NAPE NNAUYE : CCM IKIKATAA KUAMBIWA UKWELI NDIYO MWANZO WA KUANGUKA

Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye ameonya kuwa endapo chama hicho hakitataka kuambiwa ukweli na kukosolewa, utakuwa mwanzo wa kuanguka kwake.


Nape aliyewahi kuwa katibu wa itikadi na uenezi wa chama hicho, amesema endapo CCM itaua utamaduni wa kukosoana kupitia vikao itapoteza mwelekeo.

“Hiki chama tukifika mahali tukaanza kufanyiana unafiki kwamba hatutaki kuambiana ukweli tunapokosea utakuwa ndiyo mwanzo wa kuanguka kwa CCM.”

Amesema hayo juzi nyumbani kwake eneo la Kisasa mjini Dodoma katika mazungumzo maalumu na Mwananchi.

Nape ambaye leo anatimiza miaka 40 ya kuzaliwa, ameeleza kusikitishwa na namna ya baadhi ya watu aliowaita “vijana wa CCM”, kupotosha kwa makusudi kauli na ujumbe wake anaoutuma kupitia mitandao ya Twitter na Instagram.

“Kuna ambao wanamchukia tu Nape kwa sababu wanadhani alishiriki kuzuia wagombea wao na hasa hawa vijana wafuasi wa Edward Lowassa ambao bahati mbaya alipohama hawakuhama naye,” alisema.

“Hawa nao wako wanapitia humo kusema hasira zao. Mara Nape huyu anamsema Rais. Unamuona Nape huyu anaisema Serikali. Hawa nao tuwapuuze. Wakikua wataacha.

“Wanaona Nape ni beki mzuri wa kufanyia mazoezi au ya kuonekana wapo ili tu wapewe vyeo. Bahati nzuri mimi nimekulia ndani ya CCM najua lipi zuri na lipi baya kwa CCM,” alisema.

Mbunge huyo alisema husikitika anaposoma namna kauli zake zinavyopotoshwa, huku wengine wakidai anatumia maneno makali kwa vile ameondolewa kwenye uwaziri alikokuwa waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Nape alisema, “Hakuna jambo ambalo nimelisema kwenye Twitter na Instagram ambalo halifai kusemwa. Wakati mwingine nina maneno magumu kwenye vikao. Ninaamini kwenye hayo maneno magumu ndiko ambako tutakijenga chama chetu,” alisema.

Alisema akiwa katibu wa itikadi na uenezi kuna vikao vilifanyika mpaka saa sita usiku na alikuwa mkorofi kidogo kwa sababu maneno yake wakati mwingine yalikuwa magumu.

“Namshukuru sana Kikwete (Rais mstaafu Jakaya) amenilea na amenivumilia wakati mwingine, maana sarakasi nyingine na ujana huu amenivumilia sana,” alisema.

Alisema, “Katika watu wenye moyo wa ajabu sana ni Rais Kikwete (mstaafu). Katibu mkuu wetu (Abdulrahman) Kinana naye ameni shape (nijenga) sana kunivusha kutoka ujana hadi kukomaa.

“Lakini nasema lazima CCM ijenge utamaduni wa kukosoana na kujikosoa ili tuende mbele. Tukiua huo utamaduni tutakifanya hiki chama kitapoteza mwelekeo. Tuujenge kwa nguvu kubwa.”

Akizungumzia aina ya maneno anayoyatumia kufikisha ujumbe kupitia Tweeter, Nape alisema ujumbe mzuri ni ule ambao ukiwekwa unafikirisha na unamfanya mtu kueleza namna alivyouelewa.

“Tweet nzuri ni ile ambayo ukiiweka inafikirisha. Tweet nzuri ya mtu aliyetumia akili, ya mtu msomi huweki tweet ambayo kila mtu akisoma umeandika shikamoo baba. Inatakiwa iwe ambayo mtu akisoma anafikiria na anapata hamu ya kuitafakari. Nafurahi sana kwa sababu Tweet zangu zinasumbua akili wakati mwingine wanapata majibu tofauti tofauti.

