MAHAKAMA YAAMURU MKUU WA WILAYA AKAMATWE

Mahakama ya Hakimu Mkazi Bukoba imetoa hati ya kumkamata na kumfikisha mahakamani Mkuu wa Wilaya ya Misenyi, Dennis Mwira kwa kosa la kupuuza amri ya Mahakama.

Amri hiyo imetolewa Novemba 2 na Hakimu Mkazi, Samuel Maweda baada ya mkuu huyo wa wilaya kukaidi amri ya kuachia ng'ombe 541 wa wafugaji wa kitongoji cha Rwenkuba wilayani humo waliokamatwa isivyo halali.

Septemba 22, mahakama hiyo ilitoa amri ya ng'ombe hao kuachiwa baada ya wananchi kufungua shauri la madai namba 21/2017 kupinga ng'ombe wao kukamatwa katika eneo lenye mgogoro unaoendelea katika mahakama kuu kitengo cha ardhi kwa shauri namba 14/2017.

 Wakili wa wananchi143 waliofungua kesi mahakamani, Danstan Mutagahywa  Alhamisi alisema baada ya Mkuu wa Wilaya na mdaiwa mwenzake, Ladislaus Martin ambaye ni Meneja wa Ranchi ya Misenyi baada ya kukaidi kutekeleza amri hiyo, waliwasilisha ombi la watu hao kukamatwa kwa kudharau amri ya Mahakama.

"Siyo tu wamekaidi kutekeleza amri halali ya Mahakama, DC na mwenzake pia wamegoma kupokea hati za wito na kufikia hatua ya kumkamata na kumweka mahabusu dalali wa Mahakama aliyepewa amri ya kutekeleza zoezi la kurejesha ng'ombe wanaoshikiliwa isivyo halali," alisema Mutagahywa.

Alisema amri hiyo ilitarajiwa kufikishwa ofisini kwa Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa (RCO), wa Kagera jana  Ijumaa Novemba 3.

Alimtaja dalali wa Mahakama aliyekamatwa na kuswekwa mahabusu kwa amri ya DC Oktoba 31, kuwa ni Ignatus Bashemela aliyeachiwa huru baada ya yeye kuwasilisha suala hilo ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera akionyesha nyaraka halali za Mahakama kuhusu jambo hilo.

Wakati shauri la madai dhidi ya DC na mwenzake Ladislaus likitarajiwa kusikilizwa mara watakapokamatwa na kufikishwa mbele ya mahakama, ile ya ardhi ambayo bado inatajwa mbele ya Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba, Seif Musa, itatajwa tena Machi 8, 2018.

Kauli ya Mkuu wa Wilaya
Akizungumza kwa njia ya simu mkuu huyo wa wilaya amesema aliagiza kukamatwa kwa dalali wa wafugaji wa ng'ombe kutoka Uganda ambaye alifika bila kutoa taarifa yoyote kwa mamlaka za Serikali.

Alisema kuwa mtu huyo alikwenda moja kwa moja katika eneo wanapotunzwa ng'ombe zaidi ya  80 walioingizwa nchini kutoka Uganda bila kufuata utaratibu.

"Hilo suala la dalali wa Mahakama nalisikia kwako niliyeagiza akamatwe ni dalali wa wafugaji wa ng'ombe kutoka Uganda ambao tumewakamata alifika bila kufuata taratibu nikaagiza akamatwe,"amesisitiza Kanali Mwila.

Ameongeza kuwa alikamata ng'ombe zaidi ya 400 na wamiliki wake kutoka Uganda walilipa faini na kuwarudisha kwao na kubaki ng'ombe 88 aliosema alipata taarifa kuwa wanataka kuchukuliwa kwa nguvu na watu ambao hata hawakupita kwenye ofisi yake.

Pia alisema hana taarifa yoyote ya kuwepo kwa hati ya Mahakama dhidi yake na kuwa anaendelea kuwasaka raia wawili wanaodaiwa kushirikiana na wafugaji wa Uganda kuingiza mifugo hiyo bila utaratibu.

Chanzo- Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527