MUUZA DAWA ZA BINADAMU MATATANI KWA KUUA MTOTO AKIZALISHA MJAMZITO TABORA


Kijana muuza dawa za binadamu anayeishi Kijiji cha Mazira Kata ya Goweko, Igunga,Tabora, Shamsi Almasi (26) anashikiliwa na Polisi kwa tuhuma ya kusababisha kifo cha kichanga cha kike cha siku moja.

Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Grayston Mushi alithibitisha tukio hilo kutokea Novemba 8, 2017 saa 9 alasiri Kijiji cha Mazira, Kata ya Goweko. 

Alisema Maria Andrea, mjamzito anayeishi Kijiji cha Buhekela alipopatwa na uchungu alienda kwa huyo kijana Almasi kuzalishwa lakini bahati mbaya mtoto alitanguliza miguu kichwa kikabaki. 

Alisema kijana huyo baada ya kuona ameshindwa kumzalisha mama huyo mjamzito, aliamua kunyofoa kiwiliwili cha kichanga hicho na kuacha kichwa tumboni mwa mama.

Hata hivyo, alipoona hali hiyo alimwambia mume wa Maria, John Isanzule (37) ampeleke Hospitali ya Ndala kwa matibabu zaidi huku mama huyo akiwa hana fahamu. 

Aidha, Kamanda Mushi alisema baada ya kukamatwa na kuhojiwa na Polisi, iligundulika kijana huyo hana taaluma ya udaktari au ukunga wala uuguzi na upelelezi ukikamilika atafikishwa mahakamani.

Akizungumza kwa shida akiwa amelazwa wodi ya wazazi Hospitali ya Misheni ya Ndala, Maria alisema kijana aliyemzalisha alishindwa ndio maana alinyofoa kiwiliwili cha kichanga na kuacha kichwa. 

Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Misheni Ndala, George Mgalega amekiri kumpokea Maria akiwa hajitambui.

 “Ni kweli tulimpokea akiwa hajitambui na tulimfanyia upasuaji na kufanikiwa kutoa kichwa cha kichanga na hali yake inaendelea vizuri baada ya kupatiwa huduma zote zinazostahiki,” alieleza.

Imeandikwa na Lucas Raphael- Habarileo Igunga
Theme images by rion819. Powered by Blogger.