HAMASA INAHITAJIKA KWA WASICHANA WANAOPENDA KUJIFUNZA TEHAMA TANZANIA

WATANZANIA  wametakiwa kuwaunga mkono na kuwahamasisha wasichana kupenda kujifunza masuala ya TEHAMA bila ya kujali uwezo wa kiuchumi wa familia wanazotokea.

Wito huo umetolewa na Jumia Food Tanzania ambao kwa kushirikiana na Apps & Girls wanaendesha kampeni inayolenga kuwakutanisha na kusherehekea kwa pamoja msimu huu wa sikukuu.

Kampeni hiyo ambayo inawataka wateja na watanzania kwa ujumla kufanya huduma ya chakula kupitia mtandao wa Jumia Food kwa kutumia nenosiri ‘JOY,’ ambapo kwa kufanya hivyo, kila huduma ambayo itafanywa kwa kutumia nenosiri hilo itasaidia msichana mmoja katika kituo cha Apps & Girls.

Akizungumzia uamuzi wa kufanya kampeni hiyo, Meneja Uhusiano na Umma wa Jumia Food Tanzania, Bw. Geofrey Kijanga amesema kuwa huu ni msimu wa sikukuu na ni muda muafaka wa kurudisha kwa jamii ambayo inaunga mkono shughuli zake na kuifanya isonge mbele zaidi.

“Tumeona ni vema kushirikiana na taasisi ya Apps & Girls kwa kutambua umuhimu wa kazi kubwa wanayoifanya na mchango wake katika kuwakomboa watoto wa kike. Tanzania kama nchi zingine zinazoendelea Afrika na duniani, mtoto wa kike ana fursa finyu za kumfanya kuonyesha uwezo wake wa kufanya masuala mbalimbali ukilinganisha na wa kiume. Hawa wenzetu wao wameona kwamba wasichana nao wanapenda na wana uwezo wa kuwa wabunifu kwenye TEHAMA lakini wanakosa namna ya kujiendeleza na sehemu za kuonyesha uwezo wao,” alisema Meneja Uhusiano wa Umma wa Jumia Food Tanzania.

“Hatuna uwezo mkubwa wa kuwapatia kila kitu kwa ajili ya kituo chao lakini tunao moyo wa kuwatia nguvu, kuihamasisha jamii na kuonyesha kwamba tunatambua jitihada zao. Tunaamini kwamba wanafanya kazi nzuri na kitu cha kipekee ambacho taasisi nyingi hazifanyi hivyo,” aliongezea na kumalizia Bw. Kijanga kwamba, “Tunawaomba watanzania watuunge mkono kwa kutumia nenosiri ‘JOY’ kila wanapofanya huduma ya chakula kupitia Jumia Food ndani ya wiki hii itakayoishia Desemba 22. Kwa kufanya hivyo watakuwa wamewasaidia wasichana wa kwenye kituo cha Apps & Girls.”

Akizungumzia malengo ya kuanzishwa kwa Apps & Girls, Bi. Carolyne Ekyariisima ambaye ndiye mwanzilishi amebainisha kuwa, “Dhumuni kubwa ni kuwapatia wasichana wa Afrika ujuzi, nyenzo, kujiamini na kuwajengea uwezo wa kiushindani ili kuwa viongozi imara na chachu ya mabadiliko kwenye jamii yao. Lakini wakati huohuo kutengeneza taasisi na kampuni endelevu zilizojikita katika kutatua changamoto mbalimbali za kijamii barani Afrika.”

“Mpaka sasa, Apps & Girls imekwishatoa mafunzo kwa wasichana takribani 1900 tangu kuanzishwa kwake na inatarajia idadi hiyo kufikia milioni moja mnamo mwaka 2025. Kwa sasa ina wasichana 45 kwenye kituo chao na tayari 20 wameanza kutekeleza miradi yao. Wasichana wanne wameshinda mashindano kitaifa nchini Tanzania na kimataifa jijini New York, Finland na Afrika ya Kusini na kuwafanya kuwa mifano ya kuigwa na hamasa katika jamii. Kwa mfano, msichana Asha, 19, alishinda shindano la New York Junior Academy Global STEM Alliance na hivi karibuni alijishindia ruzuku ya takribani dola za Kimarekani 25,000 kutoka DLI na tunzo kutoka Internet Society ya umri wa miaka chini ya 25 (25 under 25),” aliongezea.

“Tunayo mipango mingi na mikubwa ya kuitekeleza ili kuhakikisha Apps & Girls inafika mbali kama vile; kutengeneza vituo ambavyo vitakuwa ni vitovu vya mafunzo ya teknolojia kwa wasichana kwenye shule za sekondari na vyuo vikuu ambayo vitatoa mafunzo, malezi na ushauri; kuipeleka programu ya Apps & Girls nchi nzima katika shule 58, mradi ambao utakuwa chini ya Tigo-Eschools mwaka 2018; pamoja na kuipeleka nchini Uganda,” alisema na kumalizia mwanzilishi huyo kwamba, “Mbali na mafanikio na mipango tuliyonayo lakini tunakabiliwa na changamoto kadhaa kama vile, hatuna fedha za kutosha kuendesha miradi tuliyonayo, nyenzo chache kama vile kompyuta, mtandao wa intaneti na sehemu ya kujengea vituo vya mafunzo pamoja na uwezo duni wa wasichana katika kutekeleza miradi yao kwani wengi wao wanatoka kwenye familia zisizokuwa na uwezo.”

Apps & Girls iliianzishwa mnamo mwezi Julai mwaka 2013, kwa lengo la kupunguza pengo lililopo kwenye upande wa masuala ya kiteknolojia nchini Tanzania. Taasisi hii imejikita kutoa mafunzo kwenye sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa wasichana kama vile kubuni programu za kompyuta, simu na michezo, tovuti pamoja na mafunzo ya ujasiriamali kupitia vilabu vya kujifunza programu kwenye shule za sekondari mpaka ngazi ya vyuoni. Apps & Girls pia huandaa warsha, mashindano pamoja na kutoa fursa za mafunzo kwa wasichana hao kwenye makampuni na taasisi mbalimbali.

Na Jumia Food Tanzania

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527