“Wengine wananitukana wengine wananituhumu. Kwenye Tweet zangu hizi kwa sehemu kubwa watu wanapotosha na wanaopotosha wamegawanyika katika makundi mawili. Kuna ambao hawamjui Nape na hao ndiyo wale wanaosema Nape toka (tangu) ametoka uwaziri ana tweet hivi lakini nimekuwa nikiwauliza kwani kabla sijawa waziri, sijawa katibu mwenezi sikuwa nasema?”

“Wanasahau mimi niliwahi kumnyoonyeshea kidole waziri mkuu wa Tanzania hadharani nikasema wewe fisadi. Leo wanasema Nape anasema maneno makali sana! Hivi kuna maneno makali zaidi ya kumnyooshea waziri mkuu wa nchi ukasema hapa kwenye mradi huu umefanya ufisadi?

“Hawajui mimi ndiye niliyesimama Songea nikasema Kikwete kuna mawaziri wako hapa ni mizigo. Hivi kuna kauli kubwa ya kufikia hapo?

“Mtakumbuka niliwahi kusimama kwenye mkutano wa hadhara lakini mtakumbuka nilikwenda Arusha nikamwambia Lazaro (Nyalandu) nenda katimize wajibu wako acha kuweka watetezi”.

Afikiria kujitoa mitandao ya kijamii
Akizungumzia mkanganyiko wa namna watu wanavyopotosha ujumbe mbalimbali, Nape alisema, “Pengine nitoke kwenye social media (mitandao ya kijamii) sababu unaona kila mara uki-post (kutuma) jambo ooh linakuwa kubwa sana.

“Tena wakati mwingine ni jambo la utani sana. Kwa mfano siku moja nimeangalia kipindi kwenye televisheni wanasema mara paap na mimi nikaweka mara paap.

“Nilipoweka mara paap, wakaanza mara paap kahama CCM mara paap kafanya hivi, unakaa unasema kwa nini wanafikiria negative (mabaya) kwa nini hawafikirii positive (mazuri)?”

“Kwa nini hawasemi mara paap ameimarisha chama... Ukiyaona haya naanza kutafakari seriously (makini) umefika wakati nisimame kidogo hii social media.”

Hata hivyo alisema anaona akifanya hivyo atawapoteza wafuasi wake zaidi ya 200,000 walioko Tweeter na maelfu walioko Instagram na ndiyo maana anajiuliza kwa nini atoke kwa sababu ya wapuuzi wachache?

Mbunge huyo wa Mtama alisema pamoja na watu kutafsiri tofauti na kupotosha maana halisi ya ujumbe wake, hajawahi kuitwa na chama chake kuhojiwa.

“CCM ni chama kikubwa sana na mimi nimekaa humu zaidi ya miaka 10 nikiwa mtumishi ukiacha miaka 20 nikiwa mwanachama. CCM ninaijua. Ninajua jambo gani baya na jambo gani zuri.


Hata Nyerere aliiokosoa CCM
Alisema si dhambi kuikosoa CCM ikiwa tu dhamira inakuwa ni kuijenga na kuiimarisha na kwamba hata Baba wa Taifa, Hayati Julius Nyerere alikuwa akiikosoa.


“Mwaka 1995 wakati mwalimu anazunguka kumnadi (Benjamin) Mkapa alikuwa anasema CCM kokoro hili limebeba watu wote kuna wengine humu nikijiuliza inakuwaje tuko chama kimoja nao. Yalikuwa maneno makali. Alienda Musoma pale akasema nyie CCM mmesimamisha mgombea wenu pale mla rushwa. Huyu mimi sitampigia kura nitampigia yule wa NCCR-Mageuzi.”


