba jina lake kuhifadhiwa, akieleza namna alivyotapeliwa alisema; “Huyu mzungu kwanza alionesha interest (nia) ya mapenzi kwangu.

Mwanamke huyo ambaye alisema aliishia kutapeliwa Sh 550,000, alisema mzungu huyo aliyekuwa anawasiliana naye, alijitambulisha kwa jina la Don Collin, raia wa Uingereza. “Kwanza aliniomba urafiki Facebook, kabla ya kumkubalia nilimfuatilia kuona taarifa zake na nikaona kuna baadhi ya marafiki zangu Facebook ni marafiki zake kwa hiyo nikaondoa shaka dhidi yake.

“Niliamua kumkubalia urafiki kwani alionekana kuwa ni mtu wa kuaminika kwani mwanzoni kabisa wakati wa mawasiliano yetu alijitambulisha kuwa ni Mwanajeshi anayefanya kazi kwenye meli ya Uingereza.

Alisema waliendelea na urafiki wao kwa kutumia simu na Facebook kwa muda mrefu, kabla ya kuanza kumtongoza. Alisema hatua hiyo ilizidi kumuongezea uaminifu zaidi na ni wakati huo mzungu huyo alimpa taarifa alizoona ni njema kuwa anataka kumtumia zawadi ya viatu, pochi, simu na fedha Dola za Marekani 25,000 (zaidi ya Sh milioni 50).

“Sauti yake ilikuwa ni ile ya mzungu kweli. Alikuwa akijitanabaisha kuwa ni mtu mwenye uwezo mkubwa wa kifedha na alisisitiza kuwa lengo la kunitumia zawadi na fedha hizo ni kuimarisha uhusiano wa mapenzi kwangu ambao alikuwa tayari ameuonesha,” alisema.

Alisema ilifika siku ambapo Mzungu huyo alimpigia simu na kumueleza kuwa rafiki yake ambaye ni Mwanadiplomasia, alikuwa na safari ya kuja Dar es Salaam na alisema ni nafasi nzuri ya kunitumia zawadi zangu alizosema kuwa angezifunga kwenye sanduku maalumu na kunitumia namba ya siri ya kulifungua.

“Nilikaa nikisubiri hadi siku nilipopigiwa simu na mtu kwa namba ya hapa nchini akijitambulisha kuwa ni mfanyakazi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) akinitaarifu kuwa kuna mtu amekamatwa uwanjani hapo akiwa na mzigo wangu.

“Aliniambia kuwa walimkamata kwa vile alikuwa na mzigo ambao ulikuwa haujalipiwa kodi na hivyo alisisitiza kuwa watamuachia endapo ningetuma Sh 550,000. Kwanza nilifanya utafiti kwa kumtumia mdogo wangu kujua kama KIA kuna mtu mwenye jina hilo na nikathibitishiwa kuwa yupo.

“Kwa vile akili yangu ilikuwa juu ya zile Dola za Marekani 25,000 niliona ni bora nitume fedha hiyo. Ingawa nilitia shaka kuwa masuala ya kodi hushughulikiwa na Mamlaka ya Mapato (TRA) lakini nilipochunguza namba ya usajili ya simu na jina nililopewa na ofisa wa KIA niliona yanafanana, hivyo nilituma fedha hizo,” alisema.

Alisema hata hivyo, muda mfupi baadaye, mtu huyo wa KIA alipiga simu na kumweleza kuwa wakati wanaukagua mzigo huo kwa mashine (scanner) ili kuruhusu kutoka, wamebaini kuwa kuna kiasi kikubwa cha dola zinazosafirishwa isivyo halali.

Alisema wakati wote simu hiyo ilikuwa inabadilishwa kutoka kwa ofisa wa KIA na Mwanadiplomasia huyo ili kuzungumza naye. “Walisema wamegundua kupitia Scanner kuwa ni kiasi kikubwa cha Dola ila wameshindwa kujua ni kiasi gani kwa vile sanduku hilo limefungwa kwa namba maalumu.

“Waliniambia kwa vile kitendo hicho ni kinyume cha sheria kutokana na sheria kuruhusu mtu kusafirisha dola za Marekani zisizozidi 10,000, aliyenitumia, aliyekutwa nazo na mimi, tumefanya kosa la jinai na tunatakiwa kukamatwa.

