HOJA YA MIAKA 7 YA URAIS YAUBUKIA ZANZIBAR...BALOZI ATETEA

Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd amesema ushauri wa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kutaka kuongezwa muda wa urais kutoka miaka mitano mpaka miaka saba ni suala zuri na linazungumzika bila matatizo.


Balozi Idd aliyasema hayo jana wakati akifunga mkutano wa nane wa Baraza la Tisa la Wawakilishi lililochukua muda wa wiki moja mjini hapa.


Awali baadhi ya wajumbe wa baraza hilo wakichangia Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Tume ya Uchaguzi ya mwaka 1984 na kuweka sheria ya mwaka 2017, walisema kuwa ili Zanzibar iepukane na matumizi hasa kipindi cha uchaguzi hakuna budi kuongezwa kwa muda wa utumishi wa urais.


Mmoja wa wawakilishi hao wa Jimbo la Shaurimoyo, Hamza Hassan Juma amesema kuwa ili kumpa Rais wakati mzuri wa kutumikia wananchi ipasavyo hakuna budi muda wake kuongezwa zaidi ili lengo la kufikisha maendeleo kwa wananchi liweze kufanikiwa.


Alisema kwa kuwa muda wa miaka mitano ya uongozi wa rais madarakani linaonekana kupoteza fedha nyingi za wananchi kwa kufanya uchaguzi kila baada ya miaka mitano, ni vyema uongozi ukaliona hilo na kulifanyia kazi.


Alisema kwa mujibu wa tathmini yake ya uchaguzi mkuu mara nyingi hutumia fedha nyingi za walipakodi kiwango ambacho kinaweza hata kujenga zaidi ya shule kubwa 20 ambazo zingeisaidia jamii kuondokana na uhaba wa shule.


Alisema kuwa pamoja na katiba zote mbili ya Tanzania Bara na Zanzibar kuweka muda huo wa miaka mitano, bado kuna nafasi kubwa kwa Zanzibar kufanya marekebisho ya katiba yao ili kuongeza muda, akidai kuwa ni jambo ambalo haliwezi kuathiri hata kidogo Katiba ya Tanzania.


Juma alisema ikiamuliwa kufanyika hivyo ni wazi kuwa faida kubwa inaweza kupatikana ikiwamo Rais kupata muda mwingi wa kutumikia jamii badala ya muda wa sasa wa miaka mitatu tu ya kutumia jamii huku miaka miwili iliyosalia akishughulikia masuala ya uchaguzi.


Balozi Iddi akitolea ufafanuzi suala hilo alisema kwa kuwa jambo hilo linahusiana na pande mbili za Muungano ni vema kwa wakati huu suala hilo likaachiwa kwa viongozi husika kwa kulifanyia kazi na ikionekana linafaa ni wazi linaweza kupunguza gharama kubwa hasa kwa upande wa chaguzi za viongozi wakuu.


“Hili itakuwa si suala jipya kwetu kwani hata ndugu zetu wa Rwanda nao wameongeza muda wa uongozi, hivyo nasi tukibadili miaka badala ya mitano tukaweka saba tunaweza kufanikiwa kimaendeleo kwa hatua kubwa,” amesema Balozi Idd.


Alisema hali hiyo pia inaweza kuleta mafanikio makubwa katika chaguzi zijazo kufanyika kwa ufanisi mkubwa hasa baada ya marekebisho ya sheria ya uchaguzi yaliyofanyika.


Alisema Serikali ipo tayari na itaendelea kila mara kuwa hivyo kwa kupokea michango mbalimbali ya wawakilishi ambayo inaonekana inafaa kwa ajili ya kujenga maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla.


Hata hivyo, Balozi Iddi akifunga mkutano huo alisema kuwa Serikali imedhamiria kukabiliana na changamoto zinazowakabili wananchi wake ili kuona nao wanaishi katika hali ya matumiani.


Alisema kuwa miongoni mwa hatua zinazochukuliwa na Serikali tayari wameanza kununua meli moja ya mafuta, huku harakati za ununuzi wa meli kwa ajili ya abiria zikiendelea kutoa matumaini.


“Meli hizi kwa ufupi zinaweza kusaidia harakati za wananchi wetu hasa kwa kuwa na usafiri wa uhakika ambao utasaidia katika upatikanaji wa huduma mbalimbali,” alisema Balozi Idd.


Hatua nyingine zinazochukuliwa ni kuwa Serikali inaendelea katika ufanikishaji wa mradi wa maji safi na salama, mradi ambao unadhaminiwa na Benki ya Maendeleo Afrka kwa kushirikiana na Serikali ya Zanzibar ambao unataraji kutumia dola za Marekani 25,673.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527