“Hivi kuna maneno makali nimeyasema kuliko haya? Mwalimu alisema maneno makali sana, lakini akasema kuna maneno ya uongo? Ni lazima tujenge utamaduni wa kukosoana ili kujenga”


Mbunge huyo alitumia mahojiano hayo kumpongeza Rais Magufuli kwa kutimiza miaka miwili madarakani, lakini akasema upo mjadala wa namna anavyotekeleza ilani ya CCM.


Nape alisema yote yaliyoingizwa katika ilani ambayo Rais Magufuli anaitekeleza kwa mafanikio, yalitokana na ziara yake yeye na Kinana iliyowachukua miezi 36 ya kukiimarisha CCM.


“Tulipokuwa tunazunguka yapo mambo mengi tuliyasema. Yale ndiyo yalikuja kuzaa ilani ya uchaguzi ya CCM (2015-2020). Yale ndio yalikuja kuzaa mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Tano.


“Sasa hapa tunapotimiza miaka miwili, ukifanya tathmini mambo mengi anayoyafanya Rais Magufuli pamoja na kumpongeza kwa kufikisha miaka miwili, ni yale ambayo tuliyaweka kwenye ilani.”


Alisema walipozunguka mikoani, wananchi walilalamikia kuhusu kuporomoka kwa nidhamu ya utumishi wa umma, wingi wa sherehe za kitaifa, mikataba mibovu ya madini na rushwa.


“Shida ya nidhamu katika utumishi wa umma ilikuwa kubwa. Tuliikuta kila mahali. Hili ni jambo moja Rais Magufuli amelisimamia vizuri,”alisema.


Aliyataja maeneo mengine ambayo alisema Rais ameyasimamia vizuri kuwa ni kudhibiti matumizi ya Serikali, kusimamia sera ya uchumi wa viwanda na kushughulikia migogoro ya ardhi.


Maeneo mengine ambayo alisema Rais amewafurahisha Watanzania ni kuondoa utitiri wa kodi kwa wakulima, kudhibiti rasilimali ya madini na kusimamia masilahi ya watumishi wa umma.


“Kwa hiyo amefanikiwa kugusa kila mahali lakini mjadala uliopo ni namna anavyoyatekeleza haya mambo. Hapa ndipo palipo na mjadala na watu wengi wanazungumza hapo.


“Hili mimi sitegemei watu wote watakubaliana. Wako wanaodhani angeenda taratibu kidogo, wapo wanaodhani akaze zaidi, wapo wanaodhani afinye zaidi na wako wanaodhani aende mdogomdogo.”


Nape alisema hakuna ubishi nchi ilikuwa katika matatizo makubwa ya rushwa na watu walitamani kupata kiongozi ambaye hataona aibu hata akimkuta rafiki yake anafanya ufisadi amshughulikie.


“Tunadhani Magufuli ameanza vizuri. Mjadala utakuja tu hivi katika utekelezaji pengine tupunguze mwendo, twende kasi zaidi, tutumie busara zaidi, tutumie upole fulani hivi. “Huu ndiyo mjadala ambao upo ambao nadhani si mbaya lakini sio ambao unapaswa kumrudisha nyuma. Kwa tathmini yangu mimi amefanikiwa kwa miaka hii miwili kutengeneza mwelekeo fulani.”


“Kitakachofuata sasa hapa ni namna ya kuboresha utekelezaji wa yale tulioyaweka kwenye ilani ya uchaguzi, yale ambayo ni matumaini ya Watanzania na yale ambayo tuliwaahidi,” alisema.


Ajibu kauli ya Nyalandu CCM kupoteza mwelekeo
Akizungumzia kauli ya Nyalandu kuwa CCM imepoteza mwelekeo, Nape alisema kwake anadhani huo ni mtizamo wake na wala hataki kupuuza mtizamo wake huo wala kuubeza.