“Hata hivyo, walianza kunishawishi kutoa fedha nyingine ili wauachie mzigo huo, lakini pia sisi pia tuwe huru. Niliomba kuzungumza na yule mwanadiplomasia nikamwambia atoe hizo fedha ili mimi nimrudishie baadaye, akasema hakuwa na fedha taslimu.

“Nikawasiliana na Collins kumwambia akasisitiza nitume fedha ili kumaliza suala hilo, akisema fedha zilizopo kwenye sanduku ni nyingi zaidi hivyo nisikubali kuruhusu suala hilo kuwa kubwa,” alisema mwanamke huyo.

Hata hivyo, alisema wakati huo alianza kupata shaka kuwa huenda kuna utapeli unafanyika; na ndipo alipoanza kufanya uchunguzi wa kina wa jina la ofisa wa KIA na namba ya simu aliyotumia kutuma fedha na kubaini kuwa jina lilikuwa limetofautiana kwa herufi moja ya mwanzo.

“Hapo ndipo nilipobaini kuwa nimetapeliwa na nikasitisha kutuma fedha nyingine wakati huo nikihangaika huku na kule kuanzia Tigo ili kuomba fedha hizo kuzuiwa bila kupata msaada wowote.

Hata hivyo, kupitia wanawake 10 niliozungumza nao, gazeti hili limebaini kuwa wapo wanawake ambao baada ya kutakiwa kutuma fedha za awali kwa kisingizio cha kulipa kodi waliendelea kubanwa ili kulipa fedha zaidi kati ya Sh milioni tano na 10, wakitishiwa kuwa bila kufanya hivyo watakamatwa na kufikishwa mahakamani.

Kwa vile katika uchunguzi wake, gazeti hili lilibaini kuwepo kwa wanawake wengine jijini Dar es Salaam (majina tunayo), ambao wametapeliwa kwa mtindo huo, lilifanya juhudi za kuwasiliana na maofisa wa Kitengo cha Kukabiliana na Uhalifu kwa njia za Kimtandao cha Makao Makuu ya Jeshi la Polisi na kuzungumza na ASP, Mwangasa Joshua ambaye ni Msaidizi wa Mkuu wa Kitengo hicho.

Katika ufafanuzi wake, Mwangasa alisema kuwa kumekuwa na kesi za aina hiyo na nyinginezo nyingi zikitokea mara kwa mara na kuwa matapeli hao hubadilisha mbinu kila kukicha.

Alisema, kikosi hicho kimefanikisha kuwakamata matapeli wa aina hiyo na kesi zimefikishwa mahakamani na zinaendelea kungojea hukumu na kusisitiza kuwa kikubwa ambacho kinatakiwa kufuatwa na wananchi ni kuacha tabia ya kutuma fedha kwa watu wasiowajua.

“Najua tuna wajibu wa kukabiliana na wizi huu wa mtandaoni ambao umewaliza wanawake wengi nchini lakini, wahusika wenyewe nao wasikilize ushauri tunaoutoa kila siku wa kuwa wawe makini katika kutuma fedha mitandaoni hata kama wanatuma kwa wapenzi wao ni lazima wajiridhishe,” alisema Mwangasa.

Msemaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA), Semu Mwakyanjala aliwataka wananchi kuwa makini dhidi ya wahalifu hao kwa njia za mitandao hasa kwa kutowapatia mwanya wa kuwaibia.

IMEANDIKWA NA EVANCE NG'INGO - HABARILEO
Usikubali kupitwa na habari..Pakua App ya Malunde1 blog HAPA Ili tuwe tunakutumia habari moja kwa moja Kwenye Simu yako
logoblog

Kama Una Habari,Picha,Video,Tangazo n.k Wasiliana Nasi Simu/WhatsApp +255 757 478 553 ,0625 918 527

Malunde 1 blog Ipo PlayStore....Pakua App yetu mpya HAPA Upate Habari Mpya Moja Kwa Moja Kwenye Simu yako..Utasoma habari hata kama hauna MB..Bofya Hapa
https://play.google.com/store/apps/details?id=com.malunde.blog
Previous
« Prev Post