WEZI WACHIMBA NJIA YA CHINI KWA CHINI NA KUIBA PESA KWENYE BENKI

Wezi katika mji wa Mumbai magharibi mwa India walitekeleza wizi kwenye benki moja inayomilikiwa na serikali baada ya kuchimba njia ya chini kwa chini ya urefu wa futi 25 (mita 8).

Walichimba njia hiyo kwa miezi kadhaa.

Polisi wameambia BBC kwamba pesa taslimu pamoja na vito vya thamani isiyojulikana viliibiwa.

Maafisa wanaamini kwamba wezi hao walikodisha chumba karibu na Benki ya Baroda kuwawezesha kuchimba njia hiyo.

Wanadaiwa kuendesha biashara ya kuuza mboga na matunda katika kiduka chao kuficha mipango yao.

Wezi hao walitoweka tangu Jumamosi usiku baada ya kutokea kwa wizi huo.

Haijabainika ni vipi wanaume hao walifanikiwa kuchimba njia hiyo kwa miezi kadha bila kugunduliwa.

Vyombo vya habari nchini India vimezungumza na wateja wa benki hiyo ambao vitu vyao vya thamani viliibiwa.

"Akiba yangu yote ilikuwa imewekwa kwenye sefu. Vito ambavyo tumemiliki kwa vizazi kadha, vimeibiwa," Dagdu Gavani, mmoja wa wateja aliambia Mumbai Mirror.

Wafanyakazi wa benki hiyo iliyo viungani mwa mji wa Mumbai waligundua wizi huo Jumatatu na kuwafahamisha polisi.

Polisi wameambia BBC kwamba sefu 30 kati ya 225 kwenye benki hiyo ziliporwa.

Washukiwa bado hawajatambuliwa.Benki ya Baroda humilikiwa na serikali.
Chanzo-BBC

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527