“Na mimi naamini CCM haijapoteza mwelekeo na mtakumbuka haya maneno Nyalandu sio wa kwanza kuyasema. Aliwahi kuyasema Horace Kolimba miaka hiyo na bado iko madarakani”


“Aliwai kusema Kingunge Ngombale Mwiru kuwa CCM imeishiwa pumzi na bado inapumua. Haya maneno ni mitizamo ya watu na Nyalandu anayo haki ya kuwa na mtizamo wake,”alisema.


“Alipotoka nilisema hivi kwamba aliibua hoja sita ukiacha hiyo ya kupoteza mwelekeo. Nikasema hizi hoja zote alizoziibua zinazungumzika ndani ya chama chetu. Angeweza tu kuzileta tukajadiliana”.


Kwa sababu ukisema CCM imepoteza mwelekeo ukaandika paper (mada) ukaja nayo ndani vikao uka justify (ukaitetea) ndio njia bora ya kurekebisha chama na sio kuondoka,”alisema na kuongeza;-


“Ndio maana alipoondoka mimi nika tweet nikasema kama yapo mapungufu ndani ya CCM nitayashughulikia nikiwa ndani ya CCM”


“Mimi katika utumishi wangu ndani ya CCM yako mengi sana ambayo nimeyasukuma ndani ya chama na yametokea ikiwamo kuibadili kabisa ile idara ya itikadi na uenezi”.


“Ninaamini katika kuleta mabadiliko. Kila mmoja kwenye nafasi aliyopewa akijitahidi kuleta mabadiliko fulani CCM itabadilika. CCM ya leo sio CCM ya jana”.


“Ndio maana kuna kauli mbiu CCM Mpya, Tanzania Mpya. Tunapotaka kuijenga Tanzania mpya ni pamoja na fikra na mawazo. CCM mpaka leo haina mbadala kwababu ya mfumo wake”.


Nape alisema Chadema wamejitahidi kujenga msingi chini lakini wameshindwa na chama chao kimebaki ngazi ya kitaifa zaidi lakini CCM ina uongozi hadi chini ngazi ya balozi na shina.


“Lakini CCM balozi wa nyumba kumi anajijua ni CCM na ndio nguvu ya CCM ilipo. Hata uwezo wa kupanga. Ukitaka kuiua CCM lazima uue mfumo wake jambo ambalo haliwezekaniki,”alisema.


“Kusema CCM inapoteza mwelekeo ghafla sio sawa lakini kusema hakuna mapungufu nayo sio sawa. Yapo mapungufu yanashughulikiwa na yanaweza kumalizwa na vikao na mfumo wa chama”


“Haya mapungufu ambayo pengine Lazaro aliyaona au wengine wanayaona dawa sio kuyakimbia. Dawa ni kukaa kuyashughulikia. Wewe mwenzetu unayeona yanakukera sana lete hoja”


Nape alitolea mfano walipoingia kuwa Katibu Mwenezi, kulikuwa na kitengo cha propaganda kilichokuwa kikiongozwa na watu waliotoka upinzani ambacho alitoa hoja kikabadilishwa.


“Hiki kitengo kilikuwa kinaongozwa na Tambwe Hiza. Moja ya jambo ambalo lilikuwa linanikera sana ni kitengo hiki kuwa na historia ya kuongozwa na watu waliotoka upinzani”


“Hili lilikuwa moja ya jambo lilikuwa linapeleka sura mbaya kule nje. Nilipoenda nikasema lazima tutoe hii. Tukaondoa propaganda tukatengeneza mawasiliano na umma”


“Tukaweka mawasiliano sio propaganda tu, kikaongozwa na Daniel Chongolo kwa muda mrefu tu na akakijengea heshima kubwa sana na ndio hapo tukarudisha mahusiano na vyombo vya habari”.


Nape alisisitiza kuwa endapo kuna mwana CCM anayeamini katika itikadi yake anayaona mapungufu fulani, ongeza nguvu ya kuleta hoja za mabadiliko ndani ya chama na sio kukimbia.


Chanzo: